Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akili Mnemba kuchukua zaidi ajira za ukarani tofauti na idhaniwavyo – ILO

Utafiti wabaini kuwa ajira na viwanda vingi kunufaika na Akili Mnemba lakini ajira kama za ukarani zitachukuliwa na Akili Mnemba kwa kiasi fulani.
© Unsplash/Steve Johnson
Utafiti wabaini kuwa ajira na viwanda vingi kunufaika na Akili Mnemba lakini ajira kama za ukarani zitachukuliwa na Akili Mnemba kwa kiasi fulani.

Akili Mnemba kuchukua zaidi ajira za ukarani tofauti na idhaniwavyo – ILO

Utamaduni na Elimu

Utafiti mpya uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO umebaini kuwa matumizi ya Akili Mnemba au (Artificial Intelligence- AI) yanaongeza fursa za ajira kwa binadamu badala ya kuzisambaratisha tofauti na fikra zilizoshamiri ya kwamba matumizi ya AI yataondoka kabisa jukumu la binadamu.

Utafiti huo Akili Mnemba na Ajira: Uchambuzi wa kimataifa juu ya madhara ya AI kwenye idadi na aina za ajira umechapishwa leo na ILO huko Geneva, Uswisi ukidokeza kwamba ajira nyingi na viwanda vinakabiliwa na kiwango kidogo cha matumizi ya mashine zenye Akili Mnemba yakiwemo maroboti na kwa kiwango kikubwa itahitajika binadamu kuweko sambamba na mashine hizo badala ya fikra kwamba binadamu hatohitajika tena.

“Kwa hiyo athari kubwa ya teknolojia hii inaweza kuwa sio kuondoa ajira za binadamu bali uwezekano wa mabadiliko ya ubora wa ajira, hasa kwenye kazi za mtulinga na zinazotegemea fikra za mfanyakazi,” imesema ILO ikinukuu utafiti huo.

Kazi za Ukarani

Utafiti huo umegundua kuwa ajira ya ukarani inaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na teknolojia ya Akili Mnemba ambapo robo ya kazi afanyazo karani zinaweza kufanywa na mashine huku zaidi ya nusu zikitegemea binadamu na mashine.

Hata hivyo kazi ya umeneja, ufundi na zenye ueledi zitaathirika kidogo mno na uwepo wa teknolojia ya AI.

Athari za AI kwa nchi maskini ni ndogo mno

Utafitu huo uliowakilisha sampuli kutoka dunia nzima umebaini tofauti kati ya nchi za kipato cha juu na cha chini ukimulika miundo ya sasa ya kiuchumi na pengo la teknolojia.

Kwa nchi za kipato cha juu ni asilimia 5.5 tu ya ajira zote itakumbwa na Akili Mnemba ilihali kwa nchi za kipato cha chini Akili Mnemba inaweza kuchukua asilimia 0.5 ya ajira.

Hata hivyo kwa upande mwingine, utafiti umegundua kuwa iwapo nchi zitakuwa na sera sahihi, mwelekeo mpya wa mabadiliko ya kiteknolojia yanaweza kuwa na manufaa makubwa kwa nchi zinazoendelea.

Wanawake wengi wako kwenye ukarani hivyo kuathiriwa zaidi na AI

Kijinsia, Akili Mnemba itaathiri zaidi ajira zinazoshikiliwa na wanawake ikilinganishwa na wanaume ambapo utafiti unaonesha kuwa hiyo inatokana na ukweli kwamba wanawake ni wengi kwenye ajira za ukarani kuliko wanaume.

Waandishi wa ripoti ya utafiti huu wanasema changamoto iliyoko sasa ni binadamu kuwa nyuma katika kuingia kwenye mpito wa teknolojia na hivyo kinachotakiwa ni binadamu kuongoza mpito huo badala ya kuchelea.