Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunatekeleza ibara ya 5 ya Haki za binadamu kwa vitendo: UNFPA Kenya

Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka ishirini aliyezaliwa na virusi vya Ukimwi, hutumia dawa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
© UNICEF/UN0640796/Dejongh
Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka ishirini aliyezaliwa na virusi vya Ukimwi, hutumia dawa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Tunatekeleza ibara ya 5 ya Haki za binadamu kwa vitendo: UNFPA Kenya

Haki za binadamu

Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi na idadi ya watu UNFPA nchini Kenya Anders Tomsen, ameeleza shirika hilo linatekeleza ipasavyo tamko la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu ambalo mwaka huu linafikisha miaka 75 hususan ibara ya Tano ambayo inasema Haki ya mtu ya kwamba asitumbukizwe kwenye vitendo vya mateso, ukatili, au adhabu dhalili.

Akihojiwa na mwandishi wetu wa Kenya Thelma Mwadzaya Tomsen anaanza kwa kusema shirika hilo limeundwa kwa kuzingatia misingi ya haki. 

UNFPA ni shirika lililo na misingi ya haki kila kitu tunachokifanya kinajikita kwenye haki za wanawake, haki za binadamu. Hayo yanajumuisha haki ya kuchagua, haki ya kuepusha vurugu, haki ya kukwepa vitendo vya ukatili na kuhatarisha maisha na haki ya kupata huduma za afya.” 

Ni vipi UNFPA inashirikiana na Kenya kuhakikisa watu wanapata haki zao hususan katika sekta ya afya.? 

“Huduma kamili za umma za afya ni mfumo ambao serikali ya Kenya inataka kuzindua na unajikita katika haki za binadamu na haki ya afya. Sisi kama UNFPA tunaunga mkono ajenda hiyo inayojumuisha haki ya kutoathiriwa na saratani na kujilinda dhidi yake au kuitibu kwa njia bora inapomvamia mtu. 

UNFPA inafahamika kwa shughuli zake za kutetea haki za afya ya uzazi, uzazi salama, uzazi wa mpango, kuzuwia ukatili wa kijinsia na vitendo vya kutishia maisha sasa vipi inajishirikisha na masuala ya saratani?

“Naamini ni muhimu kuisaidia serikali ya Kenya kupunguza idadi ya maambukizi ya saratani na tunayo nafasi maalum kwa jinsi tunavyofanyakazi na serikali kwani tunashirikiana na wahudumu wa jamii kote nchini wakiwemo wakunga na wauguzi. Kwa sasa kila wasiojiweza wakifika kwenye kliniki kwa mara ya kwanza, wanapata fursa ya kukutana na serikali ana kwa ana ni pale wana ujauzito au wanapohitaji huduma za kupanga uzazi. Na hiyo ni fursa mujarab ya kuzungumzia mbinu za kuepuka saratani…. elimu ya saratani… ikiwemo Saratani ya shingo ya kizazi na kupata maelezo kuhusu umuhimu wa kuchanjwa.. . Na pia kuwawezesha baadaye kujua jinsi ya kujikagua ili kutambua ishara za Saratani ya matiti. Hata hivyo Tuko kwenye mkondo wa sawa.” 

Yapi matarajio yenu katika harakati zenu hizo za kutoa elimu kuhusu saratani

“Tuna imani kuwa serikali hii mpya ambayo imeahidi kuajiri wahudumu wa ziada kote nchini katika kila kaunti tutaweza kuwatumia hao kusambaza ujumbe huu muhimu.”