Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zama za kufumbia macho ukatili wa kingono zimepita- Guterres

Mjini Gao,  nchini Mali, walinda amani wa UN wakiwa katika doria za kila siku kuhakikisha amani na utulivu kwenye eneo hilo.
MINUSMA/Marco Dormino.
Mjini Gao, nchini Mali, walinda amani wa UN wakiwa katika doria za kila siku kuhakikisha amani na utulivu kwenye eneo hilo.

Zama za kufumbia macho ukatili wa kingono zimepita- Guterres

Amani na Usalama

Suala la amani na usalama barani Afrika leo tena limepatiwa kipaumbele katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo wajumbe wamejikita zaidi katika kuangazia operesheni za ulinzi wa amani barani humo.

Akihutubia wajumbe kwenye mkutano  huo uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema kuwa walinda amani wako tayari kulipa gharama ya amani na Umoja wa Mataifa una deni kubwa.

Amegusia gharama wanayolipa walinda amani ikiwa ni  pamoja na kifo akitolea mfano tukio la wiki iliyopita ambapo walinda amani kutoka Tanzania na Malawi waliuawa wakiwa kwenye operesheni za ulinzi wa amani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

“Wengi wao walikuwa wanajaribu kuepusha shambulio kwenye mji wa Beni huko jimboni Kivu Kaskazini, nchini DRC na kuweka mazingira salama kwa wale wanaoendesha operesheni dhidi ya mlipuko wa Ebola,” amesema Katibu Mkuu na kutumia fursa hiyo kuwaomba wajumbe kusimama kwa dakika moja kukumbuka walinda amani hao.

Kisha akamulika bara la Afrika akisema kuwa kati ya operesheni 14 za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, 7 ziko Afrika na kama hiyo haitoshi zaidi ya asilimia 80 ya walinda amani wanatoka barani  humo, huku theluthi mbili ya walinda amani wote wa kike wanatoka Afrika.

Hata hivyo amesema ulinzi wa amani barain Afrika unaendelea kuwa changamoto kubwa zaidi kwa chombo hicho chenye wanachama 193, akitaja miongoni mwa changamoto hizo ni kulinda amani katika mazingira hatarishi zaidi.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kilichokutana kujadili ulinzi wa amani barani Afrika
UN /Rick Bajornas
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kilichokutana kujadili ulinzi wa amani barani Afrika

“Kwenye maeneo hayo ya ulinzi wa amani, uhalifu wa kuvuka mipaka unafanyika, kuna vikundi lukuki vilivyojihami, vikundi vya kigaidi navyo vinatishio kubwa zaidi na wakati mwingine vinalenga moja kwa moja walinda amani,” amesema Katibu Mkuu.

Amegusia pia changamoto ya ukatili wa kingono kwenye operesheni hizo za ulinzi wa amani akisema tayari wanachukua hatua kuhakikisha kuna usaidizi kwa manusura wa vitendo hivyo ambavyo vinatekelezwa na baadhi ya walinda amani.

“Tumeimarisha mafunzo yetu na kuongeza uchunguzi. Makumi kadhaa ya viongozi wa dunia wamejiunga na kikundi cha viongozi cha kuunga mkono utekelezaji wa sera ya kutovumilia kabisa ukatili wa kingono, nan chi 100 zimetia saini makubaliano ya hiari na Umoja wa Mataifa ya kushughulikia suala hili,” amesema Bwana Guterres.

Katibu Mkuu amesema zama za ukimya na kuona suala hili ni haramu kuzungumza, zimepita na zama za kuwajibika zimeanza.

Bwana Guterres amesema ili kukabili changamoto hizo za utendaji kwenye operesheni za ulinzi wa amani ambazo Umoja wa Mataifa unashirikiana vyema na Muungano wa Afrika, AU ni vyema Baraza la Usalama likachukua hatua.

“Ni muhimu operesheni hizi zinazoongozwa na AU zipatiwe mamlaka thabiti, zinazotambulika, endelevu na pia fedha ili ziweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa kuimarisha ufanisi wa ulinzi wa amani Afrika ni  jukumu la pamoja.

Ametamatisha kwa kusema kuwa wataendelea kushughulikia changamoto hizo kwa kushirikiana na wadau wao barani Afrika na duniani kote kwa ujumla.

Askari wa kike walinda amani kutoka Afrika Kusini wa kikosi cha  MONUSCO nchini DRC washika doria Mavivi Beni.
MONUSCO/Michael Ali
Askari wa kike walinda amani kutoka Afrika Kusini wa kikosi cha MONUSCO nchini DRC washika doria Mavivi Beni.