Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 50,000 wamepoteza maisha kote duniani wakihaha kuhama: IOM

Kuanzia Januari hadi Oktoba 2022, zaidi ya wahamiaji 200,000 walivuka Pengo la Darien kuendelea na safari zao.
© UNICEF/Eduard Serra
Kuanzia Januari hadi Oktoba 2022, zaidi ya wahamiaji 200,000 walivuka Pengo la Darien kuendelea na safari zao.

Watu 50,000 wamepoteza maisha kote duniani wakihaha kuhama: IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watu 50,000 duniani kote wamepoteza maisha wakati wa safari zao za uhamiaji tangu shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM lianze kuweka kumbukumbu ya wahamiaji waliopotea, kupoteza maisha  au wasiojulikana waliko mwaka 2014. 

Takwimu hizi ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya IOM iliyochapishwa leo  ambayo inasema licha ya kuongezeka kwa hasara ya watu kupoteza maisha, hatua chache zimechukuliwa na serikali katika nchi za asili wanakotoka watu hao, katika nchi wanakokupita, na wanakokwenda za kushughulikia changamoto ya kimataifa ya wahamiaji waliopotea. 

Kwa mujibu wa Julia Black mwandishi mwenza wa ripoti hii "Ingawa maelfu ya vifo vimerekodiwa katika njia za wahamiaji kila mwaka, ni hatua kidogo sana ambazo zimefanywa kushughulikia matokeo ya majanga haya, achilia mbali kuwazuia,"  

"Bila kujali sababu zinazowalazimisha au kuwasukuma watu kuhama, hakuna anayestahili kufa akitafuta maisha bora." Ameongeza 

Zaidi ya watu 30,000 waliopotea hawajulikani uraia wao 

Ripoti hiyo ya IOM inasema zaidi ya watu 30,000 katika rekodi za mradi huo wa wahamiaji waliopotea ni wa uraia usiojulikana, ikionyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wale wanaofariki dunia kwenye safari za wahamiaji bado hawajatambuliwa na kuacha maelfu ya familia zikitafuta majibu kuhusu wapendwa wao. 

“Muda unayoyoma na hakuna majibu yoyote tunayopewa” mmoja wa wahamiaji kutoka Motrocco ameliambia shirika la IOM mwaka 2021 wakati akimtafuta kaka yake ambaye alitoweka miaka 20 iliyopita akiwa safarini kuelekera Ulaya. 

Kwa wahamiaji ambao uraia wao uliweza kubainika IOM inasema zaidi ya 9000 walitoka Afrika, zaidi ya 6500 wametoka Asia na wengine 3000 wametoka katika nchi za Amerika. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo nchi tatu zinazoshika  nafasi ya juu kuwa asili ya walikotoka wahamiaji Afghanistan, Syria na Myanmar zinakabiliwa na vurugu, na watu wengi wanakimbia makazi yao kutafuta hifadhi nje ya nchi. 

Zaidi ya nusu ya vifo 50,000 vya watu vilivyoorodheshwa vilitokea kwenye njia za kuelekea na ndani ya bara Ulaya, huku njia za Bahari ya Mediterania zikigharimu maisha ya watu 25,104. 

UNHCR na IOM waonya kuhusu kuendelea kuongezeka kwa vifo vya wakimbizi na wahamiaji kwenye bahari ya Meditteranea
© UNHCR/Markel Redondo
UNHCR na IOM waonya kuhusu kuendelea kuongezeka kwa vifo vya wakimbizi na wahamiaji kwenye bahari ya Meditteranea

NJia ya kuingia Ulaya inaongoza kwa vifo 

Ripoti inasema njia za kuelekea Ulaya zinaongoza kwa idadi kubwa zaidi ya jumla na idadi ya watu ambao wamepotea na kudhaniwa kuwa wamekufa huku takriban watu 16,032 wakiripotiwa kupotea baharini ambao mabaki yao hayakupatikana kabisa. 

Afrika ni eneo la pili kwa idadi ya vifo vya watu wanaohama, huku zaidi ya vifo 9,000 vya wakati wa uhamiaji vikiwa vimerekodiwa barani humo tangu 2014. Tafiti za kikanda za kaya zinaonyesha kuwa takwimu hizi hakika ni ndogo sana ikilinganishwa na hali halisi. 

Karibu vifo 7,000 vimerekodiwa katika nchi za Amerika, vingi kwenye njia za kwenda Marekani ambavyo ni vifo 4,694.  

Kivuko cha mpaka wa Marekani na Mexico pekee ni kitovu cha vifo vya zaidi ya 4,000 tangu mwaka 2014. 

Vifo vingine 6,200 vimerekodiwa kote barani Asia na IOM inasema watoto ni zaidi ya asilimia 11 ya maisha yaliyopotea kwenye njia za wahamiaji barani Asia, idadi kubwa zaidi kuliko eneo lingine lolote.  

Kati ya vifo 717 vya watoto vilivyorekodiwa wakati wa uhamiaji katika eneo hilo, zaidi ya nusu yani vifo 436 ni wakimbizi wa Rohingya. 

Huko Asia Magharibi, takriban maisha 1,315 ya watu yamepotea kwenye njia za wahamiaji, vingi kati yao vikitokea katika nchi zenye migogoro inayoendelea ambayo hufanya kumbukumbu za wahamiaji waliopotea kuwa na changamoto kubwa.  

Takriban watu 522 wanaowasili kutoka Pembe ya Afrika wamekufa nchini Yemen, mara nyingi kutokana na ghasia, na vifo vya Wasyria 264 vimerekodiwa wakati wa majaribio ya kuvuka mpaka kwenda Türkiye. 

IOM imesema “Tunasisitiza kwamba wajibu chini ya sheria ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, ni lazima kuzingatiwa wakati wote. Tunahitaji kufanya kazi pamoja ili kuzuia na kupunguza vifo zaidi kwa kutanguliza shughuli za utafutaji na uokoaji, kuboresha na kupanua njia za kawaida na salama za uhamiaji, na kuhakikisha kwamba utawala wa uhamiaji unatanguliza ulinzi na usalama wa watu wanaohama.”