Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusisahau katika kila nyuma ya ukiukwaji wa haki kuna maisha ya mtoto: Gamba

Mtoto akikimbia kupita jengo lililoharibiwa na risasi wakati wa vita akielekea nyumbani kutoka dukani mjini Sirte
© UNICEF/Giovanni Diffidenti
Mtoto akikimbia kupita jengo lililoharibiwa na risasi wakati wa vita akielekea nyumbani kutoka dukani mjini Sirte

Tusisahau katika kila nyuma ya ukiukwaji wa haki kuna maisha ya mtoto: Gamba

Amani na Usalama

Mwaka jana, ukiukwaji mkubwa wa jumla ya vitendo 27,180 ulifanyika dhidi ya watoto waliopatikana katika maenepo ya vita ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa, limeelezwa leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Akiwasilisha ripoti yake ya hivi karibuni ambayo ni ya kila mwaka, Virginia Gamba, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya watoto na migogoro ya kivita, ametoa wito wa "hatua za ujasiri na madhubuti kuchukuliwa ili kuwalinda wavulana na wasichana dhidi ya hatari ya kifo, kuajiriwa, ubakaji na mambo mengine ya kutisha.”

Ripoti hiyo inayojumuisha hali 26 katika maeneo matano duniani kote, ikiwakilisha kiwango kingine cha juu kabisa cha ukiukwaji.

Nchi hizo ni pamoja na Ethiopia, Msumbiji na Ukraine, ambazo zinaorodheshwa kwa mara ya kwanza. 

Hali mpya ni zilizotajwa ni pamoja na Haiti na Niger na maelezo yake yataonekana katika toleo la mwaka ujao la ripoti.

Kuuawa, kusajiliwa jeshini, kutekwa nyara

Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa watoto 18,890 walikabiliwa na ukiukwaji mkubwa wakati wa vita mwaka 2022. 

Takriban watoto 8,630 waliuawa au kulemazwa, wengine 7,622 waliandikishwa na kutumika katika mapigano, na wengine 3,985 walitekwa nyara.

Bi. Gamba amesema ukiukwaji wa aina tatu umebaki kuwa ule uliothibitishwa katika ngazi za juu, na wote ziliongezeka mwaka jana.

Ameongeza kuwa “Watoto waliuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga, kwa silaha za vilipuzi, kwa risasi za moto, kwa kufyatuliana risasi, au mashambulizi ya moja kwa moja. Katika visa vingi, waliangukiwa na mabaki ya silaha za kivita,”.

Virginia Gamba Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya watoto katika mvita vya silaha akitoa taarifa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Loey Felipe
Virginia Gamba Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya watoto katika mvita vya silaha akitoa taarifa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Ubakaji na utumwa wa ngono

Zaidi ya hayo, amesema watoto 1,165, hasa wasichana, walibakwa, kubakwa na genge la watu, kulazimishwa kuolewa au kuingizwa katika utumwa wa kingono, au kushambuliwa kingono. 

Voisa vingine vilikubwa vibaya sana hadi kufikia kiasi cha waathiriwa kufariki Dunia.

Afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza “haja ya kutosahau kamwe kwamba nambari hizi zinawakilisha watoto halisi ambao hadithi zao binafsi hazisimuliki.”

Ametoa mifano kama vile kisa cha wasichana watatu nchini Sudan Kusini waliobakwa na genge kwa muda wa siku tano, msichana wa miaka 14 kutekwa nyara na kuchomwa moto akiwa hai huko Myanmar, na wavulana kuuawa kwa kilipuzi shuleni nchini Afghanistan.

Sura nyuma ya takwimu

Bi. Gamba amesema "Hii ndiyo sababu lazima tukumbuke kwamba nyuma ya takwimu hizo kuna nyuso za watoto wanaokabiliwa na unyanyasaji wa kutumia silaha kote ulimwenguni. Ni lazima tufanye juhudi zaidi kuzuia na kuwalinda watoto wetu kutokana na uharibifu wa migogoro ya kivita.” 

Bi Gamba pia amebainisha kuwa baadhi ya watoto walioathiriwa huadhibiwa kwa hali zao badala ya kupata ulinzi. 

Mwaka jana, watoto 2,496 walinyimwa uhuru kwa madai ya kushirikiana na pande zinazozozana.

"Kwa kuwa katika mazingira magumu zaidi mikononi mwa mamlaka, watoto waliokuwa kizuizini walikabiliwa na ukiukwaji zaidi wa haki zao, ikiwa ni pamoja na mateso na unyanyasaji wa kijinsia. Katika visa vingine, walihukumiwa kifo" amesema.

Shule nyingi nchini Afghanistan zimeathirwa na mzozo wa muda mrefu
©UNICEF/Marko Kokic
Shule nyingi nchini Afghanistan zimeathirwa na mzozo wa muda mrefu

Kushambuliwa kwa shule na hospitali 

Ripoti hiyo pia ilifichua mashambulizi yaliyothibitishwa dhidi ya shule 1,163 na karibu hospitali 650 mwaka wa 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 112 ikilinganishwa na mwaka uliopita. 

Nusu ya mashambulizi haya yalifanywa na vikosi vya Serikali. Alisema utumiaji wa shule na hospitali kwa madhumuni ya kijeshi pia bado ni wasiwasi mkubwa, na kulikuwa na ongezeko kubwa lililothibitishwa la zaidi ya asilimia 60 katika kesi za mwaka jana  na yalifanywa na vikosi vya jeshi na vikundi vyenye silaha.

Mashambulizi dhidi ya huduma za misaada 

Wakati huo huo, amesema wafadhili wa kibinadamu na misaada muhimu wanayotoa mara nyingi ambayo hua ni "tumaini pekee kwa watoto na jamii zilizoathiriwa na migogoro imezidi kushambuliwa.”

Umoja wa Mataifa umethibitisha zaidi ya matukio 3,930 ya kunyimwa huduma za kibinadamu kwa watoto mwaka jana. 

Wafanyakazi wa misaada pia waliuawa, kushambuliwa na kutekwa nyara, huku misaada ya kibinadamu ikiporwa, na mali na miundombinu muhimu kuharibiwa.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), Omar Abdi, pia amelieleza Baraza hilo.

Amekumbusha kwamba idadi kubwa zaidi ya ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto ilithibitishwa katika migogoro ya muda mrefu, ikiwa ni pamoja na katika maeneo kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Israel na Palestina, na Somalia.

Naibu mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Omar Abdi (Kutoka Maktaba)
UN Photo/Loey Felipe
Naibu mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Omar Abdi (Kutoka Maktaba)

Wasiwasi kwa Sudan

Ingawa mzozo wa sasa nchini Sudan ulizuka nje ya kipindi cha kuripoti, UNICEF imesema pia ina wasiwasi mkubwa juu ya athari zake kwa watoto milioni 21 nchini humo.

"Zaidi ya watoto milioni moja sasa wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano na Umoja wa Mataifa umepokea ripoti za kuaminika, chini ya uthibitisho, kwamba mamia ya watoto wameuawa na kujeruhiwa," alisema.

Bwana. Abdi amesisitiza kwamba “ ya Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na migogoro ya vita ni yenye ufanisi, akibainisha kuwa makundi yenye silaha yamewaachilia angalau wavulana na wasichana 180,000 kutoka katika vyeo vyao vya kijeshi katika kipindi cha miaka 23 iliyopita.”

Hata hivyo, amesema "idadi ya nchi kwenye ajenda ya watoto na migogoro ya silaha inavyoongezeka, ndivyo pia idadi ya watoto wanaohitaji ulinzi na msaada wetu wanavyoongezeka", akihimiza uungwaji mkono zaidi wa kimataifa kwa juhudi za Umoja wa Mataifa.

Kulaani vitendo vya kuajiri watoto vitani

Mwakilishi kijana wa kike wa mashirika ya kiraia pia alileta mtazamo kutoka nchi yake ya Colombia, ambayo inajikwamua kutokana na miongo kadhaa ya vita ambavyo vimeacha mamilioni ya waathirika.

Akijulikana kwa jina la Violeta pekee, amesema watoto na vijana huko wanaishi katika hofu ya mara kwa mara ya mabomu ya ardhini, mapigano ya makundi yenye silaha na kuajiriwa kwa lazima na vikundi vyenye silaha.

"Siyo rahisi kuona jinsi siku zinavyosonga, viti darasani vinaanza kuisha kwa sababu wavulana na wasichana wanaandikishwa kwenye makundi yenye silaha, wanauawa au wanafukuzwa, na wanahitaji kwenda mahali pengine kutafuta fursa nzuri," amesema akizungumza kwa lugha ya Kihispania.

Violeta ametoa mapendekezo kadhaa kwa ajili ya kuzingatiwa na Baraza, ambayo ni pamoja na kulaani na kuzuia uajiri wa watoto, na kulaani unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto na vijana kwa kauli kali iwezekanavyo.