Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la idadi ya wafungwa wanawake duniani ni kubwa - UNODC

Katika gereza la wanawake la Pétionville kwenye viunga vya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, watu kati ya 20 hadi 30 wanashikiliwa katika chumba kimoja na wanawake na wasichana wengine wenye umri wa hadi miaka 14 wanalala chini.
UN Photo/Victoria Hazou
Katika gereza la wanawake la Pétionville kwenye viunga vya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, watu kati ya 20 hadi 30 wanashikiliwa katika chumba kimoja na wanawake na wasichana wengine wenye umri wa hadi miaka 14 wanalala chini.

Ongezeko la idadi ya wafungwa wanawake duniani ni kubwa - UNODC

Haki za binadamu

Mtu mmoja kati ya watatu walioko jela anashikiliwa bila kufunguliwa mashtaka, hii ikimaanisha kwamba hawajapatikana na hatia katika mahakama yoyote ya haki.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa kwanza kabisa kuhusu hali ya wafungwa iliyoandaliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti madawa na uhalifu, UNODC kuelekea siku ya kimataifa ya Nelson Mandela tarehe 18 mwezi huu wa Julai.

Utafiti huo uliotolewa leo huko Vienna, Austria, umeangazia pia idadi ya wafungwa ukionesha kwamba katika miongo miwili iliyopita, 2000 hadi 2019, idadi ya wafungwa duniani kote iliongezeka kwa zaidi ya asilimia 25 ilhali kiwango cha ongezeko la idadi ya watu duniani kilikuwa asilimia 21 kipindi hicho hicho na watu milioni 11.7 wakiwa wamefungwa jela mwishoni mwa mwaka 2019.

“Idadi hiyo ya watu waliofungwa ni sawa na idadi ya watu katika nchi mathalani Burundi, Bolivia, Ubelgiji au Tunisia,” imesema ripoti hiyo.

Mwishoni mwa mwaka 2019, mwaka ambao ndio takwimu mpya zimepatikana, kulikuwepo na wafungwa 152 katika kila watu 100,000.

Idadi ya wanawake wanaofungwa imeongezeka kwa kasi kubwa ambapo ni asilimia 33 huku ongzeko la wanaume wafungwa ni asilimia 25 pekee- UNODC

Takwimu hizo zinaonesha wakati katika nchi za Amerika Kaskazini, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Ulaya MAshariki kumekuwepo na kupungua kwa idadi ya wafungwa kwa asilimia 27, kwa maeneo mengine kama Amerika ya Kusini, Australia na New Zealand, kipindi cha miongo miwili kimeshuhudia ongezeko la wafungwa kwa asilimia 68.

Kwa ujumla asilimia 93 ya wafungwa duniani kote ni wanaume lakini cha kustaajabisha katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, idadi ya wanawake wanaofungwa imeongezeka kwa kasi kubwa ambapo ni asilimia 33 huku ongzeko la wanaume wafungwa ni asilimia 25 pekee.

Mlundikano magerezani na COVID-19

Kwa kuwa UNODC ndio mlinzi na mhifadhi wa kanuni za uangalizi wa wafungwa zijulikanazo pia kama Kanuni za Nelson Mandela, imeangalia pia mlundikano kwenye magereza.

Viwango vya magereza kupindukia ni tofauti kwa kila eneo lakini katika nusu ya nchi zilizotafitiwa magereza yao yamejaa pomoni kwa zaidi ya asilimia 100.

“Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limesababisha kuelekeza msisitizo katika kujaa kupindukia kwa magereza. Kwa mujib wa vyanzo vya wazi na chambuzi za serikali, hadi mwezi Mei mwaka huu wa 2021, takribani wafungwa 550,000 katika nchi 122 waliambukizwa virusi vya Corona ambapo kati yao hao 4,000 walifariki dunia katika nchi 47.”

Katika kudhibiti mlundikano magerezani, baadhi ya nchi zilidhibiti shughuli za michezo miongoni mwa wafugwa, kazi na kutembelewa na wanafamilia.

Huku hatua za kudhibiti kusambaa kwa COVID-19 zikiwa ni vigumu kusimamia magerezani, hasa kwa yale yaliyojaa kupita kiasi, baadhi ya nchi ziliamua kuwaachilia wale waliokuwa wamewekwa korokoroni au rumande na wale waliokuwa wamefungwa kwa makosa ya kihalifu yasiyohusisha ghasia.

TAGS: UNODC, Wafungwa, COVID-19