Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

AU kukubaliwa katika G20 ni taswira ya kuongezeka kwa umuhimu wa Afrika kimataifa - Guterres

Makao Makuu ya Muungano wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia
UNECA/Daniel Getachew
Makao Makuu ya Muungano wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia

AU kukubaliwa katika G20 ni taswira ya kuongezeka kwa umuhimu wa Afrika kimataifa - Guterres

Masuala ya UM

Mkutano wa kila mwaka wa Kundi la Nchi 20 zenye Maendeleo Makubwa ya Kiuchumi Duniani (G20) umehitimishwa jana katika mji mkuu wa India New Delhi huku Umoja wa Mataifa ukiwa umekaribisha kupitishwa kwa Azimio la Viongozi wa Kundi hilo kukubali kujumuisha Muungano  wa Afrika (AU) kama mwanachama wake mpya wa kudumu.

Baadhi ya viongozi wa Afrika haraka baada ya uamuzi huo walijitokeza kuonesha furaha yao ambapo kwa upande wake Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye pia alihuduria mkutano huo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X akisema, "Tuna furaha kwamba G20 imekubali AU kama mwanachama wa G20. Mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira, matumizi yasiyo endelevu na uzalishaji na uhaba wa rasilimali ni changamoto zinazoweza kutatuliwa kwa pamoja na kwa mshikamano mkubwa."

Naye Rais wa Kenya William Ruto akitumia pia ukurasa wake wa X aliandika, "Kenya inakaribisha kuongezwa katika G20 Muungano wa Afrika - bara linalokua kwa kasi zaidi duniani. Hii itaongeza sauti ya Afrika, kuonekana, na ushawishi katika jukwaa la kimataifa na kutoa jukwaa la kuendeleza maslahi ya pamoja ya watu wetu. Hii inaendana kikamilifu na maazimio ya Mkutano wa Afrika kuhusu Tabianchi uliokamilika hivi karibuni.” 

Katika Mkutano wa G20, chini ya Kauli Mbiu “Dunia Moja, Familia Moja, Mstakabali Mmoja,” masuala muhimu kama vile uhakika wa chakula, tabianchi na nishati, maendeleo, afya na digitali yalijadiliwa.