Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa hatua muafaka tunaweza kutokomeza ukimwi ifikapo mwaka 2030: UNAIDS

Phiona anafanya kazi katika kituo cha afya nchini Uganda kama mwanaharaki wa rika ya akina mama, anasaidia kutoa mafunzo na kusaidia akina mama kujifungua watoto wasio na VVU.
© UNICEF/Karin Schermbrucker
Phiona anafanya kazi katika kituo cha afya nchini Uganda kama mwanaharaki wa rika ya akina mama, anasaidia kutoa mafunzo na kusaidia akina mama kujifungua watoto wasio na VVU.

Kwa hatua muafaka tunaweza kutokomeza ukimwi ifikapo mwaka 2030: UNAIDS

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya ukimwi UNAIDS inasema kuna njia iliyo bayana ya kutokomeza janga hilo ifikapo mwaka 2030 na njia hiyo inaweza kusaidia kujiandaa na majanga mengine makubwa yasiyo tazamiwa na hivyo kuwezesha ufikiaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kwa mujibu wa ripopti hiyo ya kimataifa iitwayo “njia ya kumaliza ukimwi” ina takwimu na tafiti zinazoonyesha kuwa “kumaliza ukimwi  ni uamuzi wa kisiasa na kifedha na nchi pamoja na viongozi wanaofuata njia hizo tayari wameshaona matokeo makubwa. “

Ripoti inasema nchi ambazo ytayari zimeanza kushuhudia mafaikio hayo ni Botswana, Eswatini, Rwanda, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Zimbabwe ambazo tayari zimefikia malengo ya "95-95-95". 

Hiyo ina maana kwamba “asilimia  95 ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi au VVU wamejua hali zao za VVU, asilimia  95 ya watu wanaojua kuwa wanaishi na VVU wanatumia dawa za kuokoa maisha, na asilimia 95 ya watu wanaopata matibabu wamepunguza makali ya virusi vya ukimwi.”

Nchi nyingine 16 zaidi, nane kati yao ziko Kusini mwa Jangwa la Sahara, eneo ambalo linachukua asilimia 65 ya watu wote wanaoishi na VVU, pia zinakaribia kufikia hatua hiyo.

Kutokomeza ukimwi itakuwa ni urithi bora wa viongozi wa sasa

Kwa mujibu wa Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS "Kutokomeza ukimwi ni fursa ya urithi wenye nguvu wa kipekee kwa viongozi wa leo. Wanaweza kukumbukwa na vizazi vijavyo kama watu ambao walikomesha janga kuu la ulimwengu. Wanaweza kuokoa mamilioni ya maisha na kulinda afya ya kila mtu. Wanaweza kuonyesha kile ambacho uongozi unaweza kufanya.”

Ripoti inabainisha kwamba hatua za kupa,mbana na VVU hufaulu wakati zimejikita katika uongozi thabiti wa kisiasa. 

“Hii inamaanisha kufuata takwimu, sayansi, na ushahidi, kukabiliana na ukosefu wa usawa unaorudisha nyuma maendeleo, kuwezesha jamii na asasi za kiraia katika jukumu lao muhimu kwenye hatua za mapambano na kuhakikisha ufadhili wa kutosha na endelevu.”

Ripoti imeongeza kuwa maendeleo yamekuwa makubwa katika nchi na kanda ambazo zina uwekezaji mkubwa zaidi wa kifedha, kama vile Mashariki na Kusini mwa Afrika ambako maambukizi mapya ya VVU yamepungua kwa asilimia 57 tangu 2010.

Upatikanadaji wa dawa za kupunguza makali ya ukimwi

Ripoti inasema shukrani kwa msaada na uwekezaji katika juhudi za kutokomeza ukimwi miongoni mwa watoto, kwani asilimia 82 ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanaoishi na VVU duniani kote walikuwa wakipata matibabu ya kupunguza makali ya ukimwi mwaka 2022, kutoka asilimia 46 mwaka 2010. 

Hii imechangia kupungua kwa asilimia 58 kwa maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto kutoka mwaka 2010 hadi 2022, ikiwa ni idadi ya chini kabisa tangu miaka ya 1980.

Maendeleo katika hatua za kukabiliana na VVU yameimarishwa kwa kuhakikisha kwamba mifumo ya kisheria na kisera haivunji haki za binadamu, bali inawawezesha na kuwalinda. 

Nchi kadhaa ziliondoa sheria hatari mwaka 2022 na 2023, zikiwemo tano  ambazo ni Antigua na Barbuda, Visiwa vya Cook, Barbados, Saint Kitts na Nevis, na Singapore ambazo zimetoa sheria ya kuharamisha mahusiano ya ngono ya jinsia moja.

Idadi ya watu wanaopata matibabu ya kupunguza makali ya VVU duniani kote iliongezeka karibu mara nne, kutoka watu milioni 7.7 mwaka 2010 hadi watu milioni 29.8 mwaka 2022.

Kutokomeza ukimwi hakutokuja kimiujiza

Hata hivyo, ripoti hiyo pia inaeleza kuwa kutokomeza ukimwi hakutakuja moja kwa moja au kimiujiza. 

Ukimwi uligharimu maisha kila dakika mwaka wa 2022. Takriban watu milioni 9.2 bado wanakosa matibabu, wakiwemo watoto 660,000 wanaoishi na VVU.

Imeongeza kuwa “Wanawake na wasichana bado wameathirika kwa kiasi kikubwa, hasa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ulimwenguni kote, vijana wa kike na wasichana 4,000 waliambukizwa VVU kila wiki mwaka wa 2022. Ni asilimia 42 tu ya wilaya zilizo na matukio ya VVU zaidi ya asilimia 0.3 Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa sasa ndizo zinashughulikiwa na mipango ya kujitolea ya kuzuia VVU kwa wasichana barubaru na wanawake vijana.”

Takriban robo moja sawa na asilimia 23 ya maambukizo mapya ya VVU yalikuwa Asia na Pasifiki ambapo maambukizi mapya yanaongezeka kwa kiwango cha kutisha katika baadhi ya nchi. 

Ongezeko kubwa la maambukizi mapya linaendelea katika eneo la Ulaya mashariki na Asia ya kati ambako kiwango kimepanda kwa asilimia 49 tangu 2010 na Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ongezeko ni la asilimia 61% tangu 2010. 

Mwenendo huu unatokana kimsingi na ukosefu wa huduma za kuzuia VVU kwa watu waliotengwa na muhimu ni vizuizi vinavyoletwa na sheria za adhabu na ubaguzi wa kijamii.

Ufadhili wa VVU pia ulipungua mwaka 2022 kutoka vyanzo vya kimataifa na vya ndani, na kurudi kwenye kiwango sawa na mwaka 2013. 

Fedha zilizopugua zilifikia dola bilioni 20.8 mwaka 2022, kati ya jumla ya dola bilioni 29.3 zinazohitajika kufikia 2025.

Kuna fursa ya kutokomeza ukimwi kupitia utashi wa kisiasa

Kwa mujibu wa ripotri kuna fursa sasa ya kumaliza ukimwi kwa kuongeza utashi wa kisiasa kwa kuwekeza katika hatua endelevu za VVU kupitia kufadhili mambo muhimu zaidi kama kuzuia na matibabu ya VVU kwa msingi wa ushahidi, ushirikiano wa mifumo ya afya, sheria zisizo na ubaguzi, usawa wa kijinsia, na mitandao ya kijamii iliyowezeshwa.

Bi Byanyima amesema "Tuna matumaini, lakini sio matumaini tulivu ambayo yanaweza kuja ikiwa yote yangeenda kama inavyopaswa kuwa. Badala yake, ni matumaini yaliyojikita katika kuona fursa ya kufaulu, fursa ambayo inategemea hatua. Ukweli na takwimu zilizojumuishwa katika ripoti hii hazionyeshi kama ulimwengu tayari uko njiani, zinaonyesha kuwa tunaweza kuwa na njia iko wazi."

Mwaka 2022, inakadiriwa kuwa:

• Watu milioni 39.0 duniani kote walikuwa wakiishi na VVU

• Watu milioni 29.8 walikuwa wakipata tiba ya kupunguza makali ya ukimwi

• Watu milioni 1.3 waliambukizwa VVU

• Watu 630 000 walikufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na ukimwi.