Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliopoteza maisha kwenye tetemeko Morocco wafika 2500, UN iko tayari kusaidia

Tetemeko la ardhi lililokuwa na kitovu katika milima limesababisha uharibifu katika jiji la kihistoria la Marrakech, Morocco.
UNESCO/Eric Falt
Tetemeko la ardhi lililokuwa na kitovu katika milima limesababisha uharibifu katika jiji la kihistoria la Marrakech, Morocco.

Waliopoteza maisha kwenye tetemeko Morocco wafika 2500, UN iko tayari kusaidia

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea mshikamano wake kwa serikali na watu wa Morocco katika kipindi hiki kigumu baada ya tetemeko la ardhi ambako kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA takwimu zilizotolewa n amalaka ya Morocco zinasema idadi ya waliopoteza maisha kufikia leo ni 2500 na waliojeruhiwa ni 2500.

 

Antonio Guterres katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake kwa waandishi wa habari mjini New York Marekani ametoa rambirambi kwa familia za wote waliopoteza maisha na kuwatakia ahuweni ya haraka majeruhi, ambapo asilimia kuwa ya walioathirika ni kutoka katika majimbo majimbo ya Al-Haouz na Taroudant.

Taarifa ya msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa imeendelea kusema kuwa "Tunasisitiza utayari wetu wa kusaidia serikali ya Morocco katika juhudi zake za kusaidia idadi kubwa ya watu walioathirika."

Pia msemaji huyo amebainisha kuwa "vizuizi vya barabarani na mazingira magumu ya kijiografia yamefanya iwe changamoto katika shughuli za utafutaji na uokoaji huku watu wengi wakihofia matetemeko mengine wamesaka hifadhi nje.”

Ameongeza kuwa "Mamlaka nchini Morocco zinaongoza juhudi za kukabiliana changamoto za baada ya tetemeko hilo na zimeanzisha mifumo ya kitaifa ya uokoaji na mikakati ya kuchukua hatua."

Vitengo vya ulinzi wa raia vimepelekwa

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu imeendelea kusema kwamba “Vitengo vya ulinzi wa raia vimetumwa ili kuongeza akiba katika hifadhi za damu na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali muhimu, ikiwa ni pamoja na maji, chakula, mahema na mablanketi kwenye maeneo yaliyoathirika. Timu za Hilali nyekundu za Morocco zinaendeleakuchukua hatua za msaada mashinani, kutoa huduma ya kwanza, msaada wa kisaikolojia na kusaidia kuwasafirisha majeruhi hadi hospitali.”

Msemaji huyo amehitimisha tarifa ya Katibu Mkuu kwa kusema kwamba, "Tunaendelea kuwa katika mawasiliano ya karibu na mamlaka ya Morocco ili kutoa msaada wetu katika tathmini, uratibu, na kukabiliana na hali hiyo."