Griffiths akaribisha kuachiliwa wafungwa wa vita nchini Yemen

30 Septemba 2019

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Martin Griffiths, amekaribisha hatua ya kundi la Ansar Allah nchini humo ya kuwaachilia huru wafungwa.

Kuachiliwa kwa wafungwa hao ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya amani huko Stockholm nchini Sweden mwaka jana, mazungumzo yaliyoleta pande kinzani nchini Yemen.

 

Griffiths kupitia taarifa yake aliyoitoa leo mjini Amman, Jordan, ametoa wito wa pande zote zihakikishe kuwa wafungw hao walioachiliwa huru wanarejea  makwao salama.

Ameongeza kuwa ana matumaini kuwa hatua hii itachangia kuwepo mipango zaidi ya kubadilishana wafungwa wote wa mizozo kwa mujibu wa makubaliano ya Stockholm.

Halikadhalika amekaribisha hatua za awali zilizochukuliwa na serikali ya Yemen na ushirikiano wa nchi za kiarabu, ambazo ziliwezesha kuachiliwa kwa wafungwa watoto 42 na hatimaye kuunganishwa na familia zao.

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen ametoa wito kwa pande husika kushirikiana kufanikisha kuachiliwa na kuwasafirisha wafungwa wanaotokana na mizozo akiongeza kuwa wafungwa na familia zao wamepitia machungu makali na taabu.

Ametoa shukran zake kwa kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu, ICRC  kwa wajibu wao muhimu katika kufanikisha kuachiliwa huru kwa wafungwa hao kutoka kundi hilo la Ansar Allah ambalo ni la wahouthi.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter