Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuchukue hatua ya pamoja kwa ajili ya hewa safi – Katibu Mkuu UN

Pichani ni eneo la Landmannalaugar, Iceland: Hewa safi ni muhimu kwa afya na maisha ya kila siku ya watu.
Unsplash/Luca Baggio
Pichani ni eneo la Landmannalaugar, Iceland: Hewa safi ni muhimu kwa afya na maisha ya kila siku ya watu.

Tuchukue hatua ya pamoja kwa ajili ya hewa safi – Katibu Mkuu UN

Tabianchi na mazingira

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi kwa ajili ya Anga la Bluu, leo siku Septemba 9, Katibu Mkuu wa Umoja wa António Guterres Guterres ametoa wito wenye nguvu wa kuongeza ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na "dharura ya kimataifa" ya hali mbaya ya uchafuzi wa hewa. 

Vichafuzi vinavyopeperuka hewani ni moja wapo ya hatari kubwa zaidi kwa afya ya mazingira. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO), asilimia 99 ya watu duniani wanavuta hewa iliyochafuliwa, huku hali hiyo ikizidi kuwa mbaya zaidi katika nchi za kipato cha chini na cha kati. 

Hali ya kuenea ya uchafuzi wa hewa inahitaji ushirikiano wa kimataifa. Kaulimbiu ya mwaka huu, Pamoja kwa ajili ya Hewa Safi, inaangazia hitaji la dharura la ushirikiano wa kimataifa wenye nguvu, kuongezeka kwa uwekezaji, na uwajibikaji wa pamoja wa kupunguza uchafuzi wa hewa. 

"Matatizo ya kimataifa yanahitaji ufumbuzi wa kimataifa. Ni lazima tuchukue hatua pamoja ili kupata hewa safi,” aanasema Bwana Guterres. 

Bwana Guterres ameongeza kusema, "Kwa pamoja, lazima tuharakishe mabadiliko ya haki na usawa kutoka kwa nishati ya mafuta ya kisukuku, hasa makaa ya mawe, kuelekea nishati safi inayoweza kurejeshwa, huku tukihakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma." 

Uchafuzi wa hewa 

Uchafuzi wa hewa unafafanuliwa kama uchafu wowote wa kemikali, kimwili au kibayolojia ambao hurekebisha sifa asili za angahewa. 

Majiko ya majumbani na vifaa vingine vya kutoa moto, magari, vifaa vya viwandani, na moto wa misitu ndio vyanzo vya kawaida vya uchafuzi wa hewa. Uchafuzi wa hewa upo nje na ndani, na huathiri vibaya afya ya binadamu. 

Vichafuzi ambavyo ni hatari zaidi ni pamoja na monoksidi ‘carbon monoxide’, ozoni, nitrogen dioxide, na sulphur dioxide. 

Uchafuzi wa hewa pia unajumuisha PM2.5, chembe chembe zinazoweza kuvutwa chini ya kipenyo cha mikromita 2.5 - chini ya ukubwa wa nywele za binadamu. 

Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi kwa ajili ya anga la buluu, ambayo inaadhimishwa tarehe 7 Septemba kila mwaka, ilianzishwa mwaka 2019 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo lilitambua umuhimu wa hewa safi na athari za uchafuzi wa hewa kwa afya ya binadamu na mifumo ikolojia, hususan athari zisizo sawa kwa wanawake, watoto na wazee.