Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunataka nyaraka ya mwisho iwe na sauti zetu sote - SASAL

Mana Omar, Afisa Mtendaji Mkuu na Muasisi wa shirika la kiraia la SASAL lililoko Kajiado nchini Kenya.
UN News/Assumpta Massoi
Mana Omar, Afisa Mtendaji Mkuu na Muasisi wa shirika la kiraia la SASAL lililoko Kajiado nchini Kenya.

Tunataka nyaraka ya mwisho iwe na sauti zetu sote - SASAL

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maji ukiwa umeingia siku ya pili hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani lengo likiwa ni kufanya mapitio ya kina ya Muongo wa hatua kwa maji na huduma za kujisafi mwaka 2018 hadi 2028 mmoja wa washiriki amezungumzia kadhia wanayopata huko atokako kutokana na uhaba wa maji.

Mana Omar ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu na Muasisi wa shirika la kiraia la SASAL lililoko Kaunti ya Kajiado nchini Kenya amesema “kule kwetu wasichana na wanawake wanatembea kilometa 8 kwenda na kurudi kila siku Kwenda kuteka maji mtoni na maji yenyewe na mtoni si masafi.”

Tweet URL

Wanawake hutembea kilometa 8 kila siku kutafuta maji

Bi. Omar anasema hiyo sio tu inawaweka hatarini kupata magonjwa, bali pia wanapokuwa kwenye misafara ya Kwenda kuteka maji wanakumbwa na majanga kama vile ubakaji au kujaribiwa kubakwa, hukimbizwa na wanaporejea nyumbani wanapigwa na waume zao kwa sababu wamechelewa na waume zao hawajui kuwa huyo mwanamke alikimbizwa na akapoteza muda na kushindwa kurejea kwa wakati.”

Sisi ni jamii ya wafugaji sasa mifugo pia inakufa

Kwa mujibu wa Mkuu huyu wa shirika la SASAL, wao pia ni jamii ya wafugaji katika eneo lao ambalo ni kame wakifuga mbuzi na ng’ombe.

“Inakuwa vigumu sana hawa mbuzi na ng’ombe na kuishi kwa sababu ya ukosefu wa maji. Na kama mvua hainyeshi, ina maana hakuna nyasi. Huwezi kupanda nyasi kama wewe mwenyewe hauna maji ya kunywa, na wala huwezi kupanda miti. Hivyo eneo linazidi kuwa kame,” amefafanua Bi. Omar.

Ukame unaathiri elimu kwa watoto

Shida zingine zinakuja kwa sababu watoto wanakosa kwenda shuleni kwa sababu hakuna maji, wanasaidia wazazi wao kwenda kuchunga mbuzi, kutafuta maji na kuni.

Matarajio yake ni nini?

SASAL inatarajia kuwa katika mkutano huu itapata fursa ya kuzungumzia changamoto za jamii yake ili kila mtu awe na uwakilishi na hatimaye nyaraka ya mwisho ya mkutano huo iitwayo Ajenda ya Hatua kwa Maji iwe na sauti na majawabu kutoka kwa kila mtu.

Ajenda ya Hatua kwa Maji

Nyaraka hiyo ya mwisho ya mkutano huu itaweka pamoja ahadi zote kutoka nchi wanachama na wadau wengine kwa lengo la kuleta mabadiliko makubwa yenye majawabu ili hatimaye kusongesha na kutekeleza lengo namba 6 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama.

Ingawa tayari ahadi mbalimbali zimeshatolewa na zinapatikana mtandaoni, matangazo ya kimsingi ya kujumuisha kwenye nyaraka hiyo yatatolewa wakati wa mkutano.

Mkutano huu umeandaliwa kwa pamoja na Uholanzi na Tajikistan na mara ya mwisho mkutano kama huu ulifanyika mwaka 1977.