Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wafungwa mitego ya mikanda ya mabomu DRC

Mama na watoto wawili wakitembea katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Goma, mashariki mwa DR Congo
© UNICEF/Jospin Benekire
Mama na watoto wawili wakitembea katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Goma, mashariki mwa DR Congo

Watoto wafungwa mitego ya mikanda ya mabomu DRC

Amani na Usalama

Ukatili dhidi ya watoto mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC umepindukia, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini humo likitolea mfano watoto mapacha ambao hivi karibuni walikutwa wamefungwa mkanda wenye mabomu kiunoni ili yeyote atakayejaribu kuufungua uwezo kulipuka na kusababisha maafa.

Ni Grant Leaity mwakilishi wa UNICEF nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC akieleza kuwa hivi karibuni alitembelea kituo kimoja jimboni Kivu Kaskazini kinachohifadhi watoto walioachiliwa huru na vikundi vilivyojihami na kukuta watoto wawili mapacha wenye umri wa mwaka mmoja waliokuwa wametelekezwa kwenye Kijiji wakiwa na mkanda kiunoni wenye mabomu. 

Amewaambia waandishi wa Habari mjini Geneva USwisi hii leo kuwa kitendo hicho ni miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto nchini DRC na kwamba ni taifa lenye matukio makubwa ya ukatili dhidi ya watoto yaliyothibitishwa na Umoja wa Mataifa. 

Katika kipindi cha mwaka mmoja, ongezeko la ghasia mashariki mwa DRC limesababisha ukimbizi mkubwa zaidi Afrika, watoto zaidi ya milioni 2.8 wakibeba mzigo wa janga hilo. 

Bwana Leity anasema niko hapa leo, natumai nitapaza sauti nisikike. Kila siku watoto wanabakwa, na wanauawa, wanatekwa, wanatumikishwa vitani na wanatumiwa na makundi yaliyojihami na tunajua ripoti tulizo nazo ni kidogo kulinganisha na matukio halisi.” 

Alipoulizwa nini kilitokea baada ya kubaini watoto hao, Mwakilishi huyo wa UNICEF DRC amesema “tuliwasiliana na wenzetu wataalamu wa kutegua mabomu ambao walikuja na kuweza kuondoa mtego huo wa mabomu kwa usalama.” 

Amesema matumizi ya vilipuzi vya kutengeneza yanazidi kuongezeka DRC. na hivyo UNICEF inatoa wito kwa hatua zichukuliwe ili kumaliza mzozo na familia zirejee nyumbani. 

Pamoja na ghasia ya kiwango cha juu dhidi ya watoto, Afisa huyo amesema maisha ya watoto mashariki mwa DRC yanatishiwa na milipuko ya magonjwa na utapiamlo. 

Takribani watoto milioni 1.2 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri kwenye eneo hilo. 

UNICEF inasema dunia inawaangusha watoto wa DRC kwani imewasahau, ikisema kuna matumaini lakini bado msaada unahitaji kwenye maeneo mawili. 

Mosi, rasilimali kuweza kukidhi mahitaji ya kibinadamu ya watoto inahitaji dola milioni 400. 

Pili ni utashi wa kisiasa kumaliza mzozo unaoendelea DRC na hivyo inatoa wito kwa serikali, mataifa ya Afrika na jamii ya kimataifa kushirikiana kusaka suluhisho la amani ya kudumu kwenye janga hilo ili familia zirejee nyumbani.