Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Moyo wa fadhila wa Mama Teresa bado unazingatiwa huko Beni, DRC

Benge Mukengere, Kiongozi wa shirika la AFNAC linalohudumia watoto na wanawake wazee katika mji wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC.
UN News/George Musubao
Benge Mukengere, Kiongozi wa shirika la AFNAC linalohudumia watoto na wanawake wazee katika mji wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC.

Moyo wa fadhila wa Mama Teresa bado unazingatiwa huko Beni, DRC

Msaada wa Kibinadamu

Katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya hisani au fadhila tunamulika vituo au watu wanaojitolea kusaidia maskini na wagonjwa ikiwa ni katika kutambua siku hii iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutambua mchango wa Hayati Mama Teresa wa Calcuta nchini India ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya amani ya Nobel. Hayati Mama Teresa alianzisha shirika la watawa wa huruma likiendesha makazi ya kuhudumia maskini na wagonjwa. 

Huko Maziwa Makuu ya Afrika, mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa George Musubao ametembelea kituo cha shirika lisilo la kiserikali au la AFNAC linalohudumia watoto na wanawake wazee katika mji wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC.    

Wazee wanaongea peke yao barabarani  

Amezungumza na Benge Mukengere mwenye umri wa miaka 62 pia kiongozi wa shirika hili ili kutaka kujua ni kwa nini walichagua kuhudumia wanawake wazee ambaye amesema "wakati tulipokuwa tukitembea tunamkuta mtu mwenye umri tangu miaka 55 na zaidi anaongea peke yake barabarani unamuuliza kwa nini? anasema anaumwa ila hapati matibabu.”  

Amesema wazee wengine wanapitapita kwenye maduka wakiomba usaidizi mara mbili kwa wiki ijapo wengine wana nguvu ilhali wengine pia wanalia kuwa watu wameuza mashamba yao n ahata wakati mwingine watoto wao wameuza nyumba sasa hawana pa kuishi.  

Bi. Mukengere amesema ndio maana waliona ni haki kuwasaidia kwani wazee wana haki ya kula vizuri, kuishi vizuri kupata matibabu na misaada mingine.  

Tawinika Chebea, Mama mwenye umri ya miaka 68 pia mmoja ya wazee wanaopokea msaadaa toka kwa AFNAC, Kivu DRC.
UN News/George Musubao
Tawinika Chebea, Mama mwenye umri ya miaka 68 pia mmoja ya wazee wanaopokea msaadaa toka kwa AFNAC, Kivu DRC.

AFNAC imetuondolea utegemezi  

Mmoja wa wanufaika wa AFNAC ni Tawinika Chebea mama mwenye umri ya miaka 68 yeye anasema, "sisi ambao bado tuna nguvu tunatengeneza bustani ya pamoja baada AFNAC kutupatia mbegu ambazo tunapanda. Wengine wazee wanafundishwa namba ya kutengeneza sabuni, tunauza na kupata pesa kidogo na wengine wanafunzwa kusuka vikapu, wanapomaliza wanauza na kupata pesa kidogo inayosaidia jamaa.”  

Mnufaika huyu anasema “tunapofanya hivi tunahisi kwamba tunatulizwa kifikra na mara wanatufunza kujitegemea katika uzee wetu ili tusiwe wa kuombaomba tunafanya kazi ili tusiwe mzigo kwenye familia".  

UN na serikali DRC wasisahau msaada kwa wazee  

Na ndipo Kiongozi wa AFNAC, Bi. Mukengere anatoa wito kwa viongozi akisema,  

"Umoja Wa Mataifa uwakumbuke pia akinamama wazee wenye  umri tangu miaka 55 na zaidi kwani wanasumbuka sana katika mji wa Beni, Kivu kaskazini nzima. Akina mama hao wanateseka wakati wanakimbia vita na mapigano kwa kuwa hawawezi kukimbia na hawawezi kubeba chochote.”  

Amesema Umoja wa Mataifa unaweza kupatia wazee hao misaada kwa sababu wana haki ya kuishi kama watu wengine, halikadhalika serikali ya DRC nayo isiwasahau.  

AFNAC ilikuwa ikihudumia zaidi ya wazee 1 200 ila sasa kutokana na ukosefu wa msaada wanasaidia wanawake  wazee 112 mjini Beni.  

 

Kutoka BENI, jimboni Kivu Kaskazini, mimi ni GEORGE MUSUBAO, UN NEWS.