Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Simulizi Yangu: Kuishi na Homa ya Ini aina ya C nchini Afrika Kusini

Koketso Mukubani akisimama nje ya Kituo cha Matibabu cha Sediba Hope huko Tshwane, Afrika Kusini. Anasema wanaotumia dawa za kulevya wanapaswa kujumuishwa kwenye mipango na utekelekezaji wa kinga, tiba na huduma dhidi ya VVU na Homa ya ini C.
© UNODC
Koketso Mukubani akisimama nje ya Kituo cha Matibabu cha Sediba Hope huko Tshwane, Afrika Kusini. Anasema wanaotumia dawa za kulevya wanapaswa kujumuishwa kwenye mipango na utekelekezaji wa kinga, tiba na huduma dhidi ya VVU na Homa ya ini C.

Simulizi Yangu: Kuishi na Homa ya Ini aina ya C nchini Afrika Kusini

Afya

Koketso Mokubane, mwanaume huyu raia wa Afrika Kusini alibainika kuwa na Homa ya Ini C. Amesimama nje ya kituo cha matibabu cha Sediba Hope kwenye kitongoji cha Tshwane. Koketso anafanya kazi ya kwenye ofisi ya Mtandao wa Watu wanaotumia dawa za kulevya nchini Afrika Kusini. Hili ni shirika lisilo la kiserikali linalopata msaada kupitia ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na Dawa na Uhalifu, (UNODC) kwa lengo la kutetea haki za watu wanaotumia dawa za kulevya.

Koketso amezungumza na UNODC kuelekea siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu Homa ya Ini inayoadhimishwa tarehe 28 mwezi Julai kila mwaka. Anazungumzia jinsi alivyotambua anaugua Homa ya Ini C, wakati wa kampeni ya kubadilishana damu kwa bomba la sindano, ambapo watu wanaotumia dawa za kulevya hupatiwa mabomba ya sindano ambayo hayajatumika.  

Koketso Mukubani akipokea dawa za matibabu methadone katika Sediba Hope.
© UNODC
Koketso Mukubani akipokea dawa za matibabu methadone katika Sediba Hope.

Niligundua kuwa nina Homa ya Ini C nikiwa kwenye hili jingo.  

Mwaka 2017, nilikuwa ninashiriki kwenye programu ya rika ya kubadilishana sindano, huko Marabastad. Nilijiulishwa kuhusu program hii katika ofisi ya Sediba Hope ya kwamba unatoa damu na kisha unapatiwa fedha.  

Nikiwa na umri wa miaka 14, mama yangu alifariki dunia kwa UKIMWI. Hapo ndipo nilianza kutumia dawa za kulevya. Nilipata uraibu. Halikadhalika kwa nyanya yangu. Wiki moja tu baada ya kifo cha mama yangu,  babu yangu naye alifariki dunia. Hivyo nyanya au bibi yangu alianza kuwa mlevi kupindukia na akauza nyumba yetu kwa sababu hakuweza kuishi ndani kwani ilikuwa inamrejeshea kumbukumbu.  

Wakati huo, nilikuwa navuta bangi, kwa madai ya kuwa nitakonda kwa sababu nilikuwa mnene. Lakini baada ya kifo cha mama yangu, nilizidi kutumia zaidi ili angalau kupunguza mawazo, kisha nikaanda kunywa pombe kupindukia, nikaacha bangi nikarukia Heroine  hadi chochote kile ambacho ningaliweza kukipata.  

Maisha yangu yalikuwa mabaya kupindukia nikishindwa kujidhibiti. Tulihamia Kijiji ambako huko sikuweza kuendana na Maisha yake. Basi nikakimbilia mtaani na wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 20.  

Kubainika na ugonjwa  

Katika kituo cha tiba, sikufahamu kuwa damu yangu wangaliitumia kufanyia nini. Motisha ya kutoa damu ilikuwa ni fedha ili nijikimu mahitaji yangu. Kwa hiyo nilienda. Walinieleza kuwa wanachunguza VVU, halikadhalika Homa ya Ini B na C.  

Nilipata mshtuko wa maisha pindi waliponieleza nina virusi vya Homa ya Ini C. sikufahamu ugonjwa huo ni nini, na hivyo niliogofya sana.  

Wanasema kuwa wanaume hawalii, lakini sikuweza kuzuia machozi yangu. 

Mhudumu wa afya alikuwa na huruma. Alinituliza, akanifafanulia kuhusu ugonjwa huo na zaidi ya yote ninaweza kuudhibiti kwa kubadilisha mfumo wa maisha.  

Nilijilaumu mwenyewe. Nilipata maambukizi kupitia matumizi holela ya dawa za kulevya.  

Uweko wa ugonjwa huu kwa watu wanaotumia dawa za kulevya ni asilimia 80. Nilirejea mtaani nikaendelea kutumia dawa za kulevya huku fikra hizo zikiwa zimesheheni kichwani mwangu.  

Hepatitis C huathiri kwa kiasi kikubwa makundi yaliyotengwa ikiwa ni pamoja na watu wanaojidunga dawa za kulevya.
Unsplash/Diana Polekhina
Hepatitis C huathiri kwa kiasi kikubwa makundi yaliyotengwa ikiwa ni pamoja na watu wanaojidunga dawa za kulevya.

Kuanza kudhibiti  

Nilitaka kudhibiti uraibu wangu wa dawa za kulevya, na kuwa na afya bora.   

Nilijiunga na Programu ya kijamii ya kudhibitia matumizi ya dawa za kulevya katika Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini ambako nilianza kutumia dawa mbadala wa afyuni, (OST). 

Dawa hizo ni Methadone ambapo nilianza kutumia ili kupungua uraibu wa afyuni. Walichukua tena damu yangu kupima iwapo kuna mabadiliko.  

Sikukosa hata siku moja. Baada ya programu ya wiki 12, walichukua tena vipimo vya damu na kwa mara nyingine tena ikaonekana virusi vimekwisha. Hapo  hapo nikapatiwa chanjo dhidi ya Homa ya Ini B.  

Nilifurahi sana na kuona ahueni kubwa kwa sababu programu hii ilienda sambamba na ujumuishaji kwenye familia. Nilianza tena uhusiano na wapendwa wangu, lakini kwa sababu ya unyanyapaa, sikuweza kuwaeleza kuhusu hali yangu ya kiafya.  

Familia  yangu ilibaini lini nilibainika sina tena virusi. Nina furaha kuwa waligundua wakati tayari sina tena virusi. Kwa sababu hofu pekee ilikuwa ni unyanyapaa. Unyanyapaa unaweza kunitibua kiasi kwamba naweza kurejea tena mtaani au kuanza kutumia dawa kwa kiasi kikubwa kuliko awali.  

Kinachotakiwa  

Tunahitaji programu ya kina ya kupunguza athari, ambayo iko tayari na inaweza kufikiwa na watu wote nchini Afrika Kusini. Tunahitaji kuimarisha programu za mashinani za ubadilishaani sindano, mbadala wa afyuni, matibabu na huduma za uchunguzi.  

Tunahitaji kujumuisha watu wanaotumia dawa kwenye mipango na utekelezaji wa miradi yote inayohusiana na afya, hasa ile miradi ambayo inaonekana kuwa itawahusu wao.  

Wao pia ni muhimu katika kuvunja fikra potofu na kubainisha manufaa ya matibabu. Wanapaswa kuajiriwa kwenye kampeni, usambazaji wa sindano na kadhalika. Sisi watu tunaotumia dawa za kulevya tunafanya kazi za kujitolea, lakini ni kazi halisi. Tuna haki ya kupatiwa malipo kama wahudumu wa afya wanaofanya kazi hiyo hiyo. 

Homa ya ini aina C ni ugonjwa unaoenezwa na kwa njia ya damu na ukiachwa bila kutibiwa, unaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa ini na hata saratani. 

Maendeleo ya hivi karibuni yamesaidia matibabu madhubuti kupatikana katika nchi nyingi za kipato cha chini na cha kati, ambako asilimia 80 ya watu walio na ugonjwa huu wanaishi.