Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka kila nchi itie saini kutofanya majaribio ya silaha za nyuklia

Watu wakiandamana kupinga silaha za nyuklia katika  mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Geneva. (maktaba)
ICAN/Lucero Oyarzun
Watu wakiandamana kupinga silaha za nyuklia katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Geneva. (maktaba)

UN yataka kila nchi itie saini kutofanya majaribio ya silaha za nyuklia

Amani na Usalama

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi amesema kitendo cha matumizi ya kijeshi duniani kufikia dola trilioni 2.2 mwaka 2022 si ishara nzuri kwa usalama wa dunia na kutoa wito wa utashi wa kisiasa kwa nchi zote katika kuhakikisha dunia haina matumizi ya silaha za nyuklia. 

Akihutubia katika mkutano wa mashauriano kuhusu siku hii katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani Kőrösi amesema kuna maswali mengi ya kujibu.

Ametaka kila mtu kujiuliza, pamoja na matumizi makubwa ya fedha hizo kwenye shughuli za kijeshi “Je,zimewezesha kusaidia kupunguza migogoro? Je dunia iko salama zaidi sasa? Majibu ni hapana na dunia sasa ipo karibu zaidi kupata majanga kuliko awali, wakati fedha za uma zikitumika hivi ni vyema kujiuliza nikwa kiasi gani tuna dhamira ya dhati ya kumaliza umasikini, kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi, au upotevu wa bayoanuwai?”

Rais huyo 77 wa Baraza Kuu la UN amesema ili kumaliza hali hiyo mbaya kwa ulimwengu “Tunahitaji mbadala unaomlenga ubinadamu katika upokonyaji silaha. Mbadala ambao unalenga kuzuia mateso na uharibifu wa mazingira usio na maana na utatekelezwa kupitia mchakato jumuishi na thabiti wa kimataifa.”

Jaribio la nyuklia lililofanywa na Marekani katika eneo la Enewetak Atoll, Marshall Islands, 1 Novemba 1952.
US Government
Jaribio la nyuklia lililofanywa na Marekani katika eneo la Enewetak Atoll, Marshall Islands, 1 Novemba 1952.

Majaribio ya Nyuklia zaidi ya 2000

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa dunia nzima kuzungumza lugha moja ya kutotumia silaha za nyuklia na kumaliza kabisa suala la kufanya majaribio ya silaha za nyuklia kwani linaleta uharibifu wa dunia. 

Katika ujumbe wake kwa siku hii alioutoa leo jijini New York Marekani Guterres ametaja takwimu zinazoonesha kuwa tangu mwaka 1945 zaidi ya majaribio 2,000 ya silaha za nyuklia yamefanyika na kusababisha “mateso ya kutisha kwa watu, yametia sumu hewa tunayopumua, na kuharibu mandhari kote ulimwenguni.” 

Akieleza hali ilivyo duniani amesema mwaka huu dunia inakabiliwa na ongezeko la kutisha la kutoaminiana na mgawanyiko kwani kuna takriban silaha za nyuklia 13,000 zimehifadhiwa duniani kote huku nchi zikiendelea kufanya kazi ya kuziboresha ili ziweze kuleta uharibifu zaidi na kusema hiki “ni kichocheo cha maangamizi.”

Ili kuondoa dunia katika hali hii ya wasiwasi na kuwakuthamini waathirika za silaha za nyuklia Katibu Mkuu Guterres ametoa wito kwa nchi zote kutia saini mkataba wa kusitisha majaribio ya silaha za nyuklia.

Guterres anaamini kwamba “marufuku ya kisheria ya majaribio ya nyuklia ni hatua ya kimsingi katika harakati za kutafuta ulimwengu usio na silaha za nyuklia.” 

Amesema mkataba huu unaopiga marufuku ya kufanya majaribio ya silaha za Nyuklia, ingawa bado haujatekelezwa, unasalia kuwa ushuhuda wenye nguvu wa nia ya wanadamu ya kuiondoa dunia katika kivuli cha maangamizi ya nyuklia mara moja na kwa wote.