Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji na utekaji nyara wa watoto kwenye maeneo ya vita vilishamiri mwaka 2021- Ripoti

Watoto wakimbizi wa ndani huko Ituri nchini DRC.
UN/Eskinder Debebe
Watoto wakimbizi wa ndani huko Ituri nchini DRC.

Mauaji na utekaji nyara wa watoto kwenye maeneo ya vita vilishamiri mwaka 2021- Ripoti

Amani na Usalama

Mwaka wa 2021  umeshuhudia mchanganyiko wa mwendelezo hatari wa mizozo, mapinduzi ya kijeshi sambamba na mizozo mipya na ile iliyodumu muda mrefu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa, vyote ambavyo kwa pamoja vimekuwa na madhara makubwa kwa watoto duniani kote, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ripoti yake ya mwaka kuhusu Watoto kwenye mizozo ya kivta, ripoti ambayo imechapishwa hii leo.

Guterres amesema, “mapigano baina ya nchi hasa katika bonde la Ziwa Chad na maeneo ya Sahel ya Kati pamoja na mapigano ya kikabila yamekuwa na madhara makubwa kwa watoto.”

Kiwango cha madhara na aina ya matukio

Ripoti inaweka bayana kuwa takribani watoto wa kike 5,242  na wavulana 13,663 walidhurika na ukiukwaji mkubwa katika nchi 21 na eneo moja. Matukio 23,982 yalithibitishwa, kiwango ambacho haikina tofauti na mwaka 2020 ikimaanisha kuwa kila sikukulikuwa na matukio 65.

“Cha kusikitisha ni kwamba asilimia 15 ya matukio hayo, watekelezaji hawakutambuliwa hali inayosababisha suala la uwajibishwaji kuwa ndoto,” imesema ripoti hiyo.
Ripoti inasema watoto waliuawa, walikatwa viungo huku wengine wakitumikishwa vitani na hata kunyimwa haki ya kupata huduma za kibinadamu.

Maeneo ambako watoto walikumbwa zaidi na matukio hayo ni Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Israel na eneo inalokalia la waplestina, Somalia ,Syria na Yemen.

Kauli ya Mwakilishi wa Guterres

Virginia Gamba, ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto walio kwenye maeneo ya mizozo anasema ,"hakuna neno la kutosha la kuelezea mazingira ya kutisha kwenye mizozo ambayo watoto wanapitia. Manusura wanakuwa wameathirika maisha yao yote. Wakisalia na makovu ya kimwili, kiakili na kihisia.”

Hata hivyo amesema “takwimu hizi zisitukatishe tamaa. Zinapaswa kuwa kichocheo cha kusongesha azma yetu ya kutokomeza na kuzuia ukiukwaji mkubwa wa haki za awatoto. Ripoti hii inatoa wito wa hatua zaidi kulinda watoto kwenye mizozo na kuhakikisha wanapata fursa halisi ya kuibuka na kustawi.”

Akigusia takwimu ya watoto 8,070 kuuawa au kuachwa na ulemavu, Bi. Gamba ametoa wito kwa pande kwenye mizozo, iwe serikali au vikundi vya kiraia vilivyojihami, kupatia fursa wataalamu wa ulinzi wa watoto na usaidizi wa kibinaamu wafanya kazi yao ya kulinda watoto kwenye mizozo.

Suala la kijinsia katika haki za watoto kwenye mizozo

Watoto wa kike walikumbwa na madhara zaidi kwenye ambapo idadi ya waliodhurika ni asilimia 30 ya watoto wote.

Katika eneo la bonde la Ziwa Chad, kulikuwa na ongezeko la idadi ya watoto wa kike ambao waliathirika ambapo Bi. Gamba anasema, “wavulana na wasichana wanaathirika tofauti kwenye mizozo na ripoti ya mtazamo wa kijinsia katika ukijaji wa haki za watoto iliyochapishwa na Ofisi yangu mwezi Mei mwaka 2020 inaonesha umuhimu wa kuelewa vyama mtazamo wa kijinsia katika ukiukwaji wa haki za watoto kwenye mizozo ili mikakati nah atua zetu iweze kuwa na majawabu sahihi.”

Vitendo vilivyoongezeka zaidi ni utekaji nyara na ubakaji na vimeongezeka kwa asilimia 20. Mashambulizi dhidi ya shule na hospitali pia viliongezeka..

Shefuka, mwenye umri wa miaka 9 akijisomea nyumbani kwa msaada wa mama na mwalimu wake, wakati huu ambapo kituo cha kujisomea kwenye kambi ya wakimbizi warohingya kimefungwa.
© UNICEF
Shefuka, mwenye umri wa miaka 9 akijisomea nyumbani kwa msaada wa mama na mwalimu wake, wakati huu ambapo kituo cha kujisomea kwenye kambi ya wakimbizi warohingya kimefungwa.

Licha ya takwimu za kutisha kuna mafanikio

Ripoti inasema kuwa licha ya takwimu hizo za kutisha za mwaka 2021, kuna nuru katika baadhi ya maeneo.

Mathalani watoto 12,214 waliachiliwa huru na makundi yaliyojihami ikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Colombia, DRC, Myanmar na Syria.

Bi. Gamba amekumbusha kuwa watoto wanaochiliwa huru wanapaswa kunufaika na misaada endelevu ya kuwajumuisha kwenye jamii, hatua ambazo zinapaswa kuzingatia umri wao, jinsia na ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia mipango ya muda mrefu ya kujumuisha tena watoto kwenye jamii.

Mafanikio mengine ni Umoja wa Mataifa uliongoza mazungumzo yaliyokuwa na nuru na pande kinzani huko Nigeria, Ufilipino, Sudan Kusini na Yemen.

Hata hivyo kuna maeneo mapya ambayo sasa yamejumushwa kuwa hali ya watoto inatia hofu na hivyo yatamulikwa kwa kina na maeneo hayo ni Ethiopia, Msumbiji na Ukraine.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu amesema, “pindi amani inapotoweka, watoto ndio wa kwanza kulipa gharama na hivyo amani lazima iwepo kwa kuwa ndio njia pekee endelevu ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto kwenye mizozo.”