Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yasema wasichana wa Afghanistan kuzuiwa kuhudhuria Chuo Kikuu ni pigo jingine la kikatili kwa haki za wanawake na wasichana

Wasichana wakiwa darasani katika Kituo cha Kujifunza cha Kasi katika Mkoa wa Wardak katika mkoa wa kati wa Afghanistan.
© UNICEF/Christine Nesbitt
Wasichana wakiwa darasani katika Kituo cha Kujifunza cha Kasi katika Mkoa wa Wardak katika mkoa wa kati wa Afghanistan.

UN yasema wasichana wa Afghanistan kuzuiwa kuhudhuria Chuo Kikuu ni pigo jingine la kikatili kwa haki za wanawake na wasichana

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umetaka mamlaka za watalibani nchini Afghanistani kubadili uamuzi wake wa kuzuia wasichana kujiunga na elimu ya Vyuo Vikuu nchini humo, tangazo ambalo limetolewa na taifa hilo la barani Asia Jumanne wiki hii ikiwa ni miezi tisa tangu watangaze kuzuia wasichana kuendelea na elimu ya sekondari.

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne usiku na na msemaji wake jijini New York, Marekani amesema anasikitishwa na taarifa ya kwamba mamlaka hizo zilizojiingiza zenyewe madarakani zimezuia fursa ya wasichana na wanawake ya kujiunga na Vyuo Vikuu.

Amelaani kitendo hicho akisema “kuwanyima elimu hakukiuki tu haki za usawa kwa wanawake na wasichana, bali pia kutakuwa na madhara makubwa kwa mustakabali wa taifa hilo.”

Ametaka mamlaka hizo zilizojiweka zenyewe madarakani zihakikishe kuna fursa sawa ya elimu kwa wanawake na wasichana katika ngazi zote za elimu.

Kamishna Mkuu wa Haki UN naye apaza sauti

Naye Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametoa maoni kufuatia taarifa zilizotolewa jana ya kuwa Mamlaka ya Afghanistan imepiga marufuku wanawake kuhudhuria chuo kikuu nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo kutoka Geneva Uswisi na ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imesema Kamishna Turk ametoa maoni kuhusu uamuzi huo wa Taliban na kusema ni pigo jingine baya na la kikatili kwa haki za wanawake na wasichana wa Afghanistan na kurudisha nyuma huzuni kubwa kwa nchi nzima.

“Kusimamishwa kwa ushiriki wa wanawake katika elimu ya juu na Vyuo Vikuu ni ukiukaji wa wazi wa majukumu ya Afghanistan chini ya sheria za kimataifa. Haki za wanawake na wasichana kupata ngazi zote za elimu bila kubaguliwa ni za msingi na zisizo na shaka.” Amesema Kamishna Turk na kuongeza kuwa “Ninatoa wito kwa mamlaka za Afghanistan, mara moja kubadili uamuzi huu na kuheshimu kikamilifu na kuwezesha haki ya wanawake na wasichana kupata elimu katika ngazi zote. Kwa ajili yao na kwa ajili ya jamii nzima ya Afghanistan.”

Hatua hii ni kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu

Ameeleza zaidi kuwa kuwatenga kimfumo wanawake na wasichana karibu nyanja zote za maisha, ni kwenda kinyume na ulimwenguni tuliopo.

“Kuwatenga wanawake kutoka elimu ya juu ni jambo la kuvunja moyo zaidi kwa kuzingatia mchango muhimu ambao wanawake wa Afghanistan wametoa katika maeneo mengi ya kitaaluma na ufundi kwa miaka mingi.”

Amezungumzia utajiri wa kuwaelimisha wasichana na kusema kuwa kuwazuia wasichana kuhudhuria shule za sekondari, kunapoteza fursa nzuri ya kuwa na madaktari wa kike, wanasheria na walimu ambao wananchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.