Siku ya amani duniani, shule ya sekondari Viwandani, Dodoma Tanzania wapanda miti 

21 Septemba 2021

Nchini Tanzania katika kuadhimisha siku ya amani duniani, wadau mbalimbali kwa kushirikiana na ofisi ya Umoja Umoja wa Mataifa nchini humo, wameiadhimisha siku hii kwa kupanda miti katika shule ya sekondari Viwandani iliyoko mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanachangia kuondoa amani katika baadhi ya maeneo duniani.

Muhammed Said ni mmoja wa wanafunzi walioshiriki tukio hilo anasema, “katika suala zima la kupokea siku ya amani duniani, kwanza tumefurahi na ni furaha kubwa lakini vilevile ni upendo ambao umeoneshwa na watu kutoka sehemu mbalimbali. Sisi kama wanachama wa ‘Club’ ya mazingira tunaweza tukatembelea shule jirani yetu ya Makole katika suala zima la kwenda kudumisha usafi na kuwafariji wagonjwa katika suala la kudumisha amani.” 

Malik Masoud ni mwalimu katika shule hiyo ya sekondari Viwandani anasema, “kwangu mimi ni faraja kwa sababu yale ambayo tunawafundisha wanafunzi kila siku darasani kuhusiana na amani leo hii wameyaona kwa vitendo na kupitia maelezo waliyoyapata kutoka kwa wageni wameamini kweli kuna haja ya kuadhimisha amani duniani kwa sababu tunaamini kabisa kwamba panapokuwa na amani ndio kunakuwa na utulivu na usalama wao wenyewe wanafunzi na wamegundua kwamba amani inawasaidia wao kusoma salama kwa hiyo kama wanafunzi wataenda kuwa mabalozi wema. Kwetu pia kupanda miti ni zawadi kubwa. Miti inaishi. Ina uwezo wa kuishi miaka 100. Itazidi kuifanya dunia kuwa salama kwa viumbe hai."

TAGS : Siku za UN, Siku ya amani duniani, Tanzania, Mazingira 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter