Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka Rais wa Niger aachiliwe huru bila masharti yoyote

Rais Mohamed Bazoum wa Niger akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu mwezi Septemba 2022.
UN Photo/Cia Pak
Rais Mohamed Bazoum wa Niger akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu mwezi Septemba 2022.

UN yataka Rais wa Niger aachiliwe huru bila masharti yoyote

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali kitendo cha serikali ya Rais Mohamed Bazoum kuondolewa madarakani kinyume cha katiba nchini Niger, kitendo ambacho kimetangazwa jumatano ya tarehe 26 Julai, 2023 na jeshi nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa unalaani vikali mashambulizi dhidi ya serikali yoyote iliyoingia madarakani kidemokrasia na kwamba “ hebu tueleweke tunaunga mkono juhudi za ECOWAS na Muungano wa Afrika za kurejesha demokrasia.”

ECOWAS ni Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ambako Niger moja ya nchi wanachama, jana jeshi limetwaa madaraka na hii leo imethibitishwa kuwa Rais wa nchi hiyo Bazoum amewekwa korokoroni na wanajeshi hao.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuhusu hali inayoendelea nchini Niger.
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuhusu hali inayoendelea nchini Niger.

Nilizungumza na Rais Bazoum jana na leo nina  ujumbe kwa wanaomshikilia

Katibu Mkuu amesema “jana nilizungumza na Rais Bazoum kumwelezea mshikamano wetu kamilifu. Na leo nataka kuzungumza moja kwa moja na wale wanaomshikilia: Mwachieni huru Rais Bazoum bila masharti yoyote. Achene kuzuia utawala wa kisheria wa nchi na heshimuni utawala wa kisheria."

Guterres amesema kinachoshuhudiwa sasa kwenye ukanda huo wa Afrika Magharibi ni mwenendo unaochukiza. Mfululizo wa uondoaji serikali madarakani kinyume cha katiba ambao una madhara kwa maendeleo na Maisha ya raia. 

Amesema hali hiyo inashuhudiwa zaidi kwenye nchi ambazo tayari zina mizozo, misimamo mikali, halikadhalika madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Rais Bazoum aachiliwe huru

Wanufaika wa programu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP ya kugawa msaada wa chakula chenye lishe kwenye kijiji kimoja eneo la Zinder nchini Niger
© WFP/Simon Pierre Diouf
Wanufaika wa programu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP ya kugawa msaada wa chakula chenye lishe kwenye kijiji kimoja eneo la Zinder nchini Niger

Mapema taarifa iliyotolewa Jumatano usiku na msemaji wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ilimnukuu Katibu Mkuu akieleza wasiwasi wake mkubwa kufuatia taarifa za kuswekwa korokoroni kwa Rais wa Niger Mohamed Bazoum na zaidi ya yote ana hofu juu ya usalama na ustawi wake.  

Ametoa wito kwa wahusika wa kitendo hicho cha kuchukiza kumwachia huru Rais huyo mara moja na bila masharti yoyote.  

“Katibu Mkuu ametoa wito kwa kukoma kwa vitendo vyovyote vinavyodidimiza misingi na kanuni za kidemokrasia nchini Niger. Amesihi pande zote zijizuie kufanya ghasia na badala yake ziheshimu utawala wa sheria.” Imesema taarifa hiyo.  

Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unashikamana na serikali iliyochaguliwa kidemokrasia nchini Niger pamoja na wananchi wake. 

Türk alaani jaribio la mapunduzi ya kijeshi Niger

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ameshtushwa, amehuzunishwa na kulaani vikali jaribio la kutaka kutwaa madaraka kijeshi nchini Niger lililofanyika hapo jana. 

Türk ametaka Rais wa Niger Mohamed Bazoum kuachiliwa mara moja na bila masharti yoyote huku usalama wake ukitakiwa kuhakikishwa.

 Ameongeza kuwa watendaji wa Serikali yake waliozuiliwa kiholela pamoja na ndugu zao nao pia lazima waachiliwe mara moja, na bila masharti. 

“Ninawasihi wahusika wote kujiepusha na vurugu na kuheshimu haki na uhuru wa kimsingi wa wote. Ni kwa maslahi ya watu wote wa Niger kwamba mafanikio muhimu ya kidemokrasia yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni yabaki yanalindwa na kuhifadhiwa.” Ameeleza Turk katika taarifa yake 

Mkuu huyo wa haki za binadamu ameeleza kwa sasa nchi hiyo inahitaji kuchukua juhudi zote ili kuweza kurejesha utulivu wa kikatiba na utawala wa sheria nchini humo.