Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama latoa wito kufanyike uchaguzi wa amani DRC

Mabango ya kampeni za uchaguzi DRC
MONUSCO/M. Asmani
Mabango ya kampeni za uchaguzi DRC

Baraza la Usalama latoa wito kufanyike uchaguzi wa amani DRC

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema uchaguzi wa Desemba 23, mwaka huu 2018 ni ishara ya uhuru wa watu na serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC na ni fursa muhimu katika historia kama uchaguzi wa kwanza unaozingatia demokrasia na ubadilishanaji wa mamlaka kwa amani DRC, na kwamba ni fursa ya kujenga msingi wa amani na kuweka mazingira kwa ajili ya maendeleo ya nchi hiyo.

Kupitia taarifa ya Baraza hilo iliyotolewa na rais wake mwezi huu, balozi Kacou Houadja Léon Adom wa  Côte d’Ivoire, wanachama wamekaribisha maandalizi ya vifaa vya uchaguzi lakini wameelezea wasiwasi wao kuhusu kampeni za uchaguzi ambazo zimesababisha watu kupoteza maisha na uharibifu mwingine.

Kwa mantiki hiyo wanachama wa Baraza la Usalama wametolea wito serikali ya DRC kuchunguza visa hivyo na kukumbusha wito wao kwa serikali na upinzani kuzingatia amani wakati wa mchakato wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi wa wazi, wenye amani na kuaminika na pia kuzingatia usalama wa DRC na ukanda mzima.

Baraza la Usalama limesisitiza umuhimu wa wanasiasa kuzingatia uhuru wa kujielezea, kujumuika na kukampeni ambavyo ni vigezo vya mchakato wa kidemokrasia unaozingatia matakwa ya watu. Aidha imewataka wanasiasa na taasisi za uchaguzi kuhakikisha mchakao wa amani ambao utapelekea makabidhiano ya mamlaka kwa njia ya amani kwa mujibu wa katiba ya DRC na makubaliano ya Desemba 31, 2016.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.