Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mambo 5 unayopaswa kujua kuhusu mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Maji wa 2023

Msichana akichota maji katika kisima cha pumpu kilichokarabatiwa hivi karibuni Gwembe Valley, Zambia
© UNICEF/Karin Schermbrucker
Msichana akichota maji katika kisima cha pumpu kilichokarabatiwa hivi karibuni Gwembe Valley, Zambia

Mambo 5 unayopaswa kujua kuhusu mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Maji wa 2023

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa maji wa 2023, ambao utafanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuanzia tarehe 22-24 Machi, unasifiwa kama fursa ya kipekee ya kizazi hiki ya kuharakisha maendeleo kuelekea upatikanaji wa maji salama na usafi wa mazingira ifikapo mwaka 2030.

Maji ndio msingi wa maendeleo endelevu. Yanasaidia nyanja zote za maisha duniani, na upatikanaji wa maji salama na safi ni haki ya msingi ya binadamu. Hata hivyo, miongo mingi ya usimamizi mbaya na matumizi mabaya imeongeza shinikizo la maji, na kutishia nyanja nyingi za maisha zinazotegemea rasilimali hii muhimu.

Maji safi ni muhimu kwa afya ya binadamu
© UNICEF
Maji safi ni muhimu kwa afya ya binadamu

1. Tunakabiliwa na tatizo la maji duniani

Maji ni muhimu kwa ustawi wa binadamu, uzalishaji wa nishati na chakula, mifumo ya ikolojia yenye afya, usawa wa kijinsia, kupunguza umaskini na mengineyo.

Lakini kwa sasa tunakabiliwa na tatizo la maji duniani. Mabilioni ya watu duniani kote bado wanakosa huduma ya maji.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 800,000 hufa kila mwaka kutokana na magonjwa yanayochangiwa moja kwa moja na maji yasiyo salama, ukosefu wa usafi wa mazingira na kanuni duni za usafi.

Mahitaji ya rasilimali hii ya thamani yanaendelea kuongezeka, takriban watu bilioni nne wanapata uhaba mkubwa wa maji kwa angalau mwezi mmoja kwa mwaka. Kwa kuwa maji ni muhimu sana kwa nyanja nyingi za maisha, ni muhimu kuhakikisha ulinzi wake na usimamizi mzuri ili kuhakikisha kuwa kila mtu ana fursa sawa ya kupata rasilimali hii muhimu ifikapo mwisho wa mwaka 2030.

Ukame unaathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji kwa jamii zisizojiweza
WMO/Edward-Ryu
Ukame unaathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji kwa jamii zisizojiweza

2. Maji na hali ya hewa ni lila na fila havitengamani

Kutokana na kuongezeka kwa mafuriko, kunyesha kwa mvua isiyotabirika, na ukame, athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye maji zinaweza kuonekana na kuhisiwa kwa kasi.

Athari hizi zinatishia maendeleo endelevu, bioanuwai, na upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira kwa watu.

Kulingana na ripoti ya hivi karibuni zaidi ya “Hali ya mabadiliko ya tabianchi katika huduma za maji “ya shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani (WMO), hatari zinazohusiana na maji zimeongezeka kwa kasi ya kutisha.

Tangu mwaka wa 2000, mafuriko yameongezeka kwa asilimia 134 huku muda wa ukame ukiongezeka kwa asilimia 29.

Lakini maji pia yanaweza kuwa suluhisho muhimu kwa mabadiliko ya tabianchi. Hifadhi ya hewa ukaa inaweza kuboreshwa kwa kulinda mazingira kama vile nyasi na ardhi oevu, kufuata kanuni za kilimo endelevu kunaweza kusaidia kupunguza shinikizo kwenye usambazaji wa maji safi, na kuboresha miundombinu ya maji na usafi wa mazingira kunaweza kuhakikisha kuwa kila mtu anapata rasilimali muhimu katika siku zijazo.

Maji lazima yawe katikati ya sera na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Usimamizi endelevu wa maji unaweza kusaidia kujenga mnepo, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na kulinda jamii na mifumo ya ikolojia. Suluhu za maji endelevu, za gharama nafuu, na zisizo hatarishi lazima ziwe kipaumbele.

Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa 2023
United Nations
Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa 2023

3. Miongo minne, ahadi mpya za ujasiri ziko mezani

Mkutano wa maji wa Umoja wa Mataifa wa 2023 utakuwa wakati muhimu wa kuamua kwa pamoja juu ya "kuchukua hatua na kushughulikia changamoto pana zinazozunguka suala la maji," kwa maneno ya Li Junhua, msaidizi waKatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kiuchumi na kijamii (DESA) na ambaye pia atakuwa katibu mkuu wa mkutano huo.

Mkutano huo utawaleta wakuu wa nchi na serikali, mawaziri, na washikadau katika sekta zote tofauti pamoja ili kufikia malengo yaliyokubaliwa kimataifa, likiwemo lengo la 6 la maendeleo endelevu la ajenda ya 2030 ya Umoja wa Mataifa kwa mustakabali wa haki, kuhakikisha upatikanaji wa maji salama, usafi wa mazingira na usafi kwa wote.

Moja ya matokeo makuu ya mkutano huo itakuwa ni agenda ya hatua za utekelezaji wa maji ambayo itachukua ahadi zote za hiari zinazohusiana na maji na kufuata maendeleo yake.

Ajenda inalenga kuhimiza nchi wanachama, wadau, na sekta binafsi kujitolea kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto za sasa za maji.

Mwanamke mjini Port-au-Prince, Haiti,akiwa amebeba maji aliyonunua kutoka kwa mjasiriamaliwa maji
© UNICEF/Odlyn Joseph
Mwanamke mjini Port-au-Prince, Haiti,akiwa amebeba maji aliyonunua kutoka kwa mjasiriamaliwa maji

4. Kuzingatia maeneo matano muhimu

Mkutano huo utakuwa na midahalo shirikishi mitano ili kuimarisha na kuharakisha hatua katika maeneo muhimu ya maji.

Mijadala shirikishi pia inaunga mkono kanuni tano za mkakati wa kimataifa wa kusongesha lengo la SDG 6, mpango wa kutoa matokeo ya haraka ili kuhakikisha upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na usafi wa mazingira kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Mijadala hiyo mitano inayoingiliana ni:

1. Maji kwa ajili ya Afya: Upatikanaji wa maji safi ya kunywa, usafi na usafi wa mazingira.

2. Maji kwa Maendeleo Endelevu: Kuthamini Maji, mkakati wa maji-nishati-chakula na maendeleo endelevu ya kiuchumi na miji.

3. Maji kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi, mnepo na mazingira: Chanzo cha Bahari, bayoanuwai, hali ya Hewa, mnepo na kupunguza hatari za maafa.

4. Maji kwa ushirikiano: Ushirikiano wa Maji wa kuvuka mipaka na kimataifa, ushirikiano mtambuka wa kisekta na maji katika Ajenda ya 2030.

5. Muongo wa hatua za maji: Kuharakisha utekelezaji wa malengo ya muongo, ikiwa ni pamoja na kupitia mpango kazi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

5. Unawezaje kushiriki?

Maji ni suala muhimu ambalo linaathiri kila mtu. Wakati Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa, serikali na washikadau wakijiandaa kufanya ahadi zao za maji, Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa kila mtu kuchukua hatua yake binafsi. Kitendo chochote - kiwe kidogo au kikubwa - kinaweza kusaidia kuharakisha mabadiliko na hatua kuelekea kufikia malengo na malengo ya SDG 6.

Hapa kuna baadhi ya vitendo rahisi ambavyo vinaweza kujumuishwa katika shughuli za kila siku:

• Oga kwa muda mfupi na upunguze upotevu wa maji nyumbani kwako. Kwa asilimia 44 ya maji machafu ya kaya hayatibiwi kwa usalama, kuoga kwa muda mfupi ni njia nzuri ya kuokoa rasilimali hii ya thamani. Mwongozo wa Mtu Mvivu wa Kuhifadhi Maji

• Shiriki katika usafishaji wa mito, maziwa au ardhi oevu. Panda mti au unda bustani yako ya maji. Hatua hizi zinaweza kusaidia kulinda mifumo ikolojia ya maji dhidi ya uchafuzi wa mazingira na kupunguza hatari ya mafuriko na kuhifadhi maji kwa ufanisi.

• Kuongeza ufahamu juu ya uhusiano muhimu kati ya vyoo, usafi wa mazingira, na hedhi. Vunja miiko kwa kuanzisha mazungumzo katika jumuiya ya eneo lako, shuleni au mahali pa kazi.

Pata maelezo zaidi kuhusu malengo na shabaha za SDG 6 na uendelee kutetea masuluhisho katika ngazi ya ndani na kitaifa. Saidia kampeni zinazohusiana na maji na ujue njia zingine unazoweza kujumuisha vitendo rahisi ambavyo vinaweza kusaidia kulinda rasilimali za maji.

Wapiga mbizi wakisaidia katika usafi wa bahari Disney Australia
UN World Oceans Day/Rosie Leaney
Wapiga mbizi wakisaidia katika usafi wa bahari Disney Australia

5. Unawezaje kushiriki?

Maji ni suala mtambuka na muhimu ambalo linaathiri kila mtu. Wakati nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, serikali na wadau wakijiandaa kufanya ahadi zao za maji, Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa kila mtu kuchukua hatua yake binafsi.

Kitendo chochote kiwe kidogo au kikubwa  kinaweza kusaidia kuharakisha mabadiliko na hatua kuelekea kufikia malengo ya maendeleo ikiwemo lengo la SDG 6.

Hapa kuna baadhi ya vitendo rahisi ambavyo vinaweza kujumuishwa katika shughuli za kila siku:

• Oga kwa muda mfupi na upunguze upotevu wa maji nyumbani kwako. Kwa sababu asilimia 44 ya maji machafu ya kaya hayasafishwi kwa usalama, kuoga kwa muda mfupi ni njia nzuri ya kuokoa rasilimali hii ya thamani. Mwongozo wa mtu mvivu wa kuhifadhi maji

• Shiriki katika usafishaji wa mito, maziwa au ardhi oevu. Panda mti au unda bustani yako ya maji. Hatua hizi zinaweza kusaidia kulinda mifumo ya ikolojia ya maji dhidi ya uchafuzi wa mazingira na kupunguza hatari ya mafuriko na kuhifadhi maji kwa ufanisi.

• Kuongeza ufahamu juu ya uhusiano muhimu kati ya vyoo, usafi wa mazingira, na hedhi. Vunja miiko kwa kuanzisha mazungumzo katika jumuiya ya eneo lako, shuleni au mahali pa kazi.

Pata maelezo zaidi kuhusu malengo na shabaha za SDG 6 na uendelee kutetea suluhisho katika ngazi ya mashinani na kitaifa.

Saidia kampeni zinazohusiana na maji na ujue njia zingine unazoweza kujumuisha vitendo rahisi ambavyo vinaweza kusaidia kulinda rasilimali za maji.