Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukomeshe ukatili dhidi ya asili: Katibu Mkuu wa UN

Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.
NASA
Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.

Tukomeshe ukatili dhidi ya asili: Katibu Mkuu wa UN

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa kukomeshwa kwa vita vya kikatili na visivyo na maana dhidi ya asili, akisisitiza kwamba afya ya mwanadamu inategemea afya ya dunia, hewa tunayovuta, maji tunayokunywa na udongo ambao chakula chetu kinakua.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyasema hayo katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia inayodhimishwa kila tarehe 22 Aprili. Aidha amehimiza kufikiria kuhusu uhusiano wa mwanadamu na ulimwengu wa asili. 

Leo, shughuli za binadamu zinaharibu misitu, ardhi ya kilimo, ardhi oevu, bahari, miamba ya matumbawe, mito, bahari na maziwa. Baionuai inapungua kwa kasi – aina za viumbe milioni moja ziko kwenye hatihati ya kutoweka. 

"Lazima tukomeshe vita hivi vya kikatili na visivyo na maana na asili. Tuna zana, maarifa na suluhu kwa hili, lakini kasi inahitaji kuharakishwa,” Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza. 

Ametoa wito wa kuimarishwa kwa hatua za kuzuia ongezeko la kasi la joto duniani na, katika suala hili, akahimiza ongezeko la uwekezaji katika miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ustahimilivu, hasa kwa nchi zilizo hatarini zaidi na jamii ambazo zimechangia kidogo katika kusababisha janga la tabianchi. 

"Mifumo ya ikolojia yenye afya, kuanzia bahari na mito hadi misitu na nyanda, pia ni muhimu kwa mapambano yetu dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa. Hebu turudi kwenye mstari na makubaliano ya kihistoria ya Umoja wa Mataifa kuhusu viumbe hai kulinda asilimia 30 ya ardhi na maji ya Dunia ifikapo mwaka 2030,” António Guterres amehimiza. 

Zaidi Guterres Aamesisitiza kwamba serikali lazima ziwe na jukumu kubwa katika kulinda maumbile, lakini muhimu vile vile ni jukumu la mashirika, taasisi na asasi za kiraia, pamoja na sifa za uongozi za watu wa asili ambao wametunza mazingira kwa maelfu ya miaka na wanaweza kutoa misaada mbalimbali ya suluhisho za majanga ya dunia, yanayohusiana na hali ya hewa na upotevu wa viumbe hai. 

"Hebu sote tuchangie pamoja kulinda nyumba yetu ya pamoja kwa ajili ya watu na sayari ya leo na kwa ajili ya vizazi vijavyo," Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amehimiza. 

Siku ya Kimataifa ya Mama Duniani iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1970. Takriban watu milioni 20, waliokasirishwa na umwagikaji wa mafuta, uchafuzi wa hewa na mito, kisha waliingia mitaani kupinga janga la mazingira. Ilikuwa ni hatua kubwa zaidi ya uanaharakati wa kiraia, na serikali zilipaswa kusikiliza: sheria zilipitishwa kulinda mazingira na mashirika husika yaliundwa. Ulikuwa ushindi uliodhihirisha nguvu ya umoja wa kijamii. 

Mnamo mwaka wa 2009, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha azimio la kutangaza Aprili 22 kuwa Siku ya Dunia.