Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je wamfahamu mtaalamu wa Akili Mnemba awezaye kuwa kwenye jopo la UN ?

Msichana akiwasiliana na roboti mjini Osaka Japan
© Unsplash/Andy Kelly
Msichana akiwasiliana na roboti mjini Osaka Japan

Je wamfahamu mtaalamu wa Akili Mnemba awezaye kuwa kwenye jopo la UN ?

Masuala ya UM

Umma sasa umepatiwa fursa ya kuteua wataalamu watakaohudumu kwenye Jopo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu la ushauri kuhusu Akili Mnemba, jopo ambalo limeitishwa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Kuteua mtu bofya hapa kujaza fomu

Guterres alitangaza kuitisha jopo hilo wakati akihutubia Baraza la Usalama tarehe 18 Julai mwaka huu akisema jopo hilo pamoja na mambo mengine litaandaa mikakati ya kitaifa katika uundaji wenye uwajibikaji, maendeleo na matumizi ya AI, kwa mujibu wa sheria za kiutu za kimataifa na sheria za haki za binadamu.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farham Haq amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani akifafanua kuwa majina hayo pendekezwa yawasilishwe kuanzia sasa hadi tarehe 31 mwezi huu wa Agosti.

Jopo hilo pia litafanya uchambuzi na kusongesha mapendekezo ya usimamizi wa kimataifa wa Akili Mnemba, na kuwasilisha mbinu za usimamizi wa Akili Mnemba ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023.

Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Teknolojia, Amandeep Singh Gill, amesema “tunahitaji kuleta pamoja utaalamu wa nyanja mbali mbali kuhusu Akili Mnemba kuhakikisha kuwa inaendana na Chata ya Umoja wa Mataifa, haki za binadamu, utawala wa sheria na maslahi kwa wote.”

Wataalamu watakaoteuliwa, wanapaswa kuwa na utaalamu mahsusi na kuongoza kwenye tasnia mbali mbali zinazohusiana na Akili Mnemba au matumizi yake.