Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimesikia maombi yenu na tutapaza sauti – Naibu Katibu Mkuu akiwa Amazon

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, atembelea jumuiya ya Mapuera katika jimbo la Pará, Brazil.
UN Brazil
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, atembelea jumuiya ya Mapuera katika jimbo la Pará, Brazil.

Nimesikia maombi yenu na tutapaza sauti – Naibu Katibu Mkuu akiwa Amazon

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Akiendelea na ziara yake nchini Brazil, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amewahakikishia watu wa jamii ya asili ya Mapuera kwenye jimbo la Pará nchini humo ya kwamba amesikia kilio chao na zaidi ya yote Umoja wa Mataifa utahakikisha sauti zao zinasikilizwa kwani wanachodai ni haki zao za msingi.

Bi. Mohammed amesema hayo wakati akizungumza na wakazi hao Alhamisi ya tarehe 3 mwezi huu wa Agosti ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano nchini Brazil.

Jamii ya Mapuera wakitumbuiza wakati Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed alipowatembelea.
UN Brazil
Jamii ya Mapuera wakitumbuiza wakati Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed alipowatembelea.

Amewaeleza wanajamii hao kuwa “nami pia natoka kabila la jamii ya watu wa asili Afrika, kwa hiyo naelewa thamani ya sauti ya watu wa jamii ya asili.” 

Bi. Mohammed ambaye ziara yake ilianzia mji mkuu wa Brazil, Brasilia na kisha kutembelea hapa Amazon akaenda mbali akisema, ziara yake isingalitimia bila kufika ukanda wa Amazon. “natembelea Brazil, lakini kutembelea Brazil bila kufika Amazon, si kutembelea Brazil.” 

Naibu Katibu Mkuu akaendelea na hotuba yake huku pembeni yake mkalimani akitafsri kwa lugha ya wakazi wa eneo hili. Bi. Mohammed akasema,na kwa hiyo basi, niko hapa leo kuwasikiliza, kuwaona, kupata hisia zenu na kwa yale mambo ambayo mmeulizia na yale mambo ambayo ni haki yenu. Na hatimaye kuchukua sauti hizi hadi Brasilia, Belém, New York na duniani kwa ujumla.” 

Mathalani Mkuu wa jamii hii ya asili na kiongozi mwingine wa wanawake waliomba usafiri, teknolojia, ardhi na huduma za msingi ambapo Naibu Katibu Mkuu amesema yote hayo si jambo la kuomba na kupatiwa kwa upendeleo bali ni haki zao kupatiwa vitu hivyo. 

“Na kwa hiyo, Umoja wa Mataifa utabeba sauti zenu, tutapazia sauti kile tunachosikia, tunachoona na tunashikamana nanyi, na wale wanaofanya kazi Brazil, wale wanaofanya kazi mjini Santarém, wanaofanya kazi mjini Belém, ili hatimaye siku moja tufanikishe upatikanaji wa hizo haki.”