Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante UNICEF, sasa kuoga si tatizo tena- Mwanafunzi Malawi

Noria Kanyama, mwanafunzi huyu wa shule moja ya msingi wilaya ya Chikwawa, mkoa wa Kusini nchini Malawi.
UNICEF Malawi
Noria Kanyama, mwanafunzi huyu wa shule moja ya msingi wilaya ya Chikwawa, mkoa wa Kusini nchini Malawi.

Asante UNICEF, sasa kuoga si tatizo tena- Mwanafunzi Malawi

Afya

Nchini Malawi, hofu ya wanafunzi wa kike kunuka wakati wakiwa kwenye hedhi kutokana na uhaba wa maji shuleni kwao imepatiwa jawabu baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, kufunga kisima cha maji kinachotumia nishati ya sola kuvuta maji kutoka ardhini. 

Noria Kanyama, mwanafunzi huyu wa shule moja ya msingi wilaya ya Chikwawa, mkoa wa Kusini nchini Malawi akikumbuka siku ambayo mafuriko yalikumba eneo lao. Anasema ililazimu wakimbilie maeneo ya mwinuko ambako ndiko aliko hivi sasa. 

Anasema, hapa ndipo tulalapo, mimi, mama yangu na wadogo zangu watatu. Pahala penyewe ni chumba kimoja na kidogo. 

Vimbunga ikiwemo Idai na Fredy vilisambaratisha miundombinu ya maji kwenye eneo lao.

Kwa hiyo kando ya zahma ya malazi, ni zahma ya maji, akisema walitembea mwendo mrefu kwenda kuteka maji mtoni ambapo walitumia saa moja kwenda na kurudi. 

Noria Kanyama, mwanafunzi huyu wa shule moja ya msingi wilaya ya Chikwawa, mkoa wa Kusini nchini Malawi.
UNICEF Malawi
Noria Kanyama, mwanafunzi huyu wa shule moja ya msingi wilaya ya Chikwawa, mkoa wa Kusini nchini Malawi.

Maji yenyewe anasema hayakuwa masafi na si salama na watu wengine waliugua kuhara kwa kunywa maji hayo. Lakini zaidi ya yote, “Ninapokuwa kwenye hedhi, wavulana shuleni huwa wanatucheka. Wanasema wasichana wananuka, wako kwenye hedhi. Hii inatufanya tusiende shuleni, tunabakia nyumbani hadi tumalize hedhi. Hii inatuacha nyuma kwa sababu wenzetu wanaendelea na masomo wakati sisi tuko nyumbani.” 

UNICEF kwa kutambua zahma hii imejenga kisima cha maji kinachotumia nishati ya sola kusukuma maji kutoka ardhini, kisima kinachohudumia watoto 504 na familia zao. 

Sasa Noria mwenye umri wa miaka 14 anasema, “Ujio wa kisima hiki umebadili maisha yangu mno. Kuoga si tatizo, halikadhalika maji ya kunywa. Magonjwa nayo yametoweka. Tunapenda kuwashukuru wale waliotuletea hii huduma ya maji. Kinachonifurahisha zaidi mama yangu ananiruhusu niende shuleni. Ndoto yangu ni kuwa daktari.”