Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunajikita kwenye kinga badala ya tiba ili kulinda watoto kwenye mizozo- Bi. Gamba

Watoto wakicheza kwenye moja ya kambi za wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
© UNICEF/Gwenn Dubourthoumi
Watoto wakicheza kwenye moja ya kambi za wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Tunajikita kwenye kinga badala ya tiba ili kulinda watoto kwenye mizozo- Bi. Gamba

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema mwelekeo wa matukio ya ukatili kupita kiasi dhidi ya watoto kwenye maeneo yenye mizozo kwa mwaka uliopita wa 2022 utaendelea kuwa sawa na mwaka 2021 ambapo zaidi ya matukio 24,000 ya ukatili dhidi ya watoto yalithibitishwa kutekelezwa.

Kauli hiyo ni ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto walio kwenye maeneo ya mizozo, Virginia Gamba, aliyoitoa leo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mjadala wa ngazi ya juu kuhusu Watoto na Mizozo: Uzuiaji wa Ukiukwaji wa kupitiliza.

Bi. Gamba katika hotuba yake yenye kurasa tano ametaja aina ya vitendo vya kikatili kupita kiasi ambavyo watoto hao walikumbana navyo ni  kuuawa, kukatwa viungo na kuachwa na ulemavu, utumikishwaji vitani pamoja na kunyimwa huduma za kiutu pamoja na kutekwa nyara.

Kinga ni bora kuliko tiba

Bi. Gamba amesema wakati huu ambapo wanaanda ripoti ya mwaka 2022, wameona ni vema hatua ya kurekodi matukio iende sambamba na hatua za kuzuia.

“Kuweka rekodi ya matukio ya ukiukwaji na unyanyasaji pamoja na kuyathibitisha ni hatua muhimu za awali za kuelewa hali ya watoto kwenye mizozo ya kivita na mashinani. Hata hivyo kutokana na matukio haya kujirudiarudia kwa sababu ya mizozo na ghasia, na mazingira kuwa magumu, tunazidi kuelewa kuwa ni muhimu zaidi kutambua mapema vihatarishi na uhatari ambamo kwao watoto wamo ili kuepusha ukiukwaji wa haki kutokea pindi vita inapoanza,” amesema Mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu kwa watoto walio kwenye mizozo ya kivita.

Mtoto akichungulia kutoka kwenye nyumba yao iliyo kama pagala kwenye eneo lenye hatari zaidi huko Al Gamalia nchini Yemen
© UNOCHA/Giles Clarke
Mtoto akichungulia kutoka kwenye nyumba yao iliyo kama pagala kwenye eneo lenye hatari zaidi huko Al Gamalia nchini Yemen

Nini kinafanyika hivi sasa

Bi. Gamba amesema ofisi yake ina mbinu bora na mipango katika ngazi mbalimbali za kulinda watoto dhidi ya ukatili uliopitiliza kwenye maeneo ya vita.

Amesema uthabiti wa mbinu hizo ni mashauriano baina ya pande kinzani kwenye mizozo yaliyoibua mamia ya ahadi ikiwemo mipango ya utekelezaji 41 iliyopitishwa na pande kinzani tangu kuanzishwa kwa ofisi yake mwaka 1996.

“Hivi karibuni, ofisi yetu imesaka kuimarisha kinga, na ilipatiwa nguvu zaidi na azimio namba 2427 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na tumeandaa mipango ya pamoja yak inga na serikali. Leo Baraza la Usalama linatupatia fursa ya kutathmini azimio hilo namba 2427 na linapaswa kutupatia msaada na uwezo wa kulitekeleza zaidi.”

Mipango ya kuzuia imeshaandaliwa

Ametaja Ufilipimo kuwa tayari imeandaa mipango ya kuzuia ukiukwaji wa haki za watoto kwenye maeneo ya mizozo huku akisema, “tunashauriana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Colombia, Mali na Sudan kuandaa ahadi zaidi za kuzuia ukiukwaji wa haki za watoto kwenye mizozo.”

Ametanabaisha kuwa kwa Sudan Kusini na Yemen, mipango yao ya utekelezaj ina vipengele vya kinga.

Hata hivyo amesema hatua zaidi zinatahijika katika kuandaa mikakati katika ngazi ya kitaifa ili kuwa na mpango wenye mtazamo mmoja wa kuweka kinga badala ya tiba.

Halikadhalika amesema ofisi yake imeimarisha ubia na ofisi ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto ili kutatua kwa ubora zaidi ghasia, kubashiri kabla hazijatokea, wakati na baada ya mzozo ili kuweza kuvunja mzunguko wa ukatili huo kwa watoto.

“Katika kutekeleza hilo tutahakikisha watoto sauti zao zinajumuishwa kwa kuwa majawabu endelevu ni yale ambamo kwayo watoto wenyewe wanachangia kupatikana,” amesema Bi. Gamba.