Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Walinda amani wa UN kutoka Tanzania washerehekea siku yao kwa kutembelea watoto

Walinda amani wa Umoja wa MAtaifa kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wamesherehekea siku ya walinda amani duniani kwa kutembelea kituo cha watoto yatima huko Oicha jimboni Kivu Kaskazini.
UN News/George Musubao

Amani na Usalama

Kikosi cha 10 cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, TANZBATT-10 kinachohudumu kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi (FIB) kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kimeadhimisha siku ya ulinzi wa amani duniani hii leo tarehe 29 Mei kwa kutembelea kituo cha watoto yatima cha DORIKA kilichopo OICHA Jimbo la Kivu kaskazini nchini DRC. Wakiwa kituoni hapo wamewapatia misaada ya kiutu watoto hao ikiwa pia ni lengo la kulinda uhusiano na ushirikiano kwenye eneo lao hilo la uwajibikaji.

Kauli mbiu ya siku ya walilnda amani duniani mwaka huu ni "Amani inaanza Nami".

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Kamanda kikosi TANZBATT -10 Luteni Kanali John Peter Kalabaka, Meja Mtindo Ameir Mtindo ametoa wito kwa walezi wa watoto hao wasichoke kuwalea na kwamba “sisi tunaelewa umuhimu wa kazi hii mnayofanya ya kuwalea hawa watoto. Ndio maana tumekuja hapa leo kuona ni kwa vipi mnafanya kazi, na sisi kwa nafasi yetu tunaweza kuwaunga mkono. Tunaamini kwamba mafanikio ya kazi yetu yatatokana na kuungwa mkono nanyi.”

Tweet URL

Chifu wa eneo la Oicha, Kikuuu Nicola akizungumza wakati wa ziara hii ya TANZBATT-10 ametoa shukrani kwa watoto hao yatima kupata ugeni na zaidi ya yote, “unajua watoto hawa watoto hawa wana haki ya kupata malezi ijapokuwa wamepoteza wazazi wao.” 

Milio ya risasi hutishia watoto hivyo tunakimbilia mjini- Mlezi wa watoto

Mlezi wa watoto kwenye kituo hiki cha DORIKA wenye umri wa kati ya miezi 6 hadi miaka 3, Katungu Saambombili Munghanda amezungumzia changamoto wanazokabiliana nazo katika kuwalea watoto ikiwemo ukosefu wa usalama kwani “watoto wanasikia milio ya risasi wanaogopa. Inabidi tuwachukue watoto tukimbilie mjini tunalala na watoto. Pia ni vigumu kupata vyakula wakati wa sasa wa vita. Watu wanaogopa kwenda shambani kwa sababu wakienda wanaweza kuuawa na waasi.”

Ameshukuru kitendo cha walinda amani wa Tanzania kutembelea kituo hicho. “Tunafurahi sana kwa kufika kwenu na tunaomba na askari wa DRC nao watutembelee.”

Kapteni Elinaike Dauson Mkonyi Afisa Mshauri Jinsia TANZBATT-10 kwa niaba ya walinda amani wanawake ameelezea ni jinsi gani alivyoguswa na changamoto zinazowakabili walezi wa watoto hawa na kuwasihi kutokukata tamaa kwani watoto hao ni taifa la kesho.

Kapteni Mkonyi amesema “tumesema leo sio mwisho wetu kufika hapa. Tutakuja tena na tutaendelea kushirikiana nao. Ujumbe wetu ni kwamba walezi wa watoto hawa wasikate tamaa.”

Walinda amani wa Umoja wa MAtaifa kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wamesherehekea siku ya walinda amani duniani kwa kutembelea kituo cha watoto yatima huko Oicha jimboni Kivu Kaskazini.
UN News/George Musubao
Walinda amani wa Umoja wa MAtaifa kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wamesherehekea siku ya walinda amani duniani kwa kutembelea kituo cha watoto yatima huko Oicha jimboni Kivu Kaskazini.

Ulinzi wa amani ni jukumu la wanawake na wanaume

Akizungumzia mchango wa walinda amani wanawake, Koplo Fatuma Salumu Mpatila amesema “tumejifunza kwamba ulinzi wa amani si wa wanaume tu, bali walinda amani wa kike nao wanashiriki pia. Inatia moyo hata kwa raia wa kike DRC kupata matumaini kuwa inawezekana na tumezungumza nao wameona kuwa matatizo yao yanaweza kusaidiwa.

Imeandaliwa na Luteni Abubakar Muna Afisa Habari TANZBATT-10 na George Musubao Mwandishi wa Habari wa UN News, DRC