Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo wa asili wa kilimo Brazil watambuliwa kimataifa

Kwenye safu ya milima ya Espinhaço katika jimbo la Minas Gerais nchini Brazil, wakulima hawa hupanda kwenye milima hiyo na kuchuma maua hayo ya Sempre-Vivas
FAO/Fernanda Testa Monteiro
Kwenye safu ya milima ya Espinhaço katika jimbo la Minas Gerais nchini Brazil, wakulima hawa hupanda kwenye milima hiyo na kuchuma maua hayo ya Sempre-Vivas

Mfumo wa asili wa kilimo Brazil watambuliwa kimataifa

Utamaduni na Elimu

Nchini Brazil mfumo wa kilimo cha asili kinachohusisha wakulima wachumao maua milimani umetambuliwa kama mfumo muhimu wa urithi wa kilimo duniani, GIAHS.
 

Taarifa ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO iliyotolewa leo huko Roma, Italia imesema kilimo hicho hufanyika kwenye maeneo ya milima ya  Espinhaço iliyoko jimbo la Minas Gerais kusini mwa Brazil.
Kwa mujibu wa FAO hii ni mara ya kwanza kwa eneo la Brazil kutambuliwa chini ya mfumo huo wa kilimo cha urithi.
Katika miteremko ya milima hiyo maua hayo ya Sempre-Vivas huchumwa katika mtindo ambao husaidia kutunza bayonuai na unyeshaji wa mvua.
Wakulima wa eneo hilo wakijulikana pia kama wachumaji wa maua ya Sempre-vivas wameendeleza mfumo fanisi wa kilimo uhusishao ukusanyaji maua, bustani za kilimo na misitu, uchungaji wa mifugo, na kilimo, vyote hivi vikifanyika eneo la milimani lililo mita 1400 kutoka usawa wa bahari.
“Mfumo huu mgumu wa kilimo unatokana na aina mbalimbali za mbinu za kijadi na hatua zilizoendelezwa kutoka kizazi hadi kizazi kusaidia watu kufanikisha kuishi kwa amani na mazingira yao huku wakihakikisha kuwa uhakika wa chakula na mbinu bora za kujipatia kipato,” imesema taarifa hiyo.
Mratibu wa GIAHS Yoshihide Endo amenukuliwa akitoa shukran akisema kuwa, “ni kutokana na uelewa wa kina wa mienendo ya kiasili na bayonuai yao wakazi wa maeneo hayo ya milimani kwa kutumia ufahamu wao wa kiasili wametambua aina za udongo, tabianchi na eneo lao la kijiografia ili kuendeleza maisha yao.”
Amesema kuwa shughuli zao pia zinachangia katika kuhifadhi aina mbalimbali za mazao, uoto wa asili na mwonekano wa ardhi katika eneo lao.
Katika mfumo huo, wakazi wa eneo hilo la milimani nchini Brazil wanafanya shughuli kuanzia kukusanya, kuchakata na kutunza maua ya asili huko milimani, ufugaji wa asili wa mifugo kupitia maeneo ya zamani ya kupitisha mifugo yao waliyotumia karne na karne, ukusanyaji wa matunda, mbegu na mimea ya dawa, na kuhifadhi bustani zao za milimani.
Bayonuai ya kipekee ya kilimo
Takribani asilimia 90 ya mazao yanayolimwa kwenye milima ya Espinhaço ni pamoja na mboga, miti ya matunda, mimea ya mizizi na vingine vingi.
Kila jamii katika eneo hilo inadhibiti maua ya asili na hupandwa kwa kuzingatia mzunguko wa kiasili ili kuhakikisha utunzaji na uendelevu wa kila aina ya mbegu.
Programu ya GIAHS 
Kujumushwa kwa mfumo wa kilimo cha wachuma maua huko Brazil, kunafanya idadi ya mifumo ya kilimo cha urithi kufikia 59 na ni kutoka katika nchi 22.
Maeneo mengine ni mfumo wa matumizi ya ardhi au Kihamba mkoani Kilimanjaro.
TAGS: GIAHS, Espinhaço, Brazil, Sempre-vivas