Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watoto 300,000 wakimbizi wa kipalestina warejea shuleni

Watoto wa Kipalestina wanarejea shuleni katika Ukanda wa Gaza.
© UNRWA/Mohamed Hinnawi
Watoto wa Kipalestina wanarejea shuleni katika Ukanda wa Gaza.

Takriban watoto 300,000 wakimbizi wa kipalestina warejea shuleni

Haki za binadamu

Takriban watoto 300,000 Wakimbizi wa Kipalestina wamerejea shuleni katika Ukanda wa Gaza. Taarifa kutoka mjini Gaza iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA imemnukuu Mkurugenzi wa Masuala ya URWA Thomas White akifurahi kuwaona watoto wakirejea shuleni. 

Whites amesema kuwa “Ilipendeza kuona jinsi watoto wanavyofurahi kurudi shuleni. Huko Gaza (Katika shule zinazoendeshwana na UNRWA) kwa watoto wengi shule zimekuwa mojawapo ya maeneo machache sana ambapo watoto wanaweza kuwa hivyo tu, watoto. Ni mahali ambapo wanajifunza, kustawi, kucheza, kutengeneza marafiki na kushirikia shughuli za nje.” 

Ili kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka miongoni mwa jumuiya za wakimbizi katika Ukanda wa Gaza, UNRWA iko katika mchakato wa kuteua zaidi ya walimu 500 wapya kusaidia watoto kupata elimu bora.

Na ili kuweza kuhimili ongezeko la zaidi ya watoto 4,600 waliojiunga na shule mwaka huu, UNRWA hivi karibuni imefungua shule tatu mpya kusini mwa Ukanda wa Gaza na katika Jiji la Gaza. Shule hizi zitasaidia kutoa nafasi salama kwa wanafunzi kujifunza na kufanikisha ndoto zao.

Whites amehitimisha taarifa yake kwa kukumbusha ahadi ya UNRWA katika kuendeleza elimu na kusema hicho ni kipaumbele chao cha kwanza, hata katika mazingira magumu. “Tuna nia ya kuwapatia watoto wakimbizi wa Kipalestina elimu ya hali ya juu, kuwapa stadi za maisha wanazohitaji ikiwa ni pamoja na kuweza kupata ajira na kujiunga na soko la ajira katika siku zijazo.”