“Jiweke katika nafasi ya mtoto ambaye tangu azaliwe Syria hajui amani”- Löfven

9 Julai 2018

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio linalotoa muongozo wa namna ya kulinda haki, usalama na ustawi wa watoto walioko ndani ya mzunguko wa mizozo, pamoja na kuimarisha juhudi za kujenga amani endelevu.

Akihutubia kikao hicho kabla ya kura iliyopitisha azimio hilo, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto kwenye vita vya silaha Virginia Gamba amesema azimio limekuja wakati muafaka kutokana na ongezeko la visa vya utekwaji nyara, uandikishwaji na utumikishwaji wa watoto wa kiume na wa Kike.

Ametolea mfano Somalia ambako watoto 1,600 walitekwa nyara baada ya jamii zao na shule kuvamiwa.

Aidha amesema ongezeko la ukatili kumesababisha kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaouawa ikiwemo huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Iraq na Mynmar, huku kundi la Boko Haram likiendelea kushambulia maeneo ya jamii na kijeshi kwa kutumia watoto kutekeleza mashambulizi ya kujitoa mhanga huko Afrika Magharibi.

Halikadhalika ametoa mtazamo wake katika suala hilo na kusema..

(Sauti ya Virginia Gamba)

"Nimeshtushwa na idadi kubwa ya visa vya ukatili dhidi ya watoto mwaka uliopita 2017 huku visa 21,000 vikiripotiwa na Umoja wa Mataifa ikiashiria kuongezeka kwa idadi ikilinganishwa na mwaka jana. Bi Gamba amesema ukatili huo umesababisha mateso kwa watoto, familia zao na jamii kwa ujumla."

 

Mkuu wa UNICEF Henrietta H. Fore akiwa katika wadi ya watoto mjini Sana'a Yemen
© UNICEF/UN0219817/
Mkuu wa UNICEF Henrietta H. Fore akiwa katika wadi ya watoto mjini Sana'a Yemen

Akizungumza baada ya kupitishwa kwa azimio hilo Mkurugenzi Mkuu wa Shirikla la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Henrietta H. Fore amesema...

(Sauti ya Henrietta H. Fore)

“Iwapo tutashindwa kuzuia ukatili dhidi ya watoto leo, tutakuwa tumeshindwa kuzuia ukatili dhidi ya watoto kesho. Watoto wa sasa watakuwa wakiona vurugu na ukatili kama kitu cha kawaida, kinachokubalika, kisichokwepeka. Fikiria mtoto ambaye amekua akijua vita tu maishani mwake, kwa mfano mtoto wa miaka saba kutoka Syria hajawahi kuona Syria yenye amani. Barubaru wa Afghanistan hajawahi kuona Afghanistan yenye amani. Tafakari yale watoto kutoka Sudan Kusini wameyapitia, na wanaendelea kushuhudia wakati wakisherehekea mwaka wa saba tangu uhuru w anchi yao leo.”

Kwa upande wake waziri mkuu wa Sweden,Stefan Löfven amesema kuna watoto milioni 357 katika mizozo akisema , “hiyo inaonyesha kushindwa kwa dunia nzima.”

Ameongeza kuwa hata kama dunia haiwezi kukubaliana katika kila jambo ni lazima kukubali kwamba kila mtoto ambaye yuko katika mazingira ya vita ni udhaifu na hilo linahitaji kubadilishwa.

Sweden inashikilia urais wa Baraza la Usalma kwa mwezi huu na ndio mfadhili wa azimio hilo lililopitishwa hii leo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter