Wavukao Mediteranea wapungua lakini vifo vyaongezeka- UNHCR
Wavukao Mediteranea wapungua lakini vifo vyaongezeka- UNHCR
Ingawa idadi ya wakimbizi na wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediteranea kwenda Ulaya imepungua, idadi ya wanaokufa imeongezeka, kwa kuwa safari ni za hatari zaidi, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo amesema, “idadi ya wanaovuka ni ndogo kuliko mwaka 2015, mwaka ambao ulishuhudia idadi kubwa zaidi, lakini wanaokufa ni wengi.”
Mwaka 2021 ilikuwa 123,000 ikilinganishwa na 141,500 mwaka 2018.
Wanaokufa Mediteranea ni wengi
Mwaka jana wa 2021, takribani watu 3,231 waliripotiwa kufa au kupotea baharini ilhali mwaka 2018 idadi ilikuwa 2,277.
Bi. Mantoo anasema pengine wengine wengi walikufa au kupotea katika jangwa la Sahara na maeneo mengine ya mipakani.
Kwa mujibu wa UNHCR idadi kubwa wanakimbia mizozo, mateso na ghasia katika nchi zao.
Ripoti ya UNHCR ambamo taarifa hizo zimepatikana ilijikita katika njia kutoka Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika kuelekea Mediteranea ya Kati.
UNHCR yahofia pia ukatili kwa wakimbizi
Kando mwa ongezeko la vifo baharini, UNHCR ina wasiwasi kuwa vifo na ukatili vimeshamiri njiani iwe kuanzia katika nchi watokazo wahamiaji na wakimbizi hao na katika vituo vya mpito ikiwemo Eritrea, Somalia, Djibouti, Ethiopia, Sudan, na Libya – ambako ndiko kumeripotiwa matukio mengi zaidi.
“Wakiwa safarini, wakimbizi na wahamiaji hawana la kuchagua zaidi ya kutegemea wasafirishaji haramu ili waweze kuvuka jangwa la Sahara, hali ambayo inawatumbukiza kwenye hatari ya kufanyiwa ukatili,” amesema Bi. Mantoo.
Amesema kutoka Libya na Tunisia, idadi kubwa hujaribu kuvuka bahari ya Mediteranea kuelekea Italia au Malta.
“Katika matukio mengi, wale wanaofanikiwa kuvuka jangwa la Sahari na kujaribu kuvuka bahari, hutelekezwa na wale wanaowasafirisha kiharamu, ilhali baadhi ya wanaoondoka kupitia Libya wanakamatwa na kurejeshwa Libya ambako huswekwa korokoroni,” amefafanua Bi. Mantoo.
Wito wa UNHCR
UNHCR inatoa wito kwa hatua zaidi za kuzuia vifo vya wakimbizi na wasaka hifadhi na kutaka ulinzi zaidi kwa kuzingatia mwongozo wake wa mwezi Aprili wa ulinzi na majawabu sambamba na fedha za kusaidia operesheni zake.
Ombi hilo linataka usaidizi zaid iwa kibinadamu na linahusisha nchi 25 katika maeneo matatu tofauti yanayounganishwa na njia za ardhini na baharini zinazotumiwa na wasaka hifadhi na wakimbizi.