Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa ulinzi wa amani nchini Ghana Desemba kupiga jeki walinda amani

Mkutano wa Mawaziri wa Mkutano wa ngazi za juu siku zijazo.
UN Photo/Laura Jarriel
Mkutano wa Mawaziri wa Mkutano wa ngazi za juu siku zijazo.

Mkutano wa ulinzi wa amani nchini Ghana Desemba kupiga jeki walinda amani

Amani na Usalama

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa ngazi ya mawaziri kuhusu ulinzi wa amani utafanyika mwaka huu mjini Accra, Ghana, tarehe 5-6 Disemba, Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa na Jamhuri ya Ghana zilitangaza leo.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York, Marekani waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kikanda wa Ghana, Shirley Ayorkor Botchwey, akiambatana na maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa, amesema mkutano huo wa kila baada ya miaka miwili utasaidia kupata uungwaji mkono wa kisiasa unaohitajika na kutoa ahadi za kuimarisha ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa kulingana na mpango wa kuchukua hatua kwa ajili ya ulinzi wa amani na A4P+ ambao ni mkakati wa utekelezaji wa mwaka 2021-2023.

Mmoja wa mapolisi wa awali kutoka Ghana kwenda kuhudumu chini ya Polisi wa Umoja wa Mataifa na hapa ni mji wa Leopoldiville huko Congo mwaka 1960. Sasa Leopoldville ni Kinshasa ya DRC.
UNPOL
Mmoja wa mapolisi wa awali kutoka Ghana kwenda kuhudumu chini ya Polisi wa Umoja wa Mataifa na hapa ni mji wa Leopoldiville huko Congo mwaka 1960. Sasa Leopoldville ni Kinshasa ya DRC.

Mkutano wa kwanza kufanyika barani Afrika

Huu utakuwa ni mkutano wa tano wa mawaziri wa Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi wa amani na wa kwanza kufanyika barani Afrika.

Mkutano huo unaangazia kupata ahadi madhubuti kutoka kwa nchi wanachama kushughulikia mapungufu muhimu, kutumia teknolojia mpya na kushughulikia vipaumbele muhimu ili kuboresha ufanisi wa utendaji wa operesheni za kulinda amani.

Huku kukiwa na changamoto na vitisho ambavyo havijawahi kushuhudiwa na operesheni hizo, mkutano wa mwaka huu utachunguza maswala muhimu kama vile ulinzi wa raia, mawasiliano ya kimkakati, kupinga upotoshaji, usalama, afya ya akili ya walinzi wa amani na jukumu muhimu la wanawake katika kudumisha amani.

"Kama nchi mchangiaji wa muda mrefu wa polisi katika operesheni za amani za Umoja wa Mataifa tangu miaka ya 1960, Ghana inatambua rekodi ya muda mrefu na chanya ya ulinzi wa amani barani Afrika na inaamini kwamba ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa una mustakabali na unabaki kuwa wa lazima na wa thamani sana katika kuendeleza amani nchini humo na katika maeneo ya migogoro duniani. Kwa hiyo ni muhimu kwamba dunia ibakie imara katika dhamira yetu ya pamoja ya kulinda chombo hiki cha kimataifa na kuunga mkono kikamilifu mipango ya Katibu Mkuu kama vile hatua kwa ajili ya ulinzi wa amani na A4P+, ambayo ni muhimu katika kuboresha ufanisi wa kudumisha amani ya kisasa na kufikia usalama na kutatua changamoto za zama zetu,” amesema waziri wa Ghana.

Wanawake walindamani wa Ghana wakiwa wamepelekwa Lebanon kama sehemu ya operesheni ya ulinzi wa amani ya UNIFIL
UNIFIL/Pasqual Gorriz
Wanawake walindamani wa Ghana wakiwa wamepelekwa Lebanon kama sehemu ya operesheni ya ulinzi wa amani ya UNIFIL

Weka ahadi za kudumisha amani

Jean-Pierre Lacroix, mkuu wa operesheni za ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa amesema "Ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ni ushirikiano wa kimataifa, na walinda amani kutoka zaidi ya nchi 120 wametumwa katika baadhi ya maeneo magumu zaidi duniani ili kuokoa maisha, kuzuia migogoro na kujenga mazingira ya amani endelevu. Mkutano wa 2023 ni fursa muhimu kwa viongozi kuthibitisha kujitolea kwao na kutoa ahadi kwa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa, ambao unasalia kuwa mojawapo ya zana muhimu za kimataifa kwa ajili ya kufikia amani na maendeleo endelevu. Tunaishukuru Ghana kwa kuandaa mkutano huu wa mawaziri na kwa michango yake muhimu katika kuimarisha shughuli zetu.”

Nchi Wanachama pia zinahimizwa kuunda au kuimarisha msaada na ushirikiano baina ya nchi na pembetatu ili kuhakikisha kuwa maboresho yanayopendekezwa ni endelevu na yana matokeo yanayohitajika.

Atul Khare, naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa msaada wa uendeshaji
UN Photo/Mark Garten
Atul Khare, naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa msaada wa uendeshaji

Akiangazia umuhimu wa mkutano wa mawaziri wa Afrika na ule wa ushirikiano, Atul Khare, naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa msaada wa uendeshaji amesema "Michango ya Ghana na Afrika katika ulinzi wa amani ni zaidi ya michango ya askari ili kutoa jukwaa muhimu ambalo nchi zinaweza kuungana na kushirikiana katika mikakati bunifu ya kushughulikia changamoto za sasa na kujadili mustakabali wa ulinzi wa amani. Ninatazamia kuunda ushirikiano kati ya washiriki ili kuboresha ufanisi wa walinda amani wetu, kuinua ubora wa huduma zao za matibabu na kuendeleza operesheni rafiki kwa mazingira.”

Naye Catherine Pollard msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia idara ya mikakati ya usimamizi, sera na uzingatiaji amesema "Mbali na changamoto nyingi zinazokabili kwa sasa, oparesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa pia zinajikuta katika wakati muhimu wa kuzuia na kushughulikia utovu wa nidhamu kama sehemu muhimu ya utendaji. Hii ni juhudi ya pamoja."