Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC: Jela zina wafungwa wengi kinyume cha kanuni

Operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa zimekuwa msitari wa mbele kuzisaidia nchi katika masuala ya haki zikiwemo za mawafungwa
MINUSCA/Leonel Grothe
Operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa zimekuwa msitari wa mbele kuzisaidia nchi katika masuala ya haki zikiwemo za mawafungwa

UNODC: Jela zina wafungwa wengi kinyume cha kanuni

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2021 watu milioni 11.2 walifungwa gerezani ulimwenguni kote hii ni sawa na kwenye kila watu 100,000 kuna wastani wa wafungwa 142 imesema leo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya dawa na Uhalifu UNODC. 

Kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Mataifa za viwango vya kawaida vya kuwahudumia wafungwa katika jela “Kanuni za Mandela” nchi wanachama zinapaswa kuendelea kupunguza mlundikano wa wafungwa na pale inapowezekana adhabu zisizohusisha kuwashikilia zinapswa kuchukuliwa. 

UNODC inasema kanuni hii ilizingatiwa kwa kiasi kikubwa kipindi cha janga la COVID-19 na idadi ya wafungwa iliripotiwa kupungua ulimwenguni kote kwa zaidi ya 600,000 mwaka 2020, ikipungua kutoka wafungwa milioni 11.7 mwaka 2019.

Hata hivyo katika ripoti yao waliyoitoa leo huko Vienna, Austria wamesema tangu mwaka 2021 idadi ya wafungwa imeanza kuongezeka tena jambo linaloashiria kuwa mbinu zilizotumika kipindi cha janga la CORONA hazikuwa endelevu.

“Idadi ya magereza duniani inawakilisha zaidi ya mara mbili ya idadi ya watu wanaoishi katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati-CAR, Norway au Singapore na takribani idadi hiyo ni sawa na idadi ya watu wa Jamhuri ya Dominika na Jordan.” Imesema ripoti hiyo 

Utafiti huo uliojumuisha takriban nchi 150 umebaini kuwa watu wengi walio gerezani duniani kote ni wanaume ambao ni 94% lakini katika miongo miwili iliyopita idadi ya wanawake gerezani imeongezeka kwa kasi +35% kuliko wanaume ambao wameongezeka kwa +16%.

Kwa kuzingatia kuendelea kwa ukuaji wa idadi ya watu, Barani Amerika ya Kaskazini, Barani Afrika- Kusini mwa Jangwa la Sahara na Barani Ulaya Mashariki kumerekodiwa kupungua kwa muda mrefu kwa viwango vya kifungo, pamoja hadi 33% tangu mwaka 2000, wakati Mabara mingine, kama vile Amerika ya Kusini na Australia/New Zealand, kumeshuhudiwa kuongezdeka kwa idadi ya wafungwa katika miongo miwili iliyopita kiwango kikiwa ni juu ya 70%.

Kusoma ripoti hiyo bofya hapa