Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mambo 5 unayopaswa kufahamu kuhusu Fistula: UNFPA 

Watalaam, hudumu za kiafya wakati wa ujauzito na kujifungua zinaweza kuzuia Fistula.
© UNFPA Mozambique
Watalaam, hudumu za kiafya wakati wa ujauzito na kujifungua zinaweza kuzuia Fistula.

Mambo 5 unayopaswa kufahamu kuhusu Fistula: UNFPA 

Afya

Fistula itokanayo na uzazi ni nini? 

Ni jeraha kubwa la wakati wa kujifungua ambalo humpokonya mwanamke au msichana afya yake, haki na utu.  

Ni shimo linalotokea kati ya njia ya uzazi na kibofu ambayo husababisha kutoweza kudhibitiwa kwa mkojo.  

Pia ni shimo kati ya njia ya uzazi na njia ya haja kubwa husababisha kinyesi kuvuja bila kujizuia.

Kwa nini hutokea  

Hutokana na mama kuugua uchungu kwa muda mrefu kabla ya kujifungua.  

Shinikizo la muda mrefu litokanalo na kichwa cha mtoto kwenye njia ya uzazi ya mama hukata usambazaji wa damu, na kusababisha mishipa kufa na kuanguka na baada ya kuanguka shimo linalojitokeza linaitwa fistula.  

Fistula ya uzazi inachangia asilimia 8% ya vifo vya uzazi, na asilimia 90%  ya visa vya kujifungua watoto wafu. 

Inawaathiri kina nani na inatokea wapi?  

Inakadiriwa kuwa wanawake na wasichana 500,000 katika nchi zaidi ya 55 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia na Pasifiki, nchi za Kiarabu, Amerika Kusini na Caribbea wanakadiriwa kuishi na fistula, huku maelfu zaidi ya visa vipya hutokea kila mwaka. 

Haya ndio mambo 5 ya kufahamu kuhusu Fistula 

1. Kuna aina tofauti za fistula  

Ingawa aina ya kawaida ni shimo kubwa kati ya njia ya uzazi na kibofu cha mkojo (inayoitwa vesicovaginal fistula), aina nyingine ni pamoja na: 

Fistula ya Rectovaginal: Shimo kati ya njia ya uzazi na rsehemu ya haja kubwa 

Fistula ya urethrovaginal: Shimo kati ya njia ya uzazi na mrija wa kupitisha mkojo Urethra ambayo hubeba mkojo kutoka kwenye kibofu hadi nje ya mwili 

Fistula ya Ureterovaginal: Shimo kati ya mirija ya uzazi ya kupeleka mkojo kwenye kibofu na njia ya uzazi. 

Vesicouterine fistula: Shimo kati ya kibofu na mfuko wa uzazi au uterasi 

Baadhi ya fistula husababishwa na taratibu za uzazi kama vile upasuaji na sehemu kutokana na huduma duni za afya na mafunzoau ujuzi mdogo wa upasuaji. Hii huitwa fistula ya iatrogenic. 

Lakini pia kuna Fistula ya kiwewe ambayo husababishwa na ukatili wa kingono haswa katika maeneo yenye migogoro, uharibifu wa uke unachukuliwa kuwa jeraha la vita. 

2. Madhara ya kimwili, kijamii na kisaikolojia ni makubwa sana. 

Maisha ya wanawake walio na hali hiyo yanaelezwa kuwa ni ya mateso ya muda mrefu ya kimwili na kihisia. 

Hali hiyo inaweza kusababisha maambukizi, vidonda, magonjwa ya figo, vidonda vyenye maumivu makali, ugumba na kifo.  

Harufu mbaya itokanayo na uvujaji wa mara kwa mara wa mkojo au kinyesi huwatenga wanawake ambao mara nyingi huaibishwa na kunyanyapaliwa, kutelekezwa na marafiki na familia zao na kutengwa na jamii zao.

Wanakabiliwa na msongo wa mawazo na hisia za kutaka kujiua na masuala mengine ya afya ya akili.  

Wakinyimwa fursa za kujikimu, wanaingizwa zaidi katika umaskini na mazingira magumu ya hatari. 

3. Wasichana wadogo ndio hasa walio katika mazingira magumu. 

Razia Shamshad aliozwa akiwa na umri wa miaka 13 na wakati wa kujifungua alipata fistula na baada ya miaka mingi alipata matibabu.
© UNFPA Pakistan
Razia Shamshad aliozwa akiwa na umri wa miaka 13 na wakati wa kujifungua alipata fistula na baada ya miaka mingi alipata matibabu.

 

Akiwa na umri miaka 13, Razia Shamshad aliolewa na kupata mimba. Baada ya kuvumilia uchungu wa uzazi kwa siku nne huku mkunga asiye na ujuzi akimsaidia, alipata fistula ya uzazi na binti yake alizaliwa mfu.  

Ilimchukua miaka, lakini Bi. Shamshad hatimaye alirudisha maisha yake ya awali baada ya kufanyiwa upasuaji mara kadhaa. "Hakuna mwanamke anayestahili kuishi kwa mateso," amesema. "Hasa wakati Fistula inatibika."  

Ingawa Fistula haibagui kwa umri, wasichana wadogo wako katika hatari zaidi kwa sababu miili yao inaweza kuwa haiko tayari kwa kujifungua.  

Watoto tisa kati ya kumi wanaozaliwa na wasichana wa kati ya umri wa miaka 15 na 19 hutokea katika ndoa au muungano wa aina fulani.  

Ulimwenguni kote, matatizo ya ujauzito na uzazi ndiyo chanzo kikuu cha vifo miongoni mwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 19.  

Na hii ni moja ya  sababu kubwa kwa UNFPA kufanya kazi kutokomeza mila mbaya ya ndoa za utotoni. 

4. Chanzo chake ni umaskini na ukosefu wa usawa wa kijinsia. 

Fistula ya uzazi imetoweka katika nchi tajiri zenye mifumo bora ya huduma za afya na wataalamu wenye ujuzi ambao wanaweza kufanya upasuaji vyema.  

Wakunga ni sehemu muhimu ya suluhisho. Shirikisho la kimataifa la wakunga linasema "kukomesha fistula ya uzazi kunahitaji ushirikishwaji kamili wa wakunga katika ngazi ya jamii, kitaifa, kikanda na kimataifa." 

Mbali ya ukosefu wa huduma bora za afya, umaskini ni hatari kubwa ya kijamii kwa sababu unahusishwa na ndoa za mapema na utapiamlo.  

Kujifungua mtoto kabla ya viungo vya uzakzi kukomaa kikamilifu pamoja na utapiamlo, kimo kidogo na hali duni za afya kwa ujumla huchangia sababu za kisaikolojia katika wakati wa uchungu wa kujifungua unaopelekea kupata Fistula . Hata hivyo, wanawake wenye umri mkubwa ambao tayari wameshapata watoto wako katika hatari pia. 

Kwa kuongezea, kwa sababu ya ukosefu wa usawa wa kijinsia katika jamii nyingi, wanawake hawana uhuru au uharaka wa kuamua ni lini waanze kupata watoto au wapi pa kujifungulia. 

Maseray Bangura anasema hadhi yake imerejeshwa baada ya kutibiwa fistula.
© UNFPA Sierra Leone
Maseray Bangura anasema hadhi yake imerejeshwa baada ya kutibiwa fistula.

 

"Heshima yangu na utu wangu vimerejeshwa," anasema Maseray Bangura, ambaye alifanyiwa upasuaji wa kurekebisha kutibu fistula katika Kituo cha wanawake cha Aberdeen huko mjini Freetown, Sierra Leone.  

Kujenga uwezo wa hospitali ili kutokomeza ugonjwa wa fistula kunaungwa mkono na serikali ya Iceland na UNFPA kama sehemu ya kampeni ya Kukomesha Fistula. 

5. Inatibika, lakini la muhimu zaidi, inaweza kuzuilika. 

Hadi asilimia 95% ya fistula inaweza kufungwa kwa upasuaji. Ukarabati kwa njia ya  ya upasuaji unagharimu dola 600, gharama ambayo wanawake wengi walio na Fistula hawawezi kuimudu endapo wanafahamu hata hali halisi ya kiafya waliyo nayo na kwamba matibabu yapo.  

Kupitia usaidizi wake kwa nchi na kampeni ya kukomesha Fistula shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani na masuala ya afya ya uzazi UNFPA, limesaidia zaidi ya upasuaji 121,000 iliyobadili maisha na maelfu ya watu tangu mwaka 2003 na kutoa mafunzo kwa maelfu ya wafanyakazi wa afya ya kuzuia na kutibu Fistula. 

Lakini kabla ya kufikia hatua ya matibabu, mkazo unapaswa kuwa juu ya kuzuia. Hatua hizo ni pamoja na “upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, wakunga wenye ujuzi na huduma ya dharura ya uzazi. Kushughulikia mambo ya kijamii yanayochangia fistula  kama ndoa za utotoni na mimba, elimu ya wasichana, umaskini na ukosefu wa uwezeshaji wa wanawake,” ambavyo pia ni sehemu ya Kampeni ya mkakati wa kukomesha Fistula. 

Kuhatarisha maisha ya mtu kwa ajili ya kuleta maisha mapya na uhai mpya duniani ni hatima mbaya sana.  

Lakini kwa ufahamu na utashi, lengo la kutokomeza hali hiyo ifikapo 2030 linaweza kufikiwa.