Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya Plus yafanikisha maabara za hedhi salama nchini Tanzania

Bi. Suzan Yumbe, Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa Afya Plus akionesha taulo ya kike iliyotengenezwa na shirika lake kupitia mradi wa Maabara ya Hedhi salama uliofadhiliwa na Mfuko wa Malala kusongesha lengo namba 6 la malengo ya maendeleo endelevu, SDG …
UN/Assumpta Massoi
Bi. Suzan Yumbe, Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa Afya Plus akionesha taulo ya kike iliyotengenezwa na shirika lake kupitia mradi wa Maabara ya Hedhi salama uliofadhiliwa na Mfuko wa Malala kusongesha lengo namba 6 la malengo ya maendeleo endelevu, SDG kuhusu maji safi na kujisafi.

Afya Plus yafanikisha maabara za hedhi salama nchini Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania shirika la kiraia la Afya Plus kupitia ufadhili wa Mfuko wa Malala limefanikisha utekelezaji wa maabara za hedhi salama za kupatia wanafunzi taulo za kike au pedi za kufua, moja ya hatua za kufanikisha lengo namba 6 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kuhusu huduma za maji safi na kujisafi.

Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Suzan Yumbe akizungumza na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni huko Iringa nchini Tanzania amesema mradi maabara za hedhi salama pamoja na kuzalisha pedi za kufua zinazodumu kwa miaka miwili, unatoa elimu kuhusu hedhi salama na afya ya uzazi kwa kutumia mtaala walioandaa kwa Pamoja na muunguzi wa mkoa na viongozi wengine wa afya na elimu mkoani humo.

Afya Plus inasongesha SDG namba 6

Afya Plus inasongesha harakati hizo wakati huu ambapo jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, SDGs linaendelea katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani huku moja ya malengo yanayomulikwa ni lengo namba 6 kuhusu maji safi na salama pamoja na huduma za kujisafi. 

Wawakilishi kutoka serikali, mashirika ya kimataifa na yale yasiyo ya kiserikali wanatathmini utekelezaji wa lengo hilo kwa kuzingatia kuwa janga la COVID-19 lilipeleka mrama mafanikio yaliyokwishakupatikana. Licha ya changamoto hizo zitokanazo na COVID-19 mashirika yasiyo ya kiserikali yanatumia mbinu bunifu kufanikisha lengo hilo hasa hedhi salama kwa wasichana na wanawake. 

Shule zimepatiwa mashine, elimu na malighafi kutengeneza taulo za kike

Afya Plus kwa kutambua changamoto za watoto wa kike na wanawake hususan maeneo ya vijijni kupata taulo za kike au pedi kwa ajili ya kujisafi inatumia mradi huo wa maabara za hedhi za salama kuondoa changamoto hiyo.

“Katika hizo maabara tumepeleka mashine, malighafi na elimu ya jinsi gani wanaweza kutengeneza pedi. Kwa hiyo wasichana, wavulana na walimu wameweza kupewa hiyo elimu. Na hadi sasa hivi wanatengeneza pedi katika ngazi ya shule na hizo taulo za kike zinatolewa bure kwa wanafunzi,” amesema Bi. Yumbe.

Mkuu huyu wa shirika la Afya Plus anasema wanashirikiana pia na serikali na viongozi wa elimu kuhakikisha kuwa pindi mradi unapomalizika muda wake, wao wanaochukua na kuweza kuhakikisha wanafunzi wanaweza kupata malighafi na pia wanaendelea na uzalishaji wa taulo za kike au pedi kwa sababu mashine tumeshawapatia, halikadhalika elimu.

Afya Plus huendesha kwa pamoja mradi huo na shule kwa miaka mitatu na kisha huachia shule kuendelea nao. Malighafi zinazotumika ni pamba.

Taulo hizi za kike zinalinda pia mazingira

Pamoja na taulo hizo za kike kutumia malighafi inayozuia muwasho kwa mtumiaji kwa sababu hazitumii malighafi ya nailoni, Bi. Yumbe amesema wamezingatia pia mazingira.

“Malighafi tuliyotumia ni rafiki kwa mazingira kwani baada ya pedí hii kutumika kwa miaka miwili inaweza kuteketezwa kirahisi na haikai kwenye udongo kwa muda mrefu,” amesema Bi. Yumbe.