Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mng’aro Mtaani Kenya: Ukimtendea mtu wema, naye atamtendea mwingine - Torrez Omoll

Torrez Omoll, muasisi wa Mngaro Mtaani, shirika la kujitolea kusaidia watu maskini na wagonjwa nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Torrez Omoll, muasisi wa Mngaro Mtaani, shirika la kujitolea kusaidia watu maskini na wagonjwa nchini Kenya.

Mng’aro Mtaani Kenya: Ukimtendea mtu wema, naye atamtendea mwingine - Torrez Omoll

Msaada wa Kibinadamu

Leo ni siku ya kimataifa ya hisani au kuwaonea huruma wagonjwa na maskini, siku iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutambua mchango wa Hayati Mama Teresa wa Calcuta nchini India ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya amani ya Nobel. Hayati Mama Teresa alianzisha shirika la watawa wa huruma likiendesha makazi ya kuhudumia maskini na wagonjwa.  

Katika jamii wapo watu wanaoyaishi maisha ya kusaidia wengine kwa vitendo. Wanatoa usaidizi, au hisani na fadhila na furaha yao ni kuona wengine wakipata mahitaji yale ambayo bila kusaidiwa hawatayapata japokuwa ni mhumu sana katika maisha yao.  

Hisani kama ulivyo ufadhili na kujitolea ni mambo ya msingi katika vita dhidi ya umaskini katika jamii. Lengo la kwanza la maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ni kutokomeza umaskini.  

Ofisi ya Mng'aro Mtaani katika mtaa wa Lucky Summer jijini Nairobi Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Ofisi ya Mng'aro Mtaani katika mtaa wa Lucky Summer jijini Nairobi Kenya.

Torrez Omoll na mradi wa Mng’aro Mtaani 

Katika mtaa wa Lucky Summer jijini Nairobi, Torrez Omoll aliamua kuchukua hatua mikononi mwake kwa kukusanya nguo kuukuu za mitumba na kuzigawa kwa wanaozihitaji katika jamii. Huduma hiyo sasa imebadili umbo na sasa wamezindua mradi wa kuwashonea watoto wa shule ya msingi sare za michezo pasina malipo. 

Torrez Omoll ni mkazi wa mtaa wa Lucky Summer jijini Nairobi anakoishi na familia yake. Nguo anazozitoa ni msaada unaowalenga watu wenye kipato cha chini katika jamii. Torrez huzikusanya kutoka kwa wasamaria wema na kisha kuzisafisha kabla ya kuzigawa kwa wanaizihitaji.  

Kupitia mitandao ya kijamii, Torrez huomba nguo hizo kuukuu kutoka kwa wasamaria wema. Shirika lake la kujitegemea la Mng’aro Mtaani huratibu misaada wanayopokea.  

Kipi kilimsukuma Torrez kuanza mradi huu wa kugawa nguo kuukuu? 

 “Napenda kutenda mema katika jamii. Nilifanyiwa hisani kupitia kanisa. Kila ninapoona mtu anatenda mema nami nafarijika kwani anayeupokea wema pia naye atamtendea mwingine wema. Hiyo ina maana kuwa tunakuwa na uvumilivu katika jamii na maendeleo yatapatikana,” anafafanua. 

Sare za shule wanazopewa wanafunzi kutoka kwa kaya maskini nchini Kenya bila.
UN News/Thelma Mwadzaya
Sare za shule wanazopewa wanafunzi kutoka kwa kaya maskini nchini Kenya bila.

Umaskini ni adui wa maendeleo 

Wakazi wa Luckysummer wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kwa sababu ya uchochole. Hisani ni njia moja ya kupambana na umaskini na kuwainua wasiojiweza katika jamii.  

Ajenda ya 2030 Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa mataifa (SDGs) inaafiki kuwa kutokomeza umaskini ndio changamoto kubwa zaidi na kigezo muhimu katika kuleta maendeleo endelevu. Hapo ndipo hisani inapopata nafasi kujaza mapengo ili kutimiza malengo. Evans Sandagi ni mmoja ya walionufaika na hisani ya shirika la Mng’aro Mtaani na anashukuru kwani harakati zimeleta tija kwani, “Kila ninapopokea hizo nguo nazikagua na ananieleza kuwa iwapo umeona chochote kinachokufaa nawe chukua.Nafurahi kwani familia yangu imefaidika kwa kiasi kikubwa.Sio rahisi kupata mtu wa kukusaidia.Ukipata wahisani nawe pia unashkuru kwani maisha yanarahisishwa.” 

Mradi wa kushona sare za michezo 

Shirika la kijamii Mng’aro Mtaani lilizindua mradi wa kushona sare za michezo mahsusi kwa wanafunzi wasiojiweza na kuwapa bure bila malipo. Kila walipotembelea shule waliwapata wanafunzi wakiwa na uhaba mkubwa wa sare za michezo kwani zilikuwa zimepasuka mno. Sasa, wanafunzi hao walioko shule karibu ya msingi ya Babadogo ni wengi wa bashasha kwani wamepokea sare mpya za michezo. 

Mary Wambui, Fundi na mwalimu wa kushona katika kituo cha Mg'aro Mtaani nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Mary Wambui, Fundi na mwalimu wa kushona katika kituo cha Mg'aro Mtaani nchini Kenya.

Mary Wambui ni fundi na mwalimu wa kushona katika kituo cha Mng’aro Mtaani na kulingana na yeye, “Kinachotupa faraja ni kuwa kila tunapowapa wanafunzi sare hizo, nyuso zao huwa zimejaa furaha hata wanashindwa kusema asante.Baadhi husema , kwa mara ya kwanza maishani mwangu nimepata sare mpya ambazo hazijawahi kuvaliwa na mtu, hilo linanifurahisha sana.Kauli kama hizo ndizo zinazotusukuma kuja kushona kila siku,” anamalizia. 

Sharon Anyango naye ni mwalimu na mtaalam wa masomo ya urembo katika kituo cha Mng’aro Mtaani. Sharon alisomea masuala ya maendeleo ya jamii kwa ufadhili.Kwasababu ya hilo aliamua naye kusaidia katika jamii ili kurejesha mkono kwani, "Nilisaidiwa kupata masomo kwani mhisani aliona haja ya kunipa nafasi. Sina budi nami kurejesha mkono kupitia shirika hili la kijamii ili mwengine naye apate nuru maishani.” anasisitiza. 

Maendeleo katika jamii 

Kila anapopata nafasi ya kuwasaidia wasiojiweza , Torrez anafarijika kwani azma yake imetimia. Mng’aro Mtaani ilianza kwa nadharia ya kuwasaidia wasiojiweza katika jamii kupata mavazi ambayo ni mchango wa wahisani.Malengo yao ni kupambana na umasikini kadhalika kuhifadhi mazingira kwa kugawa nguo kuukuu ambazo zingetupwa majaani.