Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi Afrika kuanza Septemba 4 nchini Kenya

Mtu akitembea katika maji ya mafuriko huko Gatumba, Burundi eneo ambalo linapokea mvua zisizotabirika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
© UNICEF/Karel Prinsloo
Mtu akitembea katika maji ya mafuriko huko Gatumba, Burundi eneo ambalo linapokea mvua zisizotabirika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi Afrika kuanza Septemba 4 nchini Kenya

Tabianchi na mazingira

Viongozi wa Afrika wanatarajiwa kukutana jijini Nairobi, Kenya wiki ijayo kwa ajili ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi ambako watajadili njia mbalimbali za kupunguza utoaji wa gesi chafuzi huku wakija na mbinu za kukabiliana na athari za hali ya hewa. 

Mkutano huo unaoanza tarehe 04 mpaka 06 Septemba mwaka huu unawaleta pamoja watunga sera, viongozi wafanyabiashara na wanaharakati wa mazingira kutoka kila pembe ya bara la Afrika. 

Kenya tayari imechukua hatua kwenye nishati jadidifu

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya Stephen Jackson akizungumzia mkutano huo ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Muungano wa Afrika (AU)  na serikali ya Kenya anaeleza sababu za mkutano huo kufanyikia kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.

Stephen Jackson, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya.
UN Kenya
Stephen Jackson, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya.

Anasema, Kenya ipo mstari wa mbele katika kuathirika na changamoto ya Mabadiliko ya Tabia Nchi, Kenya ipo hatua ya mbele katika kupendekeza suluhu. Hii ni sawa kwa bara la Afrika. Afrika ndilo bara litakalotupa suluhu kuhusiana na tatizo hili la Mabadiliko ya Tabia Nchi. Afrika ina pafu la pili la dunia katika msitu mkubwa nchini Congo wenye hulka ya kuwa na mvua za mara kwa mara."

Halikadhalika amesema  Afrika ina utajiri mkubwa wa dunia wa rasilimali za nishati jadidifu. Mathalani Kenya tayari ipo katika ngazi kubwa ya kutumia asilimia 93 ya nishati ya umeme unaozalishwa na nishati jadidifu. Afrika ina sehemu kubwa ya ardhi asilia yenye uwezo wa kuilisha dunia. Kwa sababu hizi zote, Afrika ndiyo mahala panapofaa kupatia suluhu kuhusiana na janga la Mabadiliko ya Tabia Nchi. Na Kenya ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kubadili mitizamo.

Kujaa maji katika ziwa Albert kumesababisha watu 100,000 wakimbie makwao na tayari UNHCR imewapatia msaada watu 14,000.
UN/ John Kibego
Kujaa maji katika ziwa Albert kumesababisha watu 100,000 wakimbie makwao na tayari UNHCR imewapatia msaada watu 14,000.

Afrika inahitaji ufadhili zaidi ili kutumia rasilimali za nishati endelevu

Mratibu Mkazi huyu anaeleza pamoja na kuwa na suluhu lakini Afrika inahitaji ufadhili wa kifedha akieleza kuwa inahitaji uwezeshwaji wa kifedha wenye masharti nafuu ili kuliwezesha bara la Afrika kutatua janga la mabadiliko ya tabianchi linalolikabili bara hilo ili pia "tutatue tatizo la dunia nzima. Hivi sasa hakuna fedha na ambapo fedha zikikosekana gharama zinakuwa ni za juu sana. Hivyo maono ya Rais William Ruto kuhusu mkutano huu na maono ya Muungano wa Afrika kuhusiana na bara hili  ni kwenda mbali zaidi ya kuangalia ajenda ya upotevu na uharibifu na agenda kuhusiana na uwezeshwaji ili kukabiliana na janga hili la mabadiliko ya `tabianchi."

Amesema ajenda bado zinabaki kuwa ni za umuhimu sana na na kuangalia ni jinsi gani watashirikiana kuchanga fedha nyingi kwa pamoja ili kuleta suluhu za kudumu za afrika katika soko la dunia.

Mkutano huu umeundwa rasmi ili kuongeza kasi ya ushawisi kabla ya viongozi hao kushiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28 huko Dubai baadaye mwaka huu.