Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Libya wawasili Rwanda; mmoja hajawahi toka kambini kwa zaidi ya miaka 4-UNHCR

Wakimbizi kutoka Libya wakiwasili nchini Rwanda tarehe 26 Septemba 2019
UNHCR/Tobin Jones
Wakimbizi kutoka Libya wakiwasili nchini Rwanda tarehe 26 Septemba 2019

Wakimbizi wa Libya wawasili Rwanda; mmoja hajawahi toka kambini kwa zaidi ya miaka 4-UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Kundi la kwanza lenye wakimbizi 66 waliohamishwa kutoka Libya na limewasili nchini Rwanda usiku wa Alhamis ya Septemba 26, kwa ndege ya kukodi ya shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR, ameeleza hii leo mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNHCR, Babar Baloch

Kundi hilo la wakimbizi wa kwanza linafaidika na mpango wa dharura wa kuwahamisha wakimbizi, maamuzi yaliyofikiwa hivi karibuni na serikali ya Rwanda, UNHCR na Muungano wa Afrika, AU.

Kati ya wakimbizi waliohamishwa, 26 ni watoto, karibia wote wakiwa hawana uangalizi wowote yaani bila wazazi au walezi kutoka kwenye  familia zao.

“Mmoja wa waliookolewa kutoka Libya hajawahi kutoka nje ya kambi alimokuwa anashikiliwa kwa zaidi ya miaka minne. Wakimbizi wote waliookolewa na kuhamishwa wanatoka Sudan, Somalia au Eritrea.” amesema Baloch.

Kundi hili liliwasili katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali majira ya saa tatu unusu saa za Rwanda, linajumuisha mtoto mchanga aliyezaliwa katika kambi nchini Libya miezi miwili iyopita.

Zainab Yousef kutoka Somalia mama wa mtoto huyo mchanga wa umri wa miezi miwili anasema, “tunamshukuru Mungu. Hatuwezi kuelezea maisha yalivyo kule Libya. Kuna mapigano hatukuweza hata kulala kwa amani wakati wa usiku. Sasa tunajihisi salama.”

Baada kuwasili, wakimbizi wamesajiliwa na kupewa nyaraka kabla ya kupelekwa katika kituo cha muda cha Gashora kilichoko takribani kilomita 60 kusini mwa mji mkuu wa Rwanda, Kigali, ambako UNHCR imewapatia nyaraka, chakula, maji, vifaa vya jikoni, vyandarua vya kuzuia mbu  na vitu vingine vya kuwasaidia kuanzia maisha.

Tumefurahi kuokolewa dhidi ya kifo

Abdelbaset Mohamed mwenye asili ya Somalia ni miongoni mwa waliowasili nchini Rwanda anasema kwa furaha, “ninajisikia mwenye furaha hapa Rwanda na nina mke na mtoto, huko Libya sikondoka na chochote lakini niña furaha hapa Rwanda.”

Mwakilishi wa UNHCR nchini Rwanda Ahmed Baba Fall anasema, “hii ni ishara nzuri sana ya mshikamano na wakimbizi kutoka kwa watu na serikali ya Rwanda. Ni mfano pia wa uongozi wa kiafrika ambao ninatumai nchi nyingine zitafuata. Kielelezo hiki cha mshikamano na uwajibikaji wa pamoja utaokoa maisha ya wengi na kuwapa matumaini wakimbizi wengi ambao bado wameparaganyika nchini Libya.”

Wakimbizi kutoka Libya wakiwasili nchini Rwanda tarehe 26 Septemba 2019
UNHCR/Tobin Jones
Wakimbizi kutoka Libya wakiwasili nchini Rwanda tarehe 26 Septemba 2019

 

Rwanda tuko tayari kuendelea kusaidia

Kwa upande wa serikali ya Rwanda, Katibu Mkuu wa wizara ya kushughulikia masuala ya dharura, MINEMA, Bwana Olivier Kayumba amenukuliwa akisema, “hata kama sisi ni nchi ndogo lakini tunauwezo wa kutosha, hatuwezi kusema kwa kuwa nchi ni ndogo hatuwezi kupokea wakimbizi zaidi. Tuna wakimbizi 149,000, tunawapokea wengine zaidi na zaidi, hakuna shida.”

Timu ya wataalamu tisa wa afya wakiwemo wanasaikolojia watafanya kazi na wataalamu wa ushauri au nasaha katika kuwasaidia watoto na manusura wa unyanyasaji wa kingono kwa kuwapatia huduma za kiafya na vilevile kuwasaidia wakimbizi ambao wamenusurika na  mateso, unyanyasaji wa kingono na ukiukwaji wa haki za binadamu walipokuwa nchini Libya.

Babar Baloch amaeongeza kusema kuwa, “kundi lote hilo limepewa hadhi ya wasaka hifadhi wakati ambapo UNHCR inaendelea kutathimini ombi lao la ukimbizi na wana haki sawa na wakimbizi wengine nchini Rwanda ikiwemo elimu na huduma ya afya, uhuru wa kutembea na kufanya kazi. Wakimbizi wote waliookolewa watakaribishwa kupata mafunzo ya lugha na elimu ya ufundi ili kuwasaidia kujumuika na jamii za wenyeji kwa muda wao wote wakaokuwa nchini Rwanda.”

Aidha UNHCR imesema kwa yeyote kati yao atakayeonekana kuwa hayiuko kwenye uhitaji wa kulindwa kimataifa atasaidiwa kurejea nyumbani au atapewa uwezekano wa kuhalalishwa kusalia nchini Rwanda.

UNHCR/Tobin Jones
UNHCR/Tobin Jones
UNHCR/Tobin Jones

 

Wakimbizi wengine watatua hivi karibuni, ufadhili unahitaji

Ndege nyingine ya pili inategemewa kutua nchini Rwanda katika wiki za hivi karibuni wakati huu ambao UNHCR inaendelea kufanya jitihada za kuwaokoa wakimbizi waliko hatarini katika kambi nchini Libya.

UNHCR imeendelea kuisihi jumuiya ya kimataifa nia ya Rwanda ya kuungana mkono na wakimbizi kwa kusaidia kutoa msaada wa kifedha na maeneo ya makazi.

Kwa mujibu wa UNHCR inakadiriwa kuwa dola milioni 10 za kimarekani zitatumika katika uwekezaji wa awali na kuendesha mpango huo wa dharura katika ya Libya na Rwanda hadi kufikia mwishini mwa mwaka huu.

UNHCR imewahamisha wakimbizi na wasaka hifadhi 4,400 kutoka nchini Libya kuwapeleka katika nchi nyingine tangu mwaka 2017 wakiwemo 2,900 kuelekea Niger na 425 kuelekea katika nchi za Ulaya kupitia katika kambi ya muda nchini Romania.