Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utoro wa shule kwa vijana barubaru Palestina ni tishio kwa mustakhbali wa taifa hilo.

Watoto ni waathirika wa mashambulizi kama hapa shule ya wasichana iliyosambaratishwa kwa mabomu huko Shuja'iyeh, mashariki mwa mji wa Gaza.
UNICEF/Eyad El Baba
Watoto ni waathirika wa mashambulizi kama hapa shule ya wasichana iliyosambaratishwa kwa mabomu huko Shuja'iyeh, mashariki mwa mji wa Gaza.

Utoro wa shule kwa vijana barubaru Palestina ni tishio kwa mustakhbali wa taifa hilo.

Haki za binadamu

Takribani asilimia 25 ya barubaru wavulana wenye umri wa miaka 15 wa kipalestina  huko Ukanda wa Gaza ni watoro wa shule.

Ripoti ya hivi karibuni zaidi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iliyotolewa kwa ushirikiano na UNESCO  na wizara ya elimu ya Palestina  imetaja sababu za utoro kuwa ni viwango duni vya elimu, migogoro ya kivita, njaa , kero za ukaguzi katika vituo vya ukaguzi, umasikini na pia tatizo la usalama ambalo huwafanya walimu kutojitolea kikamilifu.
 
Tatizo la ukaguzi uliopita kiasi linasimuliwa na Marawan, mvulana mwenye umri wa miaka 14 ambaye hupitia vituo vya ukaguzi kila siku anapokwenda shuleni na kurudi nyumbani.
 
Marawan anasema yeye na mwenzake Hamid hulazimishwa kupita mara mbili kwenye vituo vya ukaguzi viitwavyo H2 , ambavyo ni mahususi kwa ajili ya uchunguzi wa silaha, mabomu na vyuma hatari vinavyoweza kudhuru binadamu katika maandamano.

Kuhusu mazingira duni ya elimu, ripoti inasema zaidi ya theluthi mbili ya watoto wa kati ya darasa la 1 hadi la 10 wanakumbwa na ghasia za kihisia na kimwili wanapokuwa shuleni.

Kama hiyo haitoshi, mwaka 2017, zaidi ya wanafunzi 29,000 walikatisha masomo kufuatia visa 170 vilivyotokea shuleni ikiwemo mashambulizi yaliyosababishwa na mzozo uliodumu kwa muda mrefu.

Pia imeeleza kuwa kutokana na uchache wa madarasa na walimu , asilimia 90 ya wanafunzi wamegawanywa katika makundi mawili ambapo yanasoma kwa awamu ya kupishana.
 
Ili kukabiliana na hali hiyo, ripoti inasema ni muhimu kusaka njia mbadala za kuwapatia watoto elimu kwenye maeneo mengine badala ya shuleni na kuongeza ubora na huduma za usaidizi wa kimwili na kisaikolojia kwa watoto.