Hii ni siku ya kihistoria: Tamko la kisiasa kuhusu kuzuia, kujiandaa na kukabiliana magonjwa ya mlipuko
Hii ni siku ya kihistoria: Tamko la kisiasa kuhusu kuzuia, kujiandaa na kukabiliana magonjwa ya mlipuko
Viongozi na wadau wa afya wamepokea kwa furaha dhamira ya leo ya "kihistoria" iliyooneshwa na viongozi wa kimataifa, kwenye Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, walipoidhinisha tamko la kisiasa kuhusu kuzuia, kujiandaa na kukabiliana magonjwa ya mlipuko.
WHO
Akizungumza wakati wa mkutano wa ngazi ya juu mjini New York, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amewashukuru Rais na nchi zote Wanachama wa Baraza Kuu, akisema "hii ni siku ya kihistoria" .
Tedros ameendelea akisema, "Tunaweza kujaribiwa kufikiria kuwa janga la coronavirus">COVID-19 ni historia. Lakini historia inatufundisha kwamba coronavirus">COVID-19 haitakuwa janga la mwisho. Swali tunalokabiliana nalo sote ni ikiwa tutakuwa tayari majanga mengine yatakapotufika. Kama viongozi, tuna wajibu wa pamoja kuhakikisha tuko tayari.”
Mkuu huyo wa WHO ameongeza, “Tuna jukumu la pamoja kulinda jamii na uchumi wetu. Tamko la kisiasa ambalo mmekubaliana hivi punde leo ni ahadi ambayo kwa pamoja, tutatekeleza wajibu wetu.”
Baada ya mkutano huo, akizungumza na waandishi wa habari, Tedros amesema nyaraka hiyo "ni ishara thabiti kutoka kwa nchi kwamba zimejitolea kujifunza somo la janga la COVID-19 na kuimarisha ulinzi wa ulimwengu dhidi ya milipuko ya magonjwa."
"Kwa muda mrefu sana, ulimwengu umekuwa ukifanya kazi kwa mzunguko wa hofu na kutelekezwa," ameongeza.
Rais UNGA78
Wakati wa mkutano huo, Rais wa Baraza Kuu, Dennis Francis, amesema, “Kusema ukweli, hatukuwa tayari kwa shambulio kama hilo. Tunapojiweka sawa tena, inatupasa kwamba masomo magumu ambayo tumejifunza kutokana na janga hili yanatutaka kufanya vyema zaidi. Tunaweza - na ni lazima - kuepuka vifo vinavyoweza kuzuilika na msukosuko wa kiuchumi wa kimataifa wa idadi kubwa tuliyoshuhudia wakati wa COVID-19."
Naibu Katibu Mkuu UN
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohamed, pia ameshiriki katika mkutano huo, akibainisha kwamba mwitikio wa kimataifa kwa COVID-19 ni "hadithi ya werevu wa kibinadamu na kushindwa kwa binadamu."
Ameongeza, "Kwa upande mmoja - vipimo vilivyoundwa kwa kasi ya radi, na chanjo zilizotengenezwa katika muda mfupi uliovunja rekodi. Kwa upande mwingine, ukosefu wa maandalizi, walio hatarini waliathiri vibaya zaidi, na chanjo zilizohifadhiwa na nchi tajiri, kwani watu katika mataifa maskini walikosa.
"Hatupaswi kurudia makosa ya zamani wakati janga linalofuata linapiga - kama tunavyojua litafanya - na vitisho vingine vya afya vinaibuka. Hiyo inamaanisha kufanya kazi kwa pamoja,” amesema Naibu Katibu Mkuu.
Mwenyekiti Mwenza wa Zamani wa Jopo Huru la Maandalizi na Majibu kwa milipuko ya magonjwa, Helen Clark, ameongeza, "Kwa hivyo, virusi ambavyo hatukujua kuhusu miaka minne iliyopita vimeingia ulimwenguni kote kwa gharama kubwa kwa watu, jamii na kwa serikali. Tamko la kisiasa ambalo mmekubaliana hivi punde lazima liwe kichocheo cha mabadiliko ambayo yanazuia hili kutokea tena."
Tamko hilo la kisiasa lilitokana na mazungumzo chini ya uongozi mahiri wa Mabalozi Gilad Erdan wa Israel na Omar Hilale wa Morocco. Nyaraka ya makubaliano sasa itapelekwa katika Baraza Kuu ili ili kuidhinishwa na Mkutano Mkuu.