‘Jicho kwa jicho, huacha kila mtu kipofu’ – Makamu wa Rais wa Tanzania katika UNGA 78
‘Jicho kwa jicho, huacha kila mtu kipofu’ – Makamu wa Rais wa Tanzania katika UNGA 78
Msemo wa wahenga, “Jicho kwa jicho huacha kila mtu kipofu” umepata nafasi katika ukumbi maarufu wa kihistoria wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa nchini Marekani pale ambapo Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango ameutumia msemo huo akisisitiza amani ulimwenguni alipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa saa za jioni jijini New York.
“Tunatoa wito kwa pande zinazopigana duniani kote kunyamazisha bunduki na makombora yao na kutoa umuhimu kwa amani. Tutendeane kwa unyenyekevu, si kwa majivuno. Hebu tuzingatie hekima ya zamani inayosema, "jicho kwa jicho, huacha kila mtu kipofu". Amesema Dkt. Mpango akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan ambaye “ametingwa na shughuli nyingine muhimu za kitaifa” nyumbani Tanzania.
Tanzania na ulinzi wa amani
Tanzania inaendelea kujitolea kikamilifu na tayari kushirikiana na familia ya Umoja wa Mataifa katika kudumisha amani na usalama duniani ili kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi, si kwetu tu bali muhimu zaidi kwa vizazi vijavyo, ameeleza Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Tanzania kupitia hotuba yake ya takribani dakika 15 kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Bwana Mpango amesema Tanzania inaamini kwa dhati kwamba dunia inahitaji kuwekeza zaidi katika mazungumzo na diplomasia ili kuzuia na kutatua migogoro ya kivita. “Vita na makabiliano lazima viepukwe kwa gharama yoyote kwa sababu katika vita kila mtu hushindwa, ikiwa ni pamoja na pande zisivyopigana.”
Kwa maana hiyo, Tanzania ina na itaendelea kuchangia katika juhudi za kuleta amani na kudumisha amani barani Afrika na kwingineko duniani. Hadi kufikia Machi 2023, Tanzania ilisimama kama mchangiaji mkubwa wa 12 kati ya nchi 125 katika shughuli za Umoja wa Mataifa za kulinda amani. Tanzania inaitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza uungaji mkono katika mipango ya kikanda ya kuleta amani katika maeneo yenye vita katika bara la Afrika.
Wachochea migogoro
Makamu huyo wa Rais wa Tanzania kwa uwazi kabisa amepeleka ujumbe kwa ulimwengu akisema, "Wale wanaoshiriki katika kuchochea migogoro barani Afrika ama kwa madhumuni ya kufaidika na biashara ya silaha au kupata utajiri wa ‘madini ya damu’ wanapaswa kufuatiliwa na kulaaniwa kwa uwazi na Umoja wa Mataifa."
Kuhusu Ugaidi
Dkt. Mpango amesema Tanzania imeimarisha uwezo wa kukabiliana na ugaidi unaovuka mipaka, “kwa kufanya kazi na majirani zetu na washirika wa kimataifa, hasa kwa kubadilishana taarifa na mikakati.”
Hotuba ya Makamu wa Rais wa Tanzania imegusia pia masuala mengine muhimu kama Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs na Mabadiliko ya tabianchi.
“Sisi, jumuiya ya kimataifa lazima tuchukue hatua kwa uharaka. Tanzania pia inasisitiza wito wake wa mabadiliko ya haki ya nishati safi kwa Afrika.” Amesema Dkt. Mpango.
Kutazama hotuba nzima ya Dkt. Philip Isdor Mpango bofya