Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa UN kutoka Tanzania watoa huduma ya afya kwa wakazi wa Beni – Mavivi nchini DRC

UN News/George Musubao
UN News/George Musubao
UN News/George Musubao

Walinda amani wa UN kutoka Tanzania watoa huduma ya afya kwa wakazi wa Beni – Mavivi nchini DRC

Afya

Huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hususan mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini changamoto za usalama zimekuwa ‘mwiba’ kwa wakazi hususan kwenye kupata huduma za afya. Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu katika kikosi cha kujibu mashambulizi (FIB) cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO, kikosi cha 10, TANZBATT-10 wameona ni vema kutumia jukumu lao la ulinzi wa raia kwa kutoa pia huduma za afya na kugawa dawa kwenye hospitali ya Mavivi.

Soundcloud

Tiba sahihi hutokana na vipimo sahihi

Meja Paul Benedict, Mganga Mkuu wa kikosi hicho akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hizo kwenye hospitali ya Mavivi anasema wameamua kutoka huduma za afya kwa sababu ni majirani zao na wana uhusiano nao mzuri na ni moja ya kijiji kilicho ndani ya eneo la uwajibikaji wa TANZBATT-10. “Sisi kama walinda amani tuna jukumu kuhakikisha kuwa pia tunatoa elimu ya afya kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza ili wananchi waweze kuchukua tahadhari na kufika mapema hospitali na kupata huduma za matibabu.

Amesema “si kwamba ni hapa tu hata vijiji vingine vilivyo katika eneo letu la uwajibikaji tutakwenda ili wananchi waweze kupata elimu hii hii kuhusu magonjwa ili pindi wanapoona mapema zile dalili waweze kwenda hospitali mapema na kupata matibabu sahihi”

Tweet URL

Wanawake wa Mavivi wamefurahi kupata vipimo

Bi. Kivungo Eugenie Ngamuhanyaki kwa niaba ya Mganga Mkuu Dkt. Janvier Kanyambura wa Hospitali ya Mavivi amepokea msaada wa madawa na kutoa shukrani zake za dhati kwa walinda Amani kutoka Tanzania na amesema wamepokea vizuri kwani walikuwa wakiwa na shida nyingi kwa wanawake wanaofika kituoni wakiwa na changamoto za matibabu.

“Wanawake wamepata mafundisho mbalimbali kutoka kwa matabibu wa kitanzania. Wamefurahi sana kwani wamepata vipimo kama vile kisukari, shinikizo la damu. Dawa ambazo tumepokea kutoka TANZBATT-10 tutapatia wagonjwa kwa kuzingatia vipimo kutoka kwa madaktari hawa kutoka wanajeshi wa Tanzania.

Kathembo Mahambo Bozi kwa niaba ya Japier Bakola ambaye ni Chifu wa Beni MAVIVI jimboni Kivu Kaskaizni amefurahi sana uwepo wa walinda amani wa UN kutoka Tanzania waliofika hospitali kwa lengo la kutoa huduma ya Afya.

Amesema  “tuko vema sana na walinda amani hawa wa MONUSCO kutoka Tanzania na tunafurahi sana vitendo wanavyotutendea. Watu wote wafahamu watakaokuja wafahamu kuwa watanzania ni ndugu zetu na wanatupenda kwa matendo mbali mbali wanatufanyia. Wanatibu watu, wanachunguza magonjwa mbalimbali. Tunaomba wasichoke. Wametupatia pia dawa za kutosha. Wasichoke, waendelee.”

Tuna shida nyingi, ujio wenu unatutia moyo- Mnufaika wa huduma za TANZBATT-10

Happy Sifa ni mmoja wa wanawake wanufaika na upimaji afya ameshukuru na kusema “naishi hapa Mavivi lakini nafurahi sana kuona wajumbe wamefika hapa hospitali na kutupatia ushauri na kutupima vipimo vya aina yote kama sukari na shinikizo la damu. Sasa na sisi wanawake tumewaeleza shida yetu, hivyo tunasubiri siku nyingine waje watuambie watatufanyia nini. Siku nyingine tunasubiri waje tuongeee nao kwani sisi wanawake tuna shida nyingi, na tunasumbuliwa sana. Wasituchoke kwani ujio wao unatutia moyo sana.”

Kapteni Given Kiula Afisa na mtaalamu wa masuala ya saikoloila wa TANZBATT-10 amesema kazi kubwa waliyo nao ni kushughulikia afya ya akili ambayo huathirika na mambo mbali mbali.

Msaada wa dawa kwa hospitali ya Mavivi iliyoko mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuriya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kutoka kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye ujumbe wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO.
UN News/George Musubao
Msaada wa dawa kwa hospitali ya Mavivi iliyoko mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuriya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kutoka kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye ujumbe wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO.

Vita imeathiri afya ya akili ya wakazi wa Beni Mavivi

“Kwa wakazi wa hapa Beni Mavivi kwa sababu wao wameathirika na mambo waliyopitia ya vita, nimejaribu kuwashauri kadri ya uwezo wao wajaribu kusahau yale waliyopitia na yaliyotokea ili kusudi afya zao za akili ziweze kutengemaa na kuanza maisha upya kwenye hiki kipindi cha kuendelea na maisha ya kila siku,” amesema Kapteni Kiula.

Kapteni Elinaike Mkonyi ni Afisa Mshauri Jinsia amezungumzia masuala ya ushirikiano na mshikamano akisema uhusiano wao na wakazi wa Beni Mavivi  umekuwa mzuri vikiwemo vikundi vya wanawake ili kuwasaidia katika masuala ya kijamii ikiwemo misiba.

 

Ripoti hii imeandaliwa na Luteni  Abubakari Muna Afisa Habari TANZBATT - 10  na George Musubao UN News DRC