Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuaminiane na tushikamane kwa dhati bila ajenda ya siri- Rais Ndayishimiye

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
UN Photo/Cia Pak
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Tuaminiane na tushikamane kwa dhati bila ajenda ya siri- Rais Ndayishimiye

Ukuaji wa Kiuchumi

Kuaminiana na mshikamano kunapaswa kuwa msingi ambamo kwayo ushirikiano wa kimataifa usio na ukosefu wa usawa na mizozo unastawi, amesema Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo. 

Amesema ni kwa kutambua hilo ndio maana Burundi kwanza kabisa inajenga mambo hayo mawili kwenye ngazi ya taifa ili kuchipusha na kuimarisha mambo hayo mawili miongoni mwa wananchi wake. 

Kuaminiana na mshikamano vinasongesha SDGs 

“Baada ya miaka ya ukosefu wa utulivu, mchakato wa ukweli na maridhiano ulianza Burundi na sasa unazaa matunda dhahiri,” amesema Rais huyo akihutubia mjadala huo wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu, UNGA78. 

Amesema warundi hivi sasa kuaminiana na mshikamano ndio vinachochea ufanikishaji na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. 

“Ni kwa mantiki hiyo tunatoa wito kwa nchi wadau na marafiki kusaidia hatua za serikali ya Burundi na kwa dhati tunahamasisha uwekezaji kutoka nje,”ametanabisha Rais Ndayishimiye. 

Misaada rasmi kwa serikali yaelekezwa kwingineko 

Hata hivyo amesema jambo la kusikitisha ni kwamba misaada rasmi ya maendeleo inayopaswa kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikishia ustawi wananchi wake imepungua huku ikielekezwa zaidi kwa vikundi visivyo vya kiserikali akidai vyenye ajenda ya kisiri ya kiuchumi na kisiasa kwa maslahi ya nchi hisani. 

Rais Ndayishimiye amesema mshikamano wa kimataifa unapaswa kuhamasisha kwa uwazi nchi tajiri kutoa michango ya kina ya juhudi za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi zenye maendeleo duni zaidi duniani, LDCs. 

Amenukuu msemo wa kirudi, "ntawutungira mu boro", ukimaanisha ustawi utakuwa endelevu iwapo utashirikisha watu wote, akisema unakumbusha ya kwamba “kuwekeza kwenye ustawi wa Jirani, kwa hakika kunatoa hakikisho la usalama na uendelevu wa maendeleo ya mtu mwingine.” 

Hivyo amekumbusha udharura wa kufikiria upya na kuimarisha ubia wa kimataifa, ambao amesema kwa mtazamo wake unahusisha unafuu kwenye madeni, kuongeza fungu la fedha la kukabiliana na umaskini, kuimarisha ushirikiano wa nchi za kusini na kushirikishana teknolojia na ubunifu, halikadhalika kupanua wigo wa mikataba ya biashara.