Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ingawa dunia inategemea Afrika, cha ajabu Afrika haiwezi kuweka mategemeo yake kwa dunia- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki wakihutubia na waandishi wa habari mjini Addis Ababa, Ethiopia
UN News
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki wakihutubia na waandishi wa habari mjini Addis Ababa, Ethiopia

Ingawa dunia inategemea Afrika, cha ajabu Afrika haiwezi kuweka mategemeo yake kwa dunia- Guterres

Masuala ya UM

Akiwa nchini Ethiopia, hususan jijini Addis Ababa anakoshiriki mkutano wa viongozi wa nchi za Muungano wa Afrika, AU, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema suala la kusikitisha ni kwamba licha ya kwamba dunia inategemea Afrika kutatua shida zake, bado bara la Afrika halijaweza kuweka tegemeo lake kwa dunia katika kukabili changamoto inazozikabili. 

Guterres amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari, mkutano ambao umehudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika, Moussa Faki Mahamat. 

Mzozo na ukame vimesababisha ukosefu wa chakula katika maeneo mengi ya Somalia
© WFP/Kevin Ouma
Mzozo na ukame vimesababisha ukosefu wa chakula katika maeneo mengi ya Somalia

Afrika yategemewa kufyonza hewa ya  ukaa lakini haipati fedha za kukabili tabianchi 

Katibu Mkuu ametolea mfano madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayokumba Afrika, kuanzia ukame hadi mafuriko, vichocheo vikiwa ni shughuli za uchafuzi zinazosababishwa na mataifa makubwa. 

“Afrika inapokea matone tu ya usaidizi kukabili na kuhimili uharibifu huu,” amesema Katibu Mkuu akisema mamia ya watu wamepoteza maisha, mamilioni wamepoteza makazi yao kutokana na mafuriko ya hivi karibuni Nigeria, Chad na Sudan Kusini “na hili ni kumbusho juu ya kushindwa kwetu kushughulikia janga la tabianchi.” 

 Ametaja changamoto nyingine zinazokumba Afrika kama vile kukwama kwa harakati za Afrika kujikwamua kutokana na janga la COVD-19 kwa sababu ya mfumo wa kifedha wa kimataifa uliomomonyoka. 

Mizigo ya madeni yakwamisha Afrika kusonga  mbele 

Nchi nyingi za Afrika zimezidiwa na mzigo wa madeni unaozikwamisha kuwekeza katika mifumo na huduma za msingi kama vile elimu, afya, hifadhi ya jamii na fursa za ajira bila kusahau  ubunifu. 

Chakula nacho kinasalia ndoto kwa mamilioni ya wakazi wa bara la Afrika wakiwemo watu milioni 36 wanaokabiliwa na njaa kwenye Pembe ya Afrika kutokana na ukame mbaya kuwahi kukumba eneo hilo katika miongo minne. 

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu Guterres amependekeza mambo makuu matatu ya kurejesha imani ya Afrika kwa dunia na wakati huo kusongesha maendeleo na kukabili tabianchi. 

Mosi: Afrika inahitaji ubia mpya kwa ajili ya ustawi na maendeleo 

 Guterres anasema nchi zinazoendelea ikiwemo za Afrika zinahitaji msaada wa dharura kuimarisha huduma na miradi inayohitaji. 

“Mwezi uliopita nilisihi nchi za G20 zipitishe mpango wa kuchochea malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ili kuwezesha nchi zinazoendelea kuwekeza Pamoja na kuwa na fedha sambamba na kupata msamaha wa madeni.” 

Amesema mipango ipo lakini kinachohitajika ni kasi na iendane na hali halisi ya wakati husika. Mathalani vigezo mahsusi na vya kipekee kwa nchi kuweza kukopa, au Special Drawing Rights zielekezwe kwa nchi zinazohitaji badala ya kuelekezwa kwa nchi Tajiri pekee. 

Mito Chari na Logone imefurik huko N'Djamena Chad baada ya mvua kubwa iliyosababisha mafuriko
© UNICEF/Aldjim Banyo
Mito Chari na Logone imefurik huko N'Djamena Chad baada ya mvua kubwa iliyosababisha mafuriko

Pili: Afrika inahitaji na ina haki ya usaidizi kwenye tabianchi 

Katibu Mkuu amekumbusha hatua ya COP27 kuanzisha Mfuko Maalum wa kufidia hasara na Uharibifu  ni hatua muhimu katika kufikia haki kwenye tabianchi hasa kwa wale ambao wanaathirika bila kusababisha, Afrika ikiwa mojawapo. 

“Tumezindua pia mpango wa utekelezaji kuanzisha mifumo ya utoaji maonyo ili kulinda kila mkazi wa dunia, mpango unaotakuwa kuanzishwa ndani ya miaka mitano ikihusisha nchi 6 katika nchi 10 za Afrika zisizo na mifumo hiyo,” amesema Guterres. 

Hata hivyo amesema ahadi ya kuongeza maradufu ufadhili wa kukabili tabianchi hadi dola bilioni 40 kwa mwaka haijafikiwa. 

“Gharama ya kukabili madhara ya tabianchi kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahari ni dola bilioni 50 kwa mwaka kwa kipindi cha muongo mmoja ujao. Afrika haiewzi kugharimia fedha hii yote, na haipaswi,” amesema Katibu Mkuu. 

Hivyo ametaka mshikamano kuwezesha Afrika kufanikisha mipango yake. 

Tatu: Afrika ina haki ya amani na inahitaji amani  

Katibu Mkuu amesema kuanzia Sahel hadi Maziwa Makuu na hadi Ethiopia, mizozo bado ni changamoto. Na kwamba wamezungumza kwenye mkutano Addis Ababa ni kwa vipi Umoja wa Mataifa na AU wanaweza kushirikiana kuimarisha amani Afrika sambamba na haki za binadamu. 

Hata hivyo amesema “tunahitaji kuhakikisha operesheni za kulinda amani na kukabili ugaidi Afrika kwa mujibu wa Baraza la Usalama na Chata ya  Umoja wa Mataifa Ibara ya VII zinafanyika na zinakuwa tulivu huku zikipatiwa fedha zinazohitajika.” 

Guterres amesema amani si jambo rahisi lakini ni jambo muhimu hivyo Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na AU kusongesha amani, ustawi na haki ya tabianchi kwa watu wote wa Afrika kwa kuwa ni haki yao.