Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo langu ni kupata jawabu la teknolojia ya kusafisha maji eneo letu

Naibu Meya wa Wilaya ya Musanze katika jimbo la Musanze nchini Rwanda akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya UN kando mwa mkutano wa Maji, jijini New York.
UN Video
Naibu Meya wa Wilaya ya Musanze katika jimbo la Musanze nchini Rwanda akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya UN kando mwa mkutano wa Maji, jijini New York.

Lengo langu ni kupata jawabu la teknolojia ya kusafisha maji eneo letu

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maji ukiingia siku ya tatu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huku moja ya mikakati ni kuhakikisha kunakuweko matumizi endelevu ya maji, mmoja wa washiriki kutoka Rwanda amezungumzia vile ambavyo teknolojia ya kusafisha maji taka ili yaweze kutumika tena na tena inaweza kuwa mkombozi kwenye eneo lao.

Mshiriki huyo Andrew Mpuhwe Rucyahana ambaye ni Naibu Meya wa wilaya ya Musanze katika jimbo la Kaskazini nchini Rwanda amesema hayo akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Bwana Rucyahana anasema kule Musanze anakotoka ni eneo lenye shughuli nyingi za kitalii na likipokea wageni wengi wanaofika hivyo ni lazima kuwe na kiasi kikubwa cha maji tena maji safi.

Ushiriki wangu kwenye huu mkutano utaniwezesha kukutana na watu wengine na kufahamu ni vipi tunaweza kufanikisha wilaya ya Musanze iwe na maji safi na salama hasa kwa kuzingatia eneo letu liko milimani na tunapokea watalii wengi,” amesema Naibu Meya huyu wa Musanze.

Hapa kwenye mkutano tunaweza kubadilishana mawazo ni vipi watu wanajenga miundombinu ya maji.

Tweet URL

Maji  yako Musanze lakini hayatoshi

Tuna maji mengi lakini hayatoshi, tungali na kazi kubwa ya kufanya ili tufikishe maji safi kwa watu wote, anasema Bwana Rucyahana akitaja changamoto ni uhaba wa fedha za kuwezesha kujenga miundombinu ya kufikisha maji milimani.

“Tunahitaij kupata maji yaliyo safi. Mfano tupate teknolojia ya kupeleka maji milimani ambako kuna hoteli zinazopokea wageni wengi. Tuna malengo ya kufikisha maji kwa wakazi wote wa wilaya ya Musanze ifikapo mwaka 2024.”

Tunataka teknolojia ya kusafisha maji ili yatumike tena na tena

Hoja ya kutumia maji tena na tena ilitajwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi, ambaye alisema teknolojia hiyo ni moja ya mambo muhimu ya kuepusha kupoteza maji.

“Tunatakiwa kukomesha haraka upotevu wa maji. Kuwa na mzungumko wa matumizi ya maji, yaani kuyatumia tena na tena badala ya kuchimba mengine, huo ndio unapaswa kuwa mwelekeo,” 

Naibu Meya huyu wa Musanze anasema katika eneo lao watu wanatumia maji mara moja tu “unaona maji mengi yanaharibika. Lakini tayari kuna teknolojia ya kusafisha maji ili yatumike tena na tena mara mbili au tatu. Teknolojia hii ni gharama kubwa Afrika. Kwa Musanze teknolojia hiyo inatumika kwenye hotel za gharama ya juu . Lakini si katika hoteli za bei ya gharama ya chini au kwenye makazi ya watu wenye uwezo mdogo ambao ni wengi.”

Sasa tunatafuta wafadhili

Ni kwa mantiki hiyo anaamini kuwa kupitia mkutano wa maji anaweza kupata watu wenye teknolojia wanaweza kuipeleka na kuiuza huko Musanze.

Lakini juu ya yote wito wake ni kwa watu kutambua kuwa maji ni maisha yetu, kukosa maji ni kukosa maisha. Watu wote tusaidiane ili tuwe na maji safi na mengi barani Afrika.