Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC uchaguzi mkuu kufanyika mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyopangwa

Rais Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akihutubia UNGA78
UN/ Cia Pak
Rais Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akihutubia UNGA78

DRC uchaguzi mkuu kufanyika mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyopangwa

Amani na Usalama

Uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC utafanyika kama ilivyopangwa mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 na wakati  huo huo tunaomba kutekelezwa kwa ombi letu la kuongeza kasi ya kuondoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Ni miongoni mwa mambo aliyozungumzia Rais wa DRC Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo  wakati akihutubia mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa, UNGA78 jijini New York, Marekani jioni ya Jumatano Septemba 20, 2023.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwajulisha kuwa uchaguzi wa Rais hadi madiwani utafanyika mwishoni mwa mwaka huu na tayari Tume Huru ya Uchaguzi nchini DRC, CENI imeshachapisha orodha ya wagombea wa uchaguzi wa ngazi ya kitaifa, majimbo na manispaa,” amesema Rais Tshisekedi.

Taratibu sasa zinaendelea kuhakikisha kuna uwazi, ujumuishi, fursa sawa na uhalali wa chaguzi hizo zijazo.

Zaidi ya yote, mialiko, amesema imepelekwa kwa mashirika ya kimataifa, ya kiraia na taasisi za kimataifa zinazohusika na masuala ya uangalizi wa uchaguzi halikadhalika kusaidia DRC kufanikisha tukio hilo la kidemokrasia.

Ameshukuru wadau, ukiwemo Umoja wa Mataifa ambao amesema wanasaidia kufanikisha mchakato huo adhimu.

Zingatieni barua ya kasi ya kuondoka kwa MONUSCO

Kuhusu ulinzi wa amani ametaka Umoja wa Mataifa kuzingatia barua ya DRC kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya tarehe Mosi mwezi Septemba mwaka huu inayotoa ombi la kuongeza kasi ya kuondoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu wa 2023 badala ya Desemba 2024.

“Ombi letu hilo linazingatia kwamba kuondoka kwa MONUSCO kutaondoa mvutano na sintofahamu ya sasa kati yake na wananchi. Lakini tayari nimeagiza maafisa wangu kuwa na mazungumzo na UN ni kwa vipi ushirikiano wetu uendelee.

Suala la ulinzi wa amani tunaomba lisalie kuwa mamlaka ya DRC, amesema Rais Tshisekedi akitanabaisha kuwa uwepo wa MONUSCO kwa takribani miongo miwili sasa haujaweza kukomesha vikosi vya waasi au mauaji ya raia.

Amehoji pia kile alichosema undumilakuwili hasa wa Baraza la Usalama la UN kuhusu ushughulikiaji wa mizozo ikiwemo huo wa Mashariki ya DRC, Kaskazini mwa Msumbiji jimboni Cabo Delgado na Sudan.

Soma hotuba nzima hapa  na unaweza kupata video hapa