Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP imeshtushwa na kuuawa kwa mfanyakazi wake Yemen

Kitongoji cha Al Gahmalyya katika mji wa Taiz, Yemen, kimeharibiwa vibaya kutokana na mzozo wa miaka mingi.
© WFP/Mohammed Awadh
Kitongoji cha Al Gahmalyya katika mji wa Taiz, Yemen, kimeharibiwa vibaya kutokana na mzozo wa miaka mingi.

WFP imeshtushwa na kuuawa kwa mfanyakazi wake Yemen

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani  WFP limesema limeshitushwa na limesikitishwa sana kuthibitisha kwamba mfanyakazi wake mmoja amepigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana leo Ijumaa mchana huko Turbah, kusini magharibi mwa Yemen.

Moayad Hameidi, raia wa Jordan, alifariki dunia muda mfupi baada ya kupelekwa hospitalini.

Kwa mujibu wa shirika hilo Hameidi alikuwa amewasili hivi karibuni Yemen kuchukua nafasi yake mpya kama mkuu wa ofisi ya WFP huko Taiz. 

Limeongeza kuwa kama msaidizi aliyejitolea wa kibinadamu, Hameidi, alikuwa amefanya kazi na WFP kwa miaka 18, ikiwa ni pamoja na kazi ya awali huko Yemen pamoja na kutumikia kwa muda huko Sudan, Syria na Iraq.

Richard Ragan, mwakilishi wa WFP na Mkurugenzi wa shirika hilo nchi nchini Yemen amesema "Kupoteza mwenzetu ni janga kubwa kwa shirika letu na jumuiya ya kibinadamu. Hasara yoyote ya maisha katika huduma ya kibinadamu ni janga lisilokubalika."