Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuongezeka kwa mapigano kuna hatarisha hali za wenye VVU: UNAIDS

Mlinda amani kutoka Timu ya kuwahusisha wanawake ya MONUSCO akisambaza barakoa katika kijiji cha Walungu nchini DR Congo
MONUSCO
Mlinda amani kutoka Timu ya kuwahusisha wanawake ya MONUSCO akisambaza barakoa katika kijiji cha Walungu nchini DR Congo

Kuongezeka kwa mapigano kuna hatarisha hali za wenye VVU: UNAIDS

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na harakati za kutokomeza uKimwi, UNAIDS limesema lina wasiwasi mkubwa kwamba kuongezeka kwa ghasia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC kunatishia huduma za matibabu na kuzuia kuwatibu watu wenye Virusi Vya UKIMWI, VVU.

Taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo kutoka Geneva Uswisi na Kinshasa DRC imesema kuwa mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi huko mashariki mwa DRC yanasababisha usumbufu mkubwa na madhara kwenye utoaji huduma za matibabu, kinga na matunzo kwa watu wanaoishi na walioathiriwa na VVU.

Mkurugenzi wa UNAIDS Susan Kasedde amesema “Nina wasiwasi mkubwa kuhusu afya na ustawi wa watu wanaoishi na walioathirika na VVU katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano na katika jamii zinazowapokea wale ambao wamekimbia mapigano. Huenda watu walilazimika kuondoka majumbani mwao kwa haraka na hawakuchukua dawa muhimu.”

Pia ameeleza wanaunga mkono kikamilifu wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama uliotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, na Umoja wa Afrika.

Hali za wenye VVU

Katika vituo vya afya vya Rutshuru na Rwanguba ambako baadhi ya mapigano makali yameripotiwa, Mpango wa Kudhibiti UKIMWI (PNLS) huko Kivu Kaskazini umesajili watu 1155 wanaoishi na VVU wanaopatiwa matibabu kwa sasa wakiwemo wajawazito 102 na watoto 46.

Bi. Kasedde amezungumzia kundi maalum la wanawake wanaoishi na VVU “Nina wasiwasi hasa kuhusu hali za akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanaoishi na VVU na watoto wao wachanga. Kukatizwa kwa matibabu kwa akina mama hawa itakuwa na athari mbaya kwa watoto wao wachanga. Hizi ni mbio dhidi ya wakati na lazima tufanye kila tuwezalo kuwatafuta wanawake hawa kwa haraka na kuwaunganisha na huduma.”

Huku ghasia zikiongezeka, idadi kubwa ya watu inaelezwa wamekimbia makazi yao na wengi wao wakielekea kusini, katika jimbo la Goma.

Nini kinafanyika kwa sasa

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeeleza kuwa linafanya kazi kwa karibu na wasimamizi wa programu za kitaifa za VVU, mashirika ya kiraia, mashirika ya kijamii na washirika wote kusaidia wakati huu wa dharura kutokana na mapigano.

Mosi, Kuhakiki idadi ya watu wanaoishi na VVU wanaopata matibabu kwa sasa ili kujua mahitaji yao na kuweka mipango endelevu katika jamii zilizoathirika za Rutshuru na Rwanguba na katika jamii zinazowapokea.

Pili, Kufanya tathmini kwakushirikiana na mashirika mengine ya kibinadamu ili kuwezesha ujumuishaji wa huduma zinazohusiana na VVU katika mwitikio wa pamoja. Hii ni pamoja na kufanya kazi na mashirika washirika ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na UNOCHA, UNICEF, WFP, UNFPA na UNHCR kukusanya taarifa kutoka kwa mashirika ya kiraia ili kuelewa mahitaji na uwezo katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro na jumuiya zinazohifadhi watu waliokimbia makazi yao.

Tatu, Kujenga upya mitandao ya usaidizi wa jamii kwa kuwasiliana na vituo muhimu vya asasi za kiraia, mashirika ya kijamii kama vile akina mama washauri, na watoa huduma ili kuanzisha mtandao wenye uwezo wa kusaidia kufuatilia na kuwatafuta watu wanaoishi na VVU na kuwasaidia waendelee kupata  huduma za VVU ikiwa ni pamoja na huduma za kisaikolojia na kijamii kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia, na msaada wa lishe ili kuwezesha matibabu yao ya VVU.

Na Nne, Kuunga mkono juhudi za ngazi ya kijamii ili kuhakikisha wanafikisha ujumbe wenye ufanisi zaidi kwa watu wanaoishi na VVU unaohusiana na ulinzi wa haki za watu wanaoishi na VVU.

UNAIDS pia inaendesha harakati za utetezi ili kuimarisha ujumuishaji wa mahitaji ya VVU katika kukabiliana na dharura.