Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inapuuza kwa makusudi vifo vya watoto wakati wa safari hatari Bahari ya Mediterania: UNICEF

Lampedusa, kisiwa kidogo kusini mwa Italia, ni sehemu ya kwanza ya kutua kwa watu wengi wanaovuka Bahari ya Kati.
© UNICEF
Lampedusa, kisiwa kidogo kusini mwa Italia, ni sehemu ya kwanza ya kutua kwa watu wengi wanaovuka Bahari ya Kati.

Dunia inapuuza kwa makusudi vifo vya watoto wakati wa safari hatari Bahari ya Mediterania: UNICEF

Wahamiaji na Wakimbizi

Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, wavulana na wasichana 289 wamekufa walipokuwa wakivuka bahari ya Mediterania kufika Ulaya, idadi hiyo ikiwa ni mara mbili ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022, limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

“Idadi hiyo ni sawa na watoto wapatao 11 wanaokufa kila wiki, ni kubwa zaidi ya kile tunachosikia kwenye vichwa vya habari," amesema Vera Knaus, kiongozi wa shirika la Global Lead on Migration and Displacement, alipozungumza na waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa masuala ya kibinadamu wa kila wiki wa Umoja wa Mataifa huko Geneva Uswisi.

Ameongeza kuwa "Hatuwezi kuendelea kupuuza kile kinachotokea, kukaa kimya wakati karibu watoto 300 ndege nzima iliyojaa watoto wanakufa majini kati ya Ulaya na Afrika katika muda wa miezi sita".

Vifo vinavyoweza kuzuilika

UNICEF inasema migogoro na mabadiliko ya tabianchi  vinalazimisha kuongezeka kwa idadi ya watoto kuanza safari hatari ya baharini kutoka Afrika Kaskazini hadi Ulaya.

UNICEF inakadiria kuwa watoto 11,600 wamevuka katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu ikiwa ni karibu mara mbili ya kipindi kama hicho mwaka 2022.

Hata hivyo, shirika hilo limeonya kwamba idadi halisi ya watoto waliopoteza maisha huenda ikawa kubwa zaidi kwani ajali nyingi za meli katika Bahari ya Mediterrania haziachi manusura au kurekodiwa.

Bi. Knaus amesema inaonekana ulimwengu "unapuuza kwa makusudi kile kinachotokea kwa kuzingatia idadi na ukimya unaozunguka vifo hivi vinavyoweza kuzuilika.”

Kuzama kwa dunia kutochukua hatua

“Watoto wanakufa si tu mbele ya macho yetu, wanakufa huku sisi tunaonekana kufumba macho. Mamia ya wasichana na wavulana wanazama katika kupuuza kwa dunia,” amesema, akibainisha kuwa Bahari ya Mediatterania ni miongoni mwa njia mbaya zaidi za uhamiaji kwa watoto.

UNICEF inakadiria kuwa watoto wengi wanavuka bila wazazi au walezi wao, huku wasichana wakisafiri peke yao hasa katika hatari ya kukabiliwa na ukatili wa kingono katika safari nzima.

Katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu watoto 3,300 wasio na wasindikizaji au waliotenganishwa na wazazi au walezi waliwasili Ulaya kupitia njia ya Bahari ya Mediterania ya Kati, au zaidi ya asilimia 70 ya jumla ya watoto wote.

Kuimarisha ulinzi wa mtoto

Katika kukabiliana na mzozo unaoongezeka, UNICEF inazisaidia nchi katika kuimarisha ulinzi wa watoto, ulinzi wa kijamii na mifumo ya uhamiaji na hifadhi. Wafanyikazi pia wanafanya kazi na serikali kutoa usaidizi na huduma zinazojumuisha watoto wote, bila kujali hali zao za kisheria, au za wazazi wao.

"Vifo hivi vinaweza kuzuilika," amesema Bi Knaus na kuongeza kuwa  "Wanasukumwa sana na dharura za hali ngumu, migogoro na hatari ya mabadiliko ya tabianchi ambayo huwaflazimisha watoto kukimbia majumbani wako kama vile ukosefu wa hatua za kisiasa na za vitendo kufanya kile kinachohitajika kuwezesha ufikiaji salama wa hifadhi na kulinda haki na maisha ya watoto popote wanakotoka na namna ya usafiri wao.”

Okoa maisha baharini

UNICEF imesisitiza kuwa wakati huo huo, nchi katika kanda, na Muungano wa Ulaya (EU), lazima zifanye jitihada zaidi kulinda watoto wanaoishi katika mazingira magumu baharini lakini pia katika nchi za asili, za usafiri na marudio,.

Pia linasisitiza haja ya njia salama, za kisheria na zinazoweza kufikiwa kwa watoto kutafuta ulinzi na kuungana na familia zao, kupitia kupanua wigo wa fursa ya kuunganishwa tena kwa familia, kuwapatia wakimbizi makazi mapya au visa na msaada mwingine wa kibinadamu.

Zaidi ya hayo, shirika hilo limesema nchi lazima ziimarishe uratibu wa shughuli za utafutaji na uokoaji baharini na kuhakikisha zinashuka mara moja hadi maeneo salama.

Bi. Knaus alisema jukumu la mashua za kuokoa katika dhiki ni kanuni ya msingi katika sheria za kimataifa za baharini, na kuwarejesha watu nyuma baharini au katika mipaka ya nchi kavu ni ukiukaji wa sheria za kitaifa, za EU na za kimataifa.